Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri wa Ushirikiano Afrika Mashariki, Dk Diodorus Kamala, amesema wanaofikiri kuwa Tanzania ikiingia kwenye Shirikisho la Afrika Masharika, itakuwa 'shamba la bibi' la kuvuna kila mtu wanajidanganya.
"Litakuwa shirikisho ambalo halitafanya Tanzania kuwa kichwa cha mwendawazi, ambacho kila mtu hujifunzia kunyoa. Tanzania haitakuwa shamba la bibi ambalo kila mtu kuja kuvuna anavyotaka. Itabaki Tanzania kwa maslahi ya Watanzania," alisema.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na jumuiya ya Chuo Kikuu Mzumbe na Chuo Kikuu cha Waislam Morogoro, Dk Kamala alisema Rais Jakaya Kikwete ameamua maoni yatakayotolewa na wananchi jinsi ya kujiunga kwenye shirikisho ndio yataheshimiwa.
Alivitaka vyombo vinavyosimamia sheria kufanya kazi zake kwa mujibu wa sheria.
Kauli hiyo ilifuatia maoni ya baadhi ya wasomi kuonyesha wasiwasi jinsi Ziwa Victoria lilivyovamiwa na wavuvi kutoka Kenya na Uganda, huku wavuvi wa Tanzania wakiwa hawaruhusiwi kuvua sehemu za nchi hizo.
"Nani kawambia kuwa mipaka ya Ziwa Victoria imeondolewa? Mipaka ipo na haitaondolewa ingawa baadhi ya wanachama wa EAC wanataka tufanye hivyo, lakini hatuwezi kwa sababu Tanzania itabaki kwa maslahi ya Watanzania, kinachotakiwa ni vyombo vyetu vya kusimamia sheria kufanya kazi zake kikamilifu," alisema Dk Kamala.