Maneno hayo hapo chini toka kwa msimamizi wa mkutano, Msangi Mdogo, ndio yaliyofungua mkutano wetu rasmi:
NA SASA NAFUNGUA KIKAO RASMI KWA KUWAKARIBISHA NYOTE MLIOBAHATIKA KUHUDHURIA MKUTANO HUU WA KWANZA NA WA AINA YAKE KATIKA HISTORIA YA NCHI YETU. KWA WALE WALIOKO NYUMBANI TANZANIA ULIPEWA NAFASI KIDOGO KATIKA GAZETI LA MAJIRA LEO
KUNA DAKIKA MBILI KABLA YA MKUTANO KUANZA RASMI, NAOMBA TUJIPANGE KWENYE NAFASI ZETU TAYARI KWA MKUTANO
Baada ya hapo mkutano ulianza na kuendelea vyema hadi mwisho. Kuna wajumbe ambao walipata tatizo la kuingia ukumbini, nawapa pole. Naamini mkutano ujao utaboreshwa zaidi. Shukrani zimwendelee ndugu Mike Mushi “Mzee wa Mlango wa Uani” ambaye aliweza kubomoa ukuta na kuweka mlango wa uani uliowawezesha wajumbe waliokuwa na matatizo ya kuingia waweze kuingia kupitia mlango huo. (bonyeza hapo chini umalize kusoma habari hii)
Mambo yalijadiliwa kwa kirefu. Ninachofanya hapa ni kuandika maamuzi makubwa yaliyofikiwa. Siku zinavyokwenda nitakuwa naweka mambo mengine yaliyozungumziwa ili tuwe tunayafikiria (maswali ambayo hayakujibiwa, mawazo yanayohitaji kutafakariwa, na kadhalika.)
1. Mikakati ya Kufikisha Ujumbe wa Wanablogu kwa Watu Wengi Zaidi:
- kuwe na safu magazetini ya “Yaliyojiri kwenye Blogu”
- kushawishi redio kupitia habari kuu ndani ya blolgu wakati wa uchambuzi wa habari za magazetini (kama jinsi baadhi ya redio [hata luninga hufanya hivi) zinavyosoma habari zilizo katika magazeti asubuhi)
- kuwapa somo wahariri wa magazeti kuhusu blogu na faida zake
- Mike Mushi wa HabariTanzania.com ataweka kona ya “Yaliyojiri Kwenye Blogu” katika tovuti ya HabariTanzania.com
- Magazeti ambayo yanaelekea kuwa tayari au kuwa na watu ambao ni rahisi kushawishi kuwe na safu ya “Yaliyojiri Kwenye Blogu” ni Majira (ambao walikuwa na habari kuhusu mkutano wetu), Mwananchi, na Tanzania Daima
- Redio: ilitajwa Clouds FM na watu kadhaa kujitolea kufuatilia
2. Maadili:
- Mjadala huu utaendelezwa maana ni mpana sana
- Ila wajumbe wengi walionekana kukukubaliana kuwa kuna umuhimu wa kuwa na maadili, kutunza heshima na utu wa Kitanzania
- Kuwe na lugha safi, tusitumie blogu kulipiza kisasi, kuweka picha chafu, kudhalilisha, n.k.
- Ikapendekezwa kuwa pengine kuwe na kamati ya ushauri wa masuala ya maadili
- Kimsingi suala hili bado linahitaji mchango wa wanachama na muda unahitajika wa kutafakari
- Tukiwa na jumuiya wanachama itabidi wakubaliane na nguzo za kimaadili tutakazozipitisha ili wawe ni sehemu ya jumuiya hiyo
- Azimio la Dodoma lipandishwe kwenye ukurasa wetu wa wiki na kuboreshwa zaidi
3. Jumuiya:
- Tunataka jumuiya ili kufanikisha kazi tunazofanya, ili tuwe na mwelekeo sahihi wa kututambulisha
- Tuanze na jumuiya ya mtandaoni, iwapo kutakuwa na ulazima huko baadaye tunaweza kuisajili kama Shirika Lisilo La Kiserikali
- Jumuiya hiyo itakuwa na tovuti
- Jumuiya itatakuwa na kikusanya habari (aggregator) kitakachotoa habari za wanablogu kila wanapoandika (hii pamoja na faida nyingine itasaidia waandishi wa habari na watangazaji kupata habari za kutumia katika safu na vipindi vya “Yaliyojiri Kwenye Blogu”
4. Uongozi:
Kuna mambo kadhaa ambayo yalionekana kuwa yasingeweza kumalizwa katika kipindi kile kifupi cha mkutano. Hivyo mkutano uliamua kuchagua kamati ya mpito/viongozi wa muda. **Napenda kusisitiza kuwa hawa ni viongozi wa muda.**
Viongozi hao ni: Da’ Mija (mwanamke wa shoka), ndesanjo macha, Jeff Msangi, na Msangi Mdogo.
