Watu?28 wamekufa?papo hapo na?wengine 15 kujeruhiwa baadhi yao vibaya baada ya lori walilokuwa wakisafiria kupinduka eneo la Biharamulo, mkoani Kagera.
Ajali hiyo ilitokea jana saa 12:00 asubuhi wakati lori hilo aina ya Isuzu lenye namba za usajili T655AJQ likitoka eneo la Mganza, wilayani Biharamulo?kwenda Wilaya ya Kibondo, mkoani Kigoma.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Bw Ignas Mbinga, alisema gari hilo liliondoka Muganza?juzi saa 7:00 usiku na kupata ajali baada ya kufika eneo la Lusahunga wakati likiingia katika barabara ya lami itokayo Isaka-Rusumo.
Kamanda Mbinga alisema kati ya marehemu hao, 19 ni wanaume na tisa ni wanawake na kwamba 16 wametambuliwa baadhi kwa jina moja na 12 hawajatambuliwa.
Aliwataja waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni Albert Felician Buchwa, mkazi wa Biharamulo,? Daya Pande, mkazi wa Kibondo, Kigoma, George mkazi wa Kibondo, Salehe Mkanza ,mkazi wa Chato na Nyupe Iddi Salisali, mkazi wa Kibondo.
Wengine ni Maduhu Milongo, mkazi wa Biharamulo, Danford, mkazi wa Kibondo, Bitwae Michael, mkazi wa Kalenge, Biharamulo, Omari Kitwe, mkazi wa Kibondo na Mama Chami (28), mkazi wa Kibondo.
Wengine ambao hawakujulikana mahali wanakotoka ni Ezra, Mama Latifa, Shukuru Mtuma, Joyce, Projest Fransisco, Mathayo Luhongo na Shipaye Kalula.
Kamanda Mbinga alisema miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika hospitali teule ya Kibondo.
Aliwataja majeruhi wa ajali hiyo kuwa ni Joseph Moses (26), mkazi wa Nyaruyoba Kibondo, Tani Bintosho (33), mkazi wa Kibondo, Amri John (30), mkazi wa Kasulu, Abdallah Kabakule (29), mkazi wa Kibondo mjini, Jumanne William (26), mkazi wa Kasulu, Swaib Mikidard (29), mkazi wa Kigoma Mjini na Ndelabakula Ngoliki (30), mkazi wa Kakonko.
Majeruhi wengine ni Emmanuel Gwiluko (27), mkazi wa Kakonko, Kibondo, Mariki Kasindi (30), mkazi wa Makere, Kasulu, Baraka Revocatus (20), mkazi wa Kibondo, Issa, mkazi wa Kibondo, Matendo Gervas (30)? na Yotham Gervas, wakazi wa Kumshinde Kibondo mkoani Kigoma.
Wengine ni Jumanne Masese (19) na Tatu Shimba, wakazi wa Ushirombo wilayani Bukombe, mkoani Shinyanga.
Kamanda Mbinga alisema majeruhi hao wamelazwa katika hospitali ya Wilaya ya Kibondo kwa matibabu na kwamba hali zao zinaendelea vizuri isipokuwa? mtu mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Issa, hali yake ni mbaya.
Kamanda Mbinga alisema abiria wengine waliokuwa ndani ya gari hilo ambao hawakujeruhiwa sana, hawakufahamika majina yao kutokana na dereva na utingo wake kutoroka baada ya ajali hiyo.
Dereva wa gari hilo alisema alikuwa ni Baraka Kafunguku (34) na utingo wake Ndalivamali Ngunda, mkazi wa Kibondo.
Kamanda Mbinga alisema lori hilo linakadiriwa kuwa lilibeba zaidi ya abiria 50 wengi wao wakiwa ni wafanyabiashara wakiwemo wa dagaa waliokuwa wakienda Kibondo.
Alisema chanzo cha ajali hiyo kinasadikiwa kuwa ni mwendo wa kasi na kwamba dereva wa gari hilo anashikiliwa na polisi wilayani Biharamulo kwa tuhuma za kusababisha vifo vya abiria hao.
Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete, amemtumia salamu za rambirambi Mkuu waMkoa wa Kagera, Bw. Enos Mfuru kufuatia vifo vya watu hao 28 vilivyotokana na ajali hiyo ya lori.
Katika barua yake kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Rais Kikwete alisema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kusikitisha ya ajali mbaya ya gari iliyotokea jana asubuhi huko Lusahunga na kusababisha vifo vya Watanzania 28 na wengine 13 kujeruhiwa.
’’Ni wazi kuwa vifo hivyo vitakuwa vimeathiri maisha ya watu wengi. Watanzania hao waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni baba, mama, kaka na dada katika kaya fulani,’’ alisema.
Rais Kikwete aliongeza kuwa, ni wazi kwamba, vifo hivyo vitakuwa vimesababisha kuyumba kwa familia ambazo zimepoteza wapendwa wao.
Aidha, alisema vifo hivyo si tu vimepoteza wakuu wa kaya, lakini pia vimepunguza nguvu kazi katika Taifa letu.