Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Taasisi ya moyo kuanza kutibu figo
http://www.habaritanzania.com/articles/2031/1/Taasisi-ya-moyo-kuanza-kutibu-figo
By Ramadhan Semtawa
Published on 11/27/2006
 
TAASISI ya moyo nchini (THI) inatarajia kuimarisha Idara yake ya Figo kama hatua ya kuboresha huduma zake za matibabu ya moyo.

Na Ramadhan Semtawa

TAASISI ya moyo nchini (THI) inatarajia kuimarisha Idara yake ya Figo kama hatua ya kuboresha huduma zake za matibabu ya moyo.

Hatua hiyo inatokana na matatizo ya moyo hasa upasuaji kuwa na mahusiano na matatizo ya figo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki wakati wa kuutambulisha ujumbe wa wataalamu watano wa magonjwa ya moyo ikiwemo upasuaji, kutoka Ujerumani ambao umekuwepo nchini, mwanzilishi wa THI, Ferdinand Massawe, alisema mara nyingi wagonjwa wanaohitaji kufanyiwa upasuajai hukutwa pia na haja ya kusafishwa figo.

Massawe alisema kutokana na kubaini kuwepo mahusiano hayo ndiyo maana taasisi hiyo imeamua kuimarisha idara hiyo.

"Tumeanza mikakati ya kuimarisha idara yetu ya figo, tumebaini wakati mwingine wagonjwa wetu wa moyo wanahitaji kusafishwa figo," alifafanua Dk Massawe.

Dk Massawe alisema kwa sasa THI imejipanga vema na kwamba kama ni uwezo inaweza kufanya upasuaji kwa watu wawili kwa siku.

Alisema kwa sasa inasubiri kutia saini mkataba na serikali utakaoipa jukumu la kufanyia upasuaji wagonjwa wa matatizo ya moyo badala ya kuwapeleka nje.