Kati ya kazi walizonazo viongozi hawa wa muda ni kukusanya mawazo ya wanachama kuhusu aina ya jumuiya tunayoitaka na muundo wake, aina ya uongozi utakaofaa, jina la jumuiya hiyo, jina la kikusanya habari (aggregator), masuala ya ujenzi wa tovuti ya jumuiya, mfumo wa kutoa tuzo kila mwaka, aina za tuzo, namna ya kuchagua blogu za kutuzwa, n.k.
Wajumbe walipitiwa kidogo maana hawakutoa muda wa kamati hii kufanya kazi. Nadhani ni vyema kamati ikajua kuwa ina muda gani wa kufanya kazi zake. Maana unajua tena, kamati ya mpito mara imekuwa ya kudumu!
Pia kuna mjumbe ambaye huenda akaweka pingamizi dhidi ya uongozi huu wa muda! Tamba amemtaka awasiliane naye ili amuunganishe na kaka yake ambaye ni mwanasheria. Mjumbe mwingine akampa siku 21 kuwa awe ameshaweka pingamizi lake hilo la alipe elfu hamsini! Pengine anaweza pia kuwasiliana na Mrema ambaye ana uzoefu wa masuala ya kupinga uchaguzi!
5. Siku ya Blogu Tanzania:
- baada ya majadiliano marefu na kura kupigwa iliamuliwa rasmi kuwa TAREHE 18 MWEZI WA KUMI NA MOJA (NOVEMBA) itakuwa ndio Siku ya Blogu Tanzania kila mwaka. Siku hiyo ndio pia siku ambayo tuzo za blogu zitatolewa.
- Siku hii ilichaguliwa kwa kuwa ndio siku ambayo mkutano wa kwanza rasmi wa wanablogu wa Tanzania ulifanyika
Mkutano ulimalizika salama. Msimamizi aliaga kwani alitakiwa kwenye kikao cha harusi (unajua tena mambo ya vikao vya harusi!) na baadhi ya wajumbe walibaki ukumbini wakiendelea na mazungumzo baada ya mkutano.
Naamini kuwa huu ni mwanzo mzuri sana wa kujenga jumuiya madhubuti na kuelimisha watu wengi zaidi kuhusu teknolojia ya blogu na dhana nzima ya uandishi wa raia na pia kuwezesha watu wengi zaidi kupata habari tunazoandika.
Utaona kuwa habari zetu zikianza kutolewa magazetini kwenye safu ya “Yaliyojiri Kwenye Blogu” na pia kusomwa redioni na hata kwenye luninga, suala la kuwa tunayoandika bloguni ni kwa wale tu wenye uwezo wa kuingia kwenye Intaneti au walioko mijini litakuwa limepatiwa ufumbuzi fulani. Ghafla utakuta Mtanzania aliyeko kijijini na redio yake atakuwa akipata elimu na habari zilizoko bloguni kupitia redio yake (ingawa hana kompyuta).
Magazeti hutafuta habari na picha. Kuna nafasi nzuri na ya pekee kwa magazeti haya kupata habari na picha toka katika blogu zetu. Tazama, kwa mfano, picha zilizoko kwa Maggid Mjengwa. Ni gazeti gani halitapenda picha zile? Hakuna sababu yoyote ya magazeti kutotumia picha zile (kwa idhini yake). Hapa ndio hoja ya kutoa somo kwa wahariri inaonekana umuhimu wake. Michuzi yuko Daily News, sijui kama magazeti mengine yanaweza kutumia picha zake…eti Michuzi?
Siku ya Blogu Tanzania ni wazo zuri sana. Tuna muda wa kutosha kuweza kuamua tunataka siku hii isherehekewe vipi. Tuna mwaka mmoja wa kupanga na kupangua. Jamani, tumeanza hivi kimchezomchezo mara tuna siku ya kitaifa, mara jumuiya inakuja, mara tuzo, uongozi wa muda, habari zetu kuingia magazetini, tovuti ya Habari Tanzania, redioni (na hata luningani)…tunaweza. Au unabisha?
Tunaweza. Na tutaweza. Kidole kimoja haki….