Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Lowassa atishia maisha makampuni ya madini
Lowassa atishia maisha makampuni ya madini
By Habari Tanzania | Published  11/29/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI Mkuu, Edward Lowassa, amezionya kampuni za madini, akisema ustawi wake nchini utatokana na namna zinavyochangia katika ustawi wa jamii.

Alisema iwapo wananchi wataona kuwa wanadhulumiwa rasilimali zao, ustawi wa makampuni hayo utakuwa mashakani na akayataka kulichukulia kwa uzito suala hilo.

Lowassa aliyasema hayo jana katika mkutano kuhusu Maliasili na Maendeleo ya Kiuchumi ya Afrika: Wajibu wa Canada katika Karne ya 21, unaohudhuriwa na wawakilishi kutoka serikali mbalimbali za nchi za Afrika na makampuni ya uwekezaji ya Canada.

Aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa hali ya sasa ambapo inaonekana kuwa wenye rasilimali hizo hawanufaiki nazo, haikubaliki.

“Ni kweli kwamba wanatakiwa kupata mapato kwa ajili ya wenyehisa wao, lakini mikataba itakayowezesha kupatikana kwa mapato hayo itakuwa endelevu tu endapo nchi za Afrika na wananchi wake wataona kuwa wao pia wanapata manufaa yanayostahili kutokana na uchimbaji wa madini,” alisema.

Mwandishi wa Waziri Mkuu, Said Nguba, anasema kuwa baadhi ya washiriki wa mkutano waliohojiwa walisema tamko hilo la Lowassa, ambaye anahudhuria mkutano huo kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete, ni zito kutoka kwa kiongozi wa nchi za Afrika mbele ya wawekezaji wakuu katika madini wa Canada.

Kumekuwa na malalamiko nchini Tanzania na katika nchi nyingine za Afrika kuwa madini yanayochimbwa katika bara hili yanawanufaisha wawekezaji kutoka nje tu na kwamba Waafrika wanaachiwa mashimo.

Lowassa aliongeza kuwa Afrika ina haki ya kuhakikisha maliasili yake inachangia katika maendeleo ya kiuchumi ya bara hilo, kama vile ambavyo inawajibika kuhakikisha kuwa wawekezaji nao wanapata wanachostahili.

“Changamoto ambayo kila kiongozi wa nchi ya Afrika anakabiliana nayo ni jinsi gani ya kuifanya mali asili nyingi ambayo Afrika imejaliwa nayo, iwe ndiyo injini ya kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi zetu,” alisema.

Waziri Mkuu pia alisema kwa Canada na nchi ningine tajiri zinazowekeza Afrika, Wafrika wanahitaji nchi hizo zitoe tamko la dhati kuhakikisha kuwa makampuni ya madini kutoka katika nchi hizo, katika utendaji wao, yatakabiliwa na viwango vile vile vya uwajibikaji wakati yanawekeza katika Afrika kama ilivyo katika nchi zao.

Alisema nchi tajiri zinatakiwa kwenda mbele zaidi na kuhakikisha kuwa shughuli za madini zinazofanywa na makampuni yao katika Afrika zinahusishwa na mipango ya kitaifa ya uchumi ya nchi za Afrika na jamii zilizo kwenye maeneo ya uchimbaji.

“Kama fedha za misaada zitaelekezwa katika kusaidia jitihada za serikali za nchi za Afrika katika eneo hili, zitakuwa zinazisaidia nchi za Afrika kwa heshima, kwa kutumia maliasili zake zenyewe, badala ya kuendelea kutegemea fadhila za wengine,” aliongeza.

Lowassa alisema wanataka kampuni za madini kuajiri zaidi Watanzania; kuwa wazi katika ununuzi na huduma huku zikisaidiana na serikali kuwasaidia wauzaji wa ndani na kwamba, inatakiwa kubainisha maeneo yenye udhaifu na kuziba mianya hiyo.

Alisema wataendelea na majadiliano na makampuni ya madini hadi itakapobainika kuwa pande zote zinazohusika zinanufaika na kukemea uvunaji holela wa rasilimali za Afrika na kuiacha Afrika katika lindi la umaskini.

