Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Serikali yatangaza kufunga makambi ya wakimbizi kibondo
http://www.habaritanzania.com/articles/2063/1/Serikali-yatangaza-kufunga-makambi-ya-wakimbizi-kibondo
By Prosper Kwigize
Published on 11/27/2006
 
erikali wilayani Kibondo imeagiza kufungwa kwa makambi matatu ya wakimbizi wilayani humona kuwaweka wakimbizi wote katika kambi moja kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma na usalama.

Na Mwandishi wa HabariTanzania.com, Kibondo

* Ni ndani ya siku tisa tu, wakimbizi watembee kwa mguu kuhama kambi

* Mashirika yanayowahudumia yaonesha kupinga agizo hilo

* Wakimbizi wadai kuwa kuswagwa kwa miguu ni kinyume cha haki za binadamu


Serikali wilayani Kibondo imeagiza kufungwa kwa makambi matatu ya wakimbizi wilayani humona kuwaweka wakimbizi wote katika kambi moja kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma na usalama.

Agizo hilo limetolewa na mkuu wa wilaya ya Kibondo luteni kanal John Mzurikwao katika walaka wake kwa wakuu wote wa mashirika yanayohudumia wakimbizi na nakala yake kupatikana kwa vyombo vya habari.

Katika walaka huo uliogongwa mhuri wa siri, mkuu huyo wa wilaya ameyataja makambi yanayotakiwa kufungwa kuwa ni Mtendeli, Kanembwa na Mkugwa, na kwamba mwisho wa zoezi hilo ni tarehe 19 mwezi desemba.

Luteni kanali Mzurikwao ameagiza wakimbizi wote wanaotakiwa kuhama kutoka katika makambi yao kwenda katika kambi ya Nduta watatakiwa kutembea kwa mguu, na ameyataka mashirika kupeleka misaada yake katika kambi ya Nduta kuanzia tarehe 10 mwezi ujao.

Ametaja idadi ya wakimbzi watakaohamia katika kambi ya Nduta kuwa ni 31,526 ambapo kati yao watakaotoka kambi ya Kanembwa ni 11,699, kambi ya Mtendeli 19,827 na kutoka kambi ya Mkugwa wapo wakimbizi 2,503.

Aidha serikali imeagiza uvunaji wa miti kwa ajili ya ujenzi wa nyumba mpya ambapo misitu iliyoko pembezoni mwa barabara kuu toka maragalasi hadi moyowosi itavunwa kwa umbali wa mita hamsini.

Hata hivyo agizo hili limepokelewa kwa mtazamo tofauti na mashirika yanayohudumiwa wakimbizi na wengi wao wamehoji uharali wa agizo hilo huku wengine wakisema kuwa huo ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

Baadhi ya wakimbizi waliotoa maoni yao wamesema hawatakuwa tayari kutembea kwa miguu na mizigo yao pamoja na watoto kutoka katika makambi yao na kwenda katika kambi ya Nduta ambapo ni zaidi ya kilomita 80.

Wilaya ya Kibondo kwa sasa ina jumla ya makambi ya wakimbizi manne ambapo endapo yatafungwa wilaya itabaki na kambi moja ya Nduta itakayo kuwa na jumla ya wakimbizi hamsini na nne elfu na mia moja (54100).

Mashirika yanayotoa huduma kwa wakimbizi ambayo yameagizwa na serikali kuhamasisha uhamasishaji wa kufungwa kwa makambini UHNCR, UNICEF, UNWFP, TWESA, TCRS, JRS, SAEU, IRC, REDESO, ICRS na FILM AID