Na Claud Gwandu
MAHAKAMA ya Afrika Mashariki imesimamisha shughuli za Bunge la Afrika Mashariki (EALA) lililokuwa lianze kukutana mjini hapa kuanzia kesho.
Uamuzi mahakama hiyo unatokana na kesi iliyofunguliwa na watu 12 kutoka Kenya waliopinga uteuzi wa wabunge wa bunge hilo kutoka Kenya. Mahakama imeona kuwa malalamiko hayo ni ya msingi na kesi itaanza mapema mwakani.
Kwa mujibu wa mkataba wa kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bunge linapaswa kuwa na wabunge 27, tisa kutoka kila nchi mwanachama. Kutokana na maamuzi hayo, bunge hilo sasa lina wabunge kutoka Tanzania na Uganda tu.
Akitoa uamuzi wa mahakama katika kesi hiyo iliyozua malumbano makali ya kisheria kutoka kwa wakili wa walalamikaji, Mutula Kilonzo na Mwanasheria Mkuu wa Kenya, Amos Wako, Makamu wa Rais wa Makakama hiyo, Jaji Joseph Mulenga,a alikubaliana na hoja za upande wa walalamikaji na kuamuru kesi ya msingi ianze kusikilizwa.
“Kutokana na maelezo yaliyotolewa na pande zote hapa mahakamani, na kwa kufuata mkataba wa kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki na taratibu zilizokuwa zinalalamikiwa, jopo la majaji wa mahakama hii kwa kauli moja wanakubaliana na sababu za walalamikaji hivyo mawakili wa pande zote wakutane baadaye kupanga siku ya kuanza kusikiliza kesi,” alisisitiza Jaji Mulenga.
Akijibu hoja iliyotolewa na Wako kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, Jaji Mulenga alisema kwa mujibu wa mkataba wa kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kipengele cha 30, mahakama hiyo ina mamlaka kamili ya kusikiliza shauri lolote ndani ya nchi wanachama wa Jumuiya hiyo, Tanzania, Uganda na Kenya.
Akizungumza baada ya hukumu hiyo kutolewa, Wakili Kilonzo alisema amefurahishwa sana na uamuzi huo na kwamba hukumu hiyo si kwa ajili ya Wakenya tu bali wananchi wa nchi zote wanachama.
“Najisikia furaha sana kwani hii mahakama imeonyesha ukomavu mkubwa na hii inawapa imani wananchi wote wa Afrika Mashariki kwamba mahakama inaweza kuwatetea,” alisema Kilonzo aliyekuwa akipongezwa na wateja wake ambao walijazana mahakamani hapo jana.
Kwa upande wake, Wako alisema kuwa upande wa serikali ya Kenya unakubaliana na hukumu hiyo na kuwa hawana sababu ya kukata rufaa na wanajiandaa na kesi.
Katika malalamiko yao, walalamikaji hao wakiongozwa na Profesa Peter Anyang Nyong walidai kuwa taratibu zilizotumika kuwapata wabunge wa Bunge la Afrika Masharikli kutoka Kenya zilikuwa zimepindishwa na kuomba mahakama izuie kuapishwa kwa wabunge hao.
Walalamikiwa katika kesi hiyo walikuwa ni Mwanasheria Mkuu wa Kenya, Katibu wa Bunge la Kenya, Msajili wa Mahakama ya Afrika Mashariki, Makamu wa Rais wa Kenya, Moddy Awori na Mwenyekiti wa Chama cha Narc- Kenya, Dk Mukhisa Kituyi.