Na Mwandishi Wetu
SAKATA la ugawaji ardhi kiholela nchini limezidi kuiweka pagumu serikali ya awamu ya nne baada ya vigogo wawili akiwemo Waziri wa Mipango na Ubinafsishaji katika serikali ya awamu ya tatu, Dk Abdallah Kigoda, kugawiwa maeneo ambayo yana rasilimali adimu za miti aina ya mikoko kwa ajili ya uwekezaji.
Wakati Dk Kigoda amepewa eneo kwa ajili ya kujenga hoteli ya kitalii, Afisa Mstaafu wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Donatus Muyonga, amepewa eneo kwa ajili ya kufugia samaki aina ya kamba. Wote wamethibitisha kumiliki maeneo hayo wakisema waliyapata kihalali.
Lakini wakati vigogo hao wakieleza hayo, Idara ya Misitu kanda ya Dar es Salaam imesema haina taarifa hizo na kwamba imeanza kuangalia taratibu zilizotumika kugawa maeneo hayo yenye mikoko.
Waziri wa Maliasi na Utalii, Profesa Jumanne Magembe, alipoulizwa na gazeti kama wizara ina taarifa na umilikishwaji huo, kwanza alishangaa kusikia mtu anamiliki ekari 22 ndani ya eneo la kuhifadhi mikoko na kuahidi kulifanyia kazi suala hilo. Hata hivyo alisema kwa sasa hana taarifa zaidi kwani bado ni mgeni kwenye wizara hiyo na anajaribu kupata taarifa za kila idara.
Kwa mujibu wa sheria ya mikoko ya mwaka 1957, ni marufuku kwa mtu yeyote kufanya uharibifu wa aina yoyote ikiwa ni pamoja na kukata bila kibali miti hiyo adimu ambayo ni moja ya rasilimali muhimu kiuchumi.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi na kuthibitishwa na wahusika, umebaini kwamba, mwanajeshi huyo wa JWTZ, anamiliki zaidi ya ekari 22 ambazo ameamua kufuga samaki aina ya kamba, awali alijaribu kutafuta chumvi akakosa.
Mwananchi imebaini zaidi kwamba, mwanajeshi huyo amezuia mkondo wa maji unaoingia baharini hivyo kusababisha mikoko katika eneo hilo kuungua kutokana na maji kutuama.
Uchunguzi umebaini zaidi kwamba, mradi huo ambao umeanza miaka kumi iliyopita kwa sasa umefikia katika hatua ya juu ya uzalishaji wa kamba hao.
Afisa huyo wa jeshi anamiliki eneo hilo ambalo lipo kati ya wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani na Kinondoni, Dar es Salaam.
Mwananchi ilipomuuliza afisa huyo juzi, alieleza kusikitishwa kwake na kuungua kwa mikoko kwani haikuwa nia yake, lakini akatupa lawama kwa mamlaka zinazohusika na masuala ya utalii na misitu kwa kushindwa kumpa maelekezo tangu awali, juu ya njia ya kuinusuru mikoko hiyo.
Muyonga alifafanua kwamba, awali hakujua kama mikoko hiyo ingekufa kwa kuzuia maji hayo kwani maafisa wa maliasili walikuwa wakifika wakati akijenga mradi lakini hawakushauri kitu.
"Nasikitika sana kuona mikoko imeungua, haikuwa nia yangu, kwanini niue rasilimali za nchi, sikujua, maafisa wa maliasili walikuwa wanakuja wakati najenga mradi, hawakunishauri kitu, si kosa langu," alijitetea.
Hata hivyo, idara ya misitu ya Dar es Salaam kupitia mmoja wa maafisa wake aliyeomba kusitiriwa jina lake, ilisema hawamfahamu mtu huyo na wala hawajatoa hati zozote za umiliki wa eneo hilo.
Wakati afisa huyo akimiliki eneo la mikono la ekari 22, Dk Kigoda anamiliki eneo la mikoko lenye ukubwa wa mita 200 urefu na upana mita 60 (sawa na ekari nne) katika kijiji cha Ununio kilichopo Boko, amethibitisha kuwa amekwishaanza maandalizi ya ujenzi wa hoteli hiyo.
Alipoulizwa kuhusu taarifa za kumiliki eneo hilo lenye rasilimali za mikoko, Dk Kigoda alisema: "Mimi nimepata eneo hilo kupitia TIC (Kituo cha Uwekezaji nchini)."
Alisema TIC ndiyo inajua iligawaje maeneo hayo na kuthibitisha kwamba ujenzi wa hoteli ya kitalii ni moja ya mpango wake, lakini kwa sasa anatafuta mwekezaji.
Dk Kigoda aliongeza kwamba ni dhahiri kwamba kama atajenga hoteli, atapaswa kuikata mikoko hiyo.
Alipoulizwa, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Emmanuel ole Naiko, iwapo kituo hicho kimegawa eneo lenye mikoko, alijibu: "Kwanza, sijaangalia faili kuthibitisha hilo, lakini ni kweli tuna ardhi tumepewa na wizara eneo la Ununio," alisema ole Naiko.
Hata hivyo, ole Naiko alisema siku zote TIC haigawi ardhi maeneo ambayo yana rasilimali kama mikoko na kwamba kama ipo, mwekezaji atapaswa kujenga nje ya mikoko.
Alisema kibali cha ujenzi (Building Permit) kinapaswa kuonyesha eneo la ardhi la uwekezaji lina rasilimali gani na kuzingatia suala zima la uhifadhi wa mazingira.
Kwa upande wa Profesa Magembe akizungumzia zaidi suala hilo tena, alisema, tayari amekwisha kuwaagiza wakuu wa wilaya za husika (Bagamoyo na Kinondoni) kufuatilia suala hilo kabla yeye hajaenda.
"Nimeagiza wakuu wa wilaya husika, waende wakaangalie maeneo hayo kisha na mimi natarajia kwenda baada ya Desemba 4, mwaka huu," alisema Profesa Magembe ambaye awali aliliambia gazeti hili pia kwamba alikuwa akisubiri kupata taarifa za maendeleo ya mradi wa Marine Coastal Envirometal Programme (Mpango wa Uhifadhi Mazingira ya Bahari katika ukanda wa Pwani), ambao uko chini ya Dk Magnus Ngoile.
Hata hivyo, Profesa Magembe alisema licha ya kwamba hajapata taarifa hizo, atajitahidi kuzipata kwa kina. Juhudi za kumpata Dk Ngoile hazikuweza kufanikiwa.
Nalo Baraza la Taifa la Uhifadhi wa Mazingira (Nemc) lilisema halina taarifa za kuwapo kwa sakata hilo na kusema itazifanyia kazi taarifa hizo.
Kaimu Mkurugenzi wa Habari wa Nemc, Barthlomew Tarimo, aliliambia gazeti hili ofisini kwake jana kwamba, hakuwa na taarifa za kuwapo kwa matukio hayo.
Tarimo alifafanua kwamba, anachofahamu ni kwamba mikoko haikatwi kwa namna yoyote ile na kuongeza kwamba hatua hiyo ni kinyume cha sheria inayolinda rasilimali hiyo.