Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Dereva, konda waua abiria
Dereva, konda waua abiria
By Habari Tanzania | Published  11/28/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated

Na Mwandishi Wetu

POLISI mkoani hapa wanamshikilia dereva na kondakta wake wa basi dogo la abiria aina ya Toyota Coaster kwa tuhuma za kumuua abiria, Herry Losujak Saning’o (34) aliyekuwa anadai arejeshewe chenji yake ya Sh600 baada ya kulipa nauli.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Matei Basilio, alisema baada ya kumpiga na kumuua abiria huyo, watuhumiwa hao walikamatwa wakimtupa katika eneo la makaburi ya Kaloleni jijini hapa.

Kamanda Basilio alisema, tukio hilo lilitokea juzi saa 1.30 jioni baada ya gari hilo kurejea jijini hapa likitokea Moshi mkoani Kilimanjaro, ambako hufanya safari zake za kila siku.

Wakielezea tukio hilo, ndugu wa marehemu ambao walikuwa wamesafiri naye kutoka eneo la King’ori wilayani Arumeru kuja mjini hapa, walisema ugomvi baina ya marehemu na kondakta wa basi hilo, ulianzia katika eneo la Mianzini wakati alipoanza kudai chenji yake.

William Mandaine ambaye ni shemeji wa marehemu, alisema wakiwa kwenye gari hilo, Saning’o ambaye alikuwa ameandamana na mkewe, Glory Herry, alitoa Sh2,000 kama nauli.

Mandaine alisema nauli ya kutoka King’ori hadi Arusha mjini ni Sh700 na hivyo aliomba kurejeshewa Sh600, kitu ambacho kondakta alikataa.

“Baada ya kumuomba kwa muda mrefu tulipofika Mianzini ambapo ndio mwisho wa safari yetu, tulianza kushuka na ndipo Saning’o alikumbushia kupewa Sh600 yake, na ndipo kulitokea kutoelewana baina yao. Dereva kuona hivyo, alishuka kwenye gari hilo kuingilia,” alisema Mandaine.

Alisema badala ya dereva huyo kusuluhisha ugomvi huo, naye alimuunga mkono kondakta wake kuwa kamwe hawarejeshi fedha, kwani wao ndio wanadai na hapo hapo walimbeba Saning’o na kumrejesha kwenye gari na kuondoka naye kwa kasi.

Mandaine alisema, baada ya kuondoka na Saning’o, wao walikodi teksi na kuanza kuwafuata kwa nyuma lakini kutokana na mwendo kasi ya gari hilo, walipotezana katikati ya jiji, hivyo wakaamua kwenda polisi.

Alisema wakiwa polisi, waliliona gari hilo likiwa katika makaburi ambayo yapo jirani na Kituo Kikuu cha Polisi mjini hapa na ndipo nao walipokwenda na kukuta tayari polisi wamefika.

“Mara baada ya kuwakuta polisi, ndipo tulipewa taarifa kuwa kondakta na dereva huyo wameonekana wakimtupa mtu nje ya gari na baada ya kufuatilia ndipo tulimkuta Saning’o akiwa katika hali mbaya na baadaye alifariki,” alisema.

Kwa mujibu wa taarifa ya awali ya uchunguzi wa kifo hicho, Saning’o alifariki kutokana na jeraha kubwa kichwani baada ya kupigwa na kitu kizito kilichotoboa sehemu ya kichwa.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda Basilio, alisema polisi bado inafanya uchunguzi ili kujua chanzo cha kifo hicho lakini taarifa ya awali inaonyesha marehemu alipigwa na kitu kizito kichwani.

“Tunaandika maelezo na yakikamilika tutawafikisha mahakamani watuhumiwa hao… hiki ni kitendo cha kinyama kamwe hatuwezi kukaa kimya,” alisema Kamanda Basilio

Marehemu huyo, ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kiranyi, Wilaya ya Arumeru ameacha mjane na watoto wawili ambao ni Jesca anayesoma darasa la pili na Linda anayesoma shule ya awali.

Kutokana na tukio hilo, chama cha wamiliki wa magari ya abiria Arusha na Kilimanjaro (Akiboa) na chama cha madereva mkoa wa Arusha (Umma) wamelaani kwa nguvu kitendo kilichofanywa na dereva huyo na kondakta wake.

Katibu Mkuu wa Akiboa, Locken Adolf, alisema jana kuwa wamepokea kwa mshituko tukio hilo na wanatoa pole kwa familia ya marehemu.

Tukio hilo limekuja siku chache baada ya dereva mwingine wa gari dogo la daladala maarufu, kama kifodi jijini hapa, kumjeruhi kwa sime askari ya kikosi cha usalama barabarani, PC Hamad.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
This article has been added to your 'Articles to Read' list.
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.