Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Novemba 18 kila mwaka ni siku ya Blogu Tanzania
Novemba 18 kila mwaka ni siku ya Blogu Tanzania
By Habari Tanzania | Published  11/26/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
“Na sasa nafungua kikao rasmi kwa kuwakaribisha nyote mliobahatika kuhudhuria mkutano huu wa kwanza na wa aina yake katika historia ya nchi yetu.” Haya ndio yalikuwa maneno ya msimamizi wa mkutano rasmi wa kwanza wa wanablogu wa Tanzania, Ramadhani Msangi (http:/msangimdogo.blogspot.com/).

Jumamosi iliyopita wanablogu wa Tanzania (http://tinyurl.com/y7w54n) walifanya mkutano rasmi wa kwanza (http://tinyurl.com/y639q3). Iwapo ulisoma gumzo la wiki iliyopita utakuwa unajua kuwa mkutano huo ulifanyika hewani, au mtandaoni! Kuweza kufanyika kwa mkutano huu huku washiriki wakiwa wametapakaa sehemu mbalimbali ni moja ya vielelezo vilovyomfanya mwandishi Thomas Friedman kumpigia mkewe simu alipokuwa nchini India na kumwambia, “Waridi wangu, dunia ni tambarare!” Aliporudi nchini Marekani, Thomas Freedman, alikaa chini na kuandika kitabu kilichobeba jina hilo: Dunia ni Tambarare (The World Is Flat). Utambarare wa dunia ulijionyesha katika hatua zote za mkutano huu. Jeff Msangi ( HYPERLINK "http://harakati.blogspot.com/" http://harakati.blogspot.com/) alitoa wazo akiwa Canada kupitia blogu yake. Mimi nikiwa Marekani nikaunga mkono na kupendekeza zana za mtandaoni za kutumika kufanikisha mkutano huu. Ramadhani Msangi aliyeko Tanzania akachaguliwa kuwa msimamizi wa mkutano.

Mike Mushi wa HabariTanzania.com (mzee wa mlango wa uani) akatumia utaalamu wake kujenga mlango wa uani kusaidia washiriki waliokuwa wakipata matatizo ya kuingia kwenye chumba cha mkutano (kilichokuwa mtandaoni). Kwa dakika chache aliwawezesha washiriki waliokuwa wakipata tabu kuweza kuingia kwa kupitia tovuti nyingine! Luzango Mfupe akashiriki akiwa Afrika Kusini, Egidiyo (http://www.gaphiz.blogspot.com/) akiwa India, Kitururu (http://simon-kitururu.blogspot.com/) akiwa Ufini, Tungaraza (http://mwandani.blogspot.com/) akiwa Australia, Da”Mija (http://damija.blogspot.com/) (mwanamke wa shoka) akiwa Uholanzi, Mongi ( HYPERLINK "http://mongidreams.blogspot.com/" http://mongidreams.blogspot.com/) akiwa Tanzania, Miriam akiwa Marekani, Jeff akiwa Canada, n.k. Dunia tambarare. Wote tukawa kama vile tuko pamoja ana kwa ana. Zana zilizotumika, kama nilivyoandika katika gumzo lililopita, ni kama vile wiki. Wiki ni aina ya tovuti inayowezesha mtu kuandika jambo bila kuhitaji kuwa na utaalamu wa masuala ya kompyuta. Ukurasa wa wiki ulitengenezwa ili kuwezesha washiriki kubangua bongo kwa pamoja, kupendekeza msimamizi wa mkutano, kupendekeza ajenda, na mambo mengine. Ukurasa huu utaendelea kutumika kwa mambo ambayo hayakupatiwa muafaka wakati wa kikao. Zana nyingine ilikuwa ni Doodle iliyowezesha wanachama kupiga kura kuhusu tarehe na saa ya mkutano, na nyingine ni zana iitwayo IRC ambayo ndio ilitumika kama chumba cha mkutano. Mkutano huu uliashira mwanzo wa zama mpya za uandishi wa raia. Uandishi wa mtandaoni. Dhana ya uandishi wa aina hii imejengwa juu ya mantiki kadhaa.

