Na Joyce Kisaka SERIKALI imesema kuwa polisi wanafanyia kazi orodha iliyopelekwa kwa Rais Jakaya Kikwete inayohusu watuhumiwa wakuu wa dawa za kulevya maarufu kama 'wazungu wa unga' na kuongeza kuwa kutaja majina yao kwa sasa kutaharibu utaratibu mzima wa uchunguzi.
Waziri wa Usalama wa Raia, Bakari Mwapachu alisema jana kuwa hoja ya watu kuwa serikali inapata kigugumizi kutaja orodha ya watuhumiwa wa dawa za kulevya si sahihi na pia si vizuri kwa sasa kuchapisha magazetini na katika vyombo vya habari majina ya watuhumiwa kwani wanaweza kukimbia na pengine kuficha ushahidi.
Alisema hakuna siri yoyote inayofichwa kwenye kutaja majina zaidi ya kuwa yataharibu uchunguzi na kama kuna mtu anayefuatilia namna