“Kama siyo hivyo, almasi ya Afrika ikiendelea kuboreshwa nje ya bara, hasa Ubelgiji na Israel, kunawafanya watu wake kuwa matajiri na Afrika kubaki maskini,” alisema Lowassa.

Lowassa, alisema Afrika ni kwa rasilimali nyingi ambazo zikimilikiwa vizuri na kukataa mirija inayonyonya kwa kigezo cha kuongeza ubora, zinaweza kuifanya Afrika kuwa tajiri.

"Kama kuna muda wa kufanya rasilimali za Afrika ziinufaishe ni sasa…nchi nyingi za Afrika zimeboresha sera za uwekezaji, mabunge na vivutio. Nyingi zimeimarisha utawala bora, siasa na uchumi. Migogoro imemalizika. Uwekezaji katika miundombinu na mahitaji mengine yameongezwa, huku nyingine zikizingatia uchumi mdogo ili kupunguza wigo wa matajiri,” alisema.

Alisema anaamini nchi zilizoendelea zina wajibu wa kuhakikisha kampuni zinazowekeza Afrika zinaondokana na kupigwa faini na vikwazo, kwa kuongeza uchangiaji wa huduma za jamii ambazo zimo ndani ya nchi hizo na kwamba, zitatakiwa kusaidia Afrika kujenga uwezo wa kuratibu rasilimali.

Waziri Mkuu, alisema Rais Jakaya Kikwete alitaka kuhudhuria mkutano huo, lakini akatingwa na kazi nyingi za kitaifa na kimataifa na kwamba, sababu za kutaka kuwepo kwake ni kutokana na Tanzania kuwa na rasilimali nyingi ambazo zinaweza kutumika kutokomeza umaskini.

Lowassa, alisema wanajaribu kujifunza mikakati ya jinsi rasilimali zinavyoweza kukuza uchumi wa taifa kutoka kwa mataifa yaliyoendelea kama Canada ambalo ni taifa lenye nguvu kwa nishati inayotokana na madini, mafuta, gesi na rasilimali na kwamba lina historia ndefu ya utafutaji wa madini.

Sababu nyingine ambayo ilikuwa imfanye Rais Kikwete kuhudhuria mkutano huo, Lowassa alisema, ni kutokana na ahadi alizotoa wakati wa kampeni kuwa atajadiliana na kampuni za migodi ili kurekebisha mikataba na sera ya madini, kauli ambayo inajenga uadui dhidi ya wawekezaji hao.

"Kwa sababu Canada ina kampuni kubwa zilizowekeza Tanzania kwenye madini na nishati, tumekuja kwenye mkutano huu kuwahakikishia hali ilivyo na itakavyokuwa baadaye nchini mwetu, kuwa hakuna hatari ya uwekezaji ambayo inaweza kuharibu heshima yetu tuliyojiwekea kuwa ni kituo salama cha uwekezaji,” alisema Lowassa.

Tangu mwaka 1995, Tanzania imeongeza mauzo ya madini nje ya nchi kwa asiliamia 0.07 hadi 42.4 mwaka 2005, huku mchango wa madini kwa pato la taifa (GDP) ukipanda kutoka asilimia 1.4 mwaka 1995 hadi 3.5 mwaka jana.

Lowassa, alisema licha ya mafanikio yaliyopatikana, wanakabiliwa na changamoto za kuhakikisha nchi inanufaika na sekta ya madini, kujenga uwezo wa wauzaji wa bidhaa na huduma katika kampuni, kuongeza ubora wa madini ndani ya nchi na kuendeleza miundombinu kwenye maeneo yenye migodi.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by Njimba)
    Rating
    Well done Lowassa, the message is clear, is time we benefit from the minerals. The question remains who entered on these unfair contracts? I believe they are our brothers and sisters. Any action against them? I they not still in the same office?
    Njimba.
     
Submit Comment


Article Options
This article has been added to your 'Articles to Read' list.
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.