Moja: matukio hayasuburi “waandishi wa habari” hivyo kuna faida mbalimbali wananchi wa kawaida wanapopewa uwezo wa kuwa maripota. Pili, kila mtu ana haki ya kujieleza na kutoa mawazo yake. Haki hii lazima iendane na mifumo, zana, na taratibu za kumwezesha kila mtu kutimiza haki yake hiyo. Tatu, haki ya kujieleza na kutoa maoni inaendana pia na haki ya kila raia kutoa hayo mawazo yake kwa watu wengine na haki ya wengine kuweza kuyapata maoni na mawazo hayo. Yaani sio tu mtu awe na haki ya kutoa maoni na mawazo ila kuwe hakuna namna ya watu wengine kuyajua, kuyasoma, au kuyasikia mawazo hayo. Nne, wasomaji, watazamaji (luninga), na wasikilizaji sio mazezeta. Mmoja wa wapiga mbiu wa uandishi huu, Dan Gilmor, anapenda kueleza sababu iliyomfanya kuanza kuingia kwenye kambi ya uandishi wa mtandaoni/raia. Anasema kuwa wakati akifanya kazi magazetini aligundua kuwa wasomaji wake wengi wanajua mambo anayoandika zaidi yake. Vyombo vya habari vya zama zinazotokomea vilikuwa vikitufanya sisi kama vile ni watu wa kupokea habari tu. Tunasoma, tunatazama, tunasikiliza. Lakini hatuna namna ya kujumuika katika kuzalisha habari. Zaidi zaidi tukiwa na jambo wanatuambia eti tumwandikie barua mhariri. Au tupige simu redioni! Kwahiyo, hiki bado ni kipengele cha nne, watu wa kawaida wana mawazo, maarifa, na elimu inayofaa kujumuishwa katika mijadala na habari. Zana kama blogu inatupa basi raia uwezo na njia ya kujumuika katika mijadala mbalimbali ya kitaifa na hata ile ambayo sio ya kitaifa. Hakuna haja ya kusubiri hadi mtu apewa safu gazetini. Ukitaka kuwa mtangazaji wa redio huna haja ya kusubiri hadi uajiriwe. Unaweza kuanzisha redio yako mwenyewe. Itakuchukua dakika chache tu.

Ukiomba ajira sio unatuma wasifu karatasini bali unatuma rekodi za vipindi toka katika redio yako! Muda utakaotumia kusoma makala hii na kuimaliza unaweza kuutumia kuanzisha luninga yako mtandaoni. Hili sio jambo la mchezo. Wala usifikiri ni utani. Raia tunapewa nguvu na zana ambazo huko nyuma walikuwa nazo watu fulani na fulani kwakuwa wana vinazo vikubwa vya mapato. Tazama redio aina ya podikasiti iitwayo Redio Butiama (http://butiama.podomatic.com/). Dakika chache tu unaweza kuwa na yako kama hii. Kama hujui jinsi ya kuanzisha, sema utasaidiwa. Tano, vyombo vikubwa vya habari huwa vinapenda sana habari za “zinazouza.” Habari zenye zilizotiwa chumvi chumvi hivi. Hivyo utakuta habari mbalimbali zenye manufaa makubwa kwa jamii hazipewe kipaumbele. Habari kuhusu afya au mazingira haipewi kipaumbele kama habari ya Abdala kafumaniwa. Habari za mahakamani zinazopendwa kuandikwa ni zile zisemazo, “Asahau jina mahakamani.” Au “Nusura azirai kizimbani.” Undani wa kesi, sheria, na taratibu za mahamakani (hizi ni taarifa muhimu zenye kuelimisha) zinaonekana ni kavu sana. Sasa wananchi wanachoweza kufanya ni kuanza kuandika mambo ambayo wanaona yana faida. Ndio unakuta tuna wanablogu wanaaondika habari za mazingira, kilimo, historia (ile historia ambayo shuleni haifundishwi na magazetini haiandikwi), n.k. Wanasiasa badala ya kusubiri hadi “press release”zao zichapwe magazetini wanaweza kuwa na vyombo vyao vya habari vyao ambavyo vitazichapa. Wanaharakati wakiona habari za mikutano yao haziandikwi maana hawakutoa “mshiko” kwa waandishi wanaweza kuzitoa kwenye redio, luninga, au blogu zao ambazo walitumia dakika kumi, ishirini tu kuzianzisha.

