Na Mussa Juma
FUNDI umeme, mkazi wa eneo Mianzini mjini hapa, Abraham Maenda(33) amefariki baada ya kushambuliwa na kundi kubwa la mbwa ambao wamekuwa wakijikusanya katika eneo la Mianzini nyakati za usiku.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Matei Basilio akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema kundi hilo la mbwa ambao wamekuwa wakilalamikiwa kwa muda mrefu lilimvamia fundi huyo wakati akirejea nyumbanikwake.
Kamanda Basilio alisema Maeda aliumwa na mbwa hao hadi kufariki baada ya kumzidi nguvu.
Hata hivyo, alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa Maeda aliweza kuvamiwa na mbwa hao na kujeruhiwa sana kwa kuwa alikuwa amelewa, hivyo alishindwa kupambana nao.
Kamanda Basilio alisema kutokana na tukio hilo, anawasiliana na maafisa kadhaa wa mkoa wa Arusha ili kuhakikisha kuwa wanaanza msako mkali wa kuwaua mbwa hao.
“Ni kweli eneo la Mianzini limekuwa na mbwa wengi ambao wanatembea ovyo, hivyo tunawasiliana na wahusika ili kuanza kuwaua mbwa hao,” alisema Basilio.
Katika tukio jingine, Mtoto, Hamis Yusuph(1) amefariki juzi katika eneo la Mianzini baada ya kutumbukia kwenye shimo la shoo.