Na Mwandishi Wetu
ASKARI polisi mmoja, mwenye cheo cha konstebo na mwenzake aliyefukuzwa kazi polisi mwaka jana, wamenusurika kuuawa na wananchi wenye hasira baada ya kukamatwa wakiiba madumu matupu 10 ya mafuta ya alizeti.
Watu walioshuhudia tukio hilo, wamelieleza Mwananchi kuwa watuhumiwa hao (majina tunayasetiri kwa sasa), walipata kipigo hicho na kuumia vibaya sehemu mbalimbali za mwili.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Celina Kaluba, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kulielezea kuwa ni la kulifedhehesha Jeshi la Polisi.
Akielezea tukio hilo, Kamanda Kaluba alisema lilitokea Novemba 24, mwaka huu majira ya saa 2.30 usiku katika kiwanda cha kukamua mafuta cha Singida Fresh Mills, mali ya Urari Mustapha, kilichopo eneo la Utemini mjini hapa.
Alisema siku ya tukio, wafanyakazi wa kiwanda hicho walikuwa wakiteremsha madumu matupu ya kuwekea mafuta ya alizeti kutoka kwenye lori lenye namba za usajili T283 AMJ, lililokuwa limeegeshwa ng'ambo ya barabara, umbali wa mita 500 kutoka kiwandani.
Kazi hiyo ya kushusha madumu ilikuwa ikifanywa na Yusuf Omari huku wenzake wakihamisha na kuyapeleka kiwandani.
Wakiwa kiwandani, ghafla walitokea watu wawili na kuwaamuru wakae chini, na kuwatishia kuwa vinginevyo risasi zingerindima kwenye eneo hilo. Vijana hao pamoja na mlinzi wao walitii amri hiyo, wakakaa chini.
Wakati wa purukushani za wavamizi hao kutaka kuondoka na madumu kumi matupu, mlinzi wa kiwanda hicho, Ramadhani Abdallah (56) alifanikiwa kutoroka na kuanza kupiga filimbi na mayowe ya kuomba msaada ambayo yaliwavuta wananchi waliokuwa maeneo ya jirani.
Wananchi hao walianza kuwashambulia kwa mawe na fimbo na kupiga kelele za wezi.
Wakati wananchi wakiendelea kuwapiga watuhumiwa hao, askari polisi walipata taarifa na kuwahi katika eneo hilo na kuwaokoa.
"Baada ya kuwafikisha kituoni huku wakiwa wameumizwa vibaya sehemu mbalimbali za miili yao ikiwamo mikono na kichwani, tuligundua kwamba mmoja wao ni askari wetu wa kikosi cha ufundi Singida," alisema Kamanda Kaluba.
Alisema askari huyo alipohojiwa alikana kuhusika na wizi huo, akidai kwamba alipita tu kwenye eneo hilo akitokea katika baa moja iitwayo Zebra alikokwenda kudai fedha, zake ndipo watu walimshuku kuwa mwizi na kuanza kumpiga.
Kwa mujibu wa RPC, siku ya tukio askari huyo aliomba ruhusa kwamba ni mgonjwa, lakini cha kushangaza alipokamatwa alikuwa akinuka pombe.
"Kwa kweli kitendo cha huyu askari wetu kwenda kuiba madumu tena matupu ya Sh35,000 kimenisikitisha sana na kimelifedhehesha jeshi la polisi mkoani Singida," alisema RPC Kaluba.
Alisema askari huyo alifunguliwa mashitaka ya kijeshi tangu Jumamosi, wakati mwenzake, amefikishwa mahakamani jana kujibu tuhuma zinazomkabili za unyanganyi wa kutumia nguvu.
Alisema wananchi watajulishwa baadaye hatua zitakazochukuliwa dhidi ya askari huyo