Siku hizo waandishi nchi za magharibi wanakuwa makini sana. Kumetokea matukio mbalimbali ambapo mwandishi anamhoji mwanasiasa au mtu fulani maarufu. Halafu, kama ilivyo kawaida yao, wanapindisha kidogo maneno ya waliyemhoji ili kutia chumvi. Basi huyo aliyehojiwa kama hana blogu tayari, anafungua blogu na kuchapa mahojiano yote na kusema, “Huu ndio ukweli wa nilichosema.” Mwandishi anabaki akiimbiwa, “Anaona haya huyo… Tunaona pia jinsi ambavyo vipaji ambavyo vimejificha vinajitokeza kupitia bloguni ambapo pamejazana watunzi, washairi, wapiga picha, n.k. Kwa mfano, unakutana na mwanablogu wa Sahara Soul Food ( HYPERLINK "http://saharasoulfood.wordpress.com/" http://saharasoulfood.wordpress.com/) ambaye ana uandishi wa hadithi kwa kuchanganya Kiswahili na kiingereza. Uandishi wa aina yake. Au unakutana na wengine wanaotumia ujuzi wao kufaidisha wengine kama Miriam (http://blog.mirecipe.com/) ambaye anatumia ujuzi wake wa mapishi kuandika kuhusu mapishi mbalimbali.

Au unakutana na picha nzuri sana ambazo huwezi kuzikuta magazetini kwenye blogu ya Mjengwa (http://mjengwa.blogspot.com/). Au unakutana na mijadala ya masuala ya dini kwenye blogu ya Bwalya ( HYPERLINK "http://bwaya.blogspot.com/" http://bwaya.blogspot.com/). Basi tukafanya mkutano. Ukaenda vizuri. Mkutano ulijadili masuala ya mikakati ya kuongeza idadi ya wasomaji wa blogu na wanablogu, maadili, umuhimu wa kuwa na jumuiya rasmi, na kuchagua viongozi wa jumuiya hiyo. Kwakuwa kulikuwa na mambo mengi ambapo haikuwezekana kumaliza kuyajadili, washiriki walipiga kura (huko huko hewani!) na kuchagua kamati ya muda. Kamati hiyo ya muda inaundwa na Da’Mija, Jeff Msangi, ndesanjo macha, na Ramadhani Msangi. Kati ya kazi za kamati ya muda ni kutafuta jina muafaka la jumuiya hiyo, kukusanya mawazo ya wanachama kuhusu aina ya jumuiya wanayoitaka na muundo wake, aina ya uongozi utakaofaa, watakusanya maoni kuhusu masuala ya ujenzi wa tovuti ya jumuiya, maoni ya wanachama kuhusu tuzo za wanablogu, mfumo wa kutoa tuzo hizo kila mwaka, aina za tuzo, namna ya kuchagua blogu za kutuzwa, na jina la kikusanya habari (aggregator). “Aggregator” ni aina ya tovuti ambayo huchapisha habari mpya kila inapotokea kwenye blogu.

Mwanablogu wa Tanzania anapochapisha habari mpya, tovuti hii itakuwa ikizidaka na kuzichapisha. Hivyo badala ya wasomaji kutembelea blogu moja moja na wakati mwingine kukuta nyingine hazina jipya msomaji ataweza kwenda kwenye tovuti hii na kusoma habari zote mpya za siku,. Mkutano huo ulifikia pia uamuzi mmoja uliowagusa wanablogu wengi. Kuanzia mwaka ujao, tarehe 18 Novemba (siku ambayo mkutano ulifanyika), itakuwa ni Siku ya Blogu ya Kitaifa nchini Tanzania. Siku hii ndio siku ambayo pia tuzo za blogu bora itakuwa ikitolewa. Hivi wewe una blogu? Huna?! Una ngoja nini? Blogu: http://jikomboe.com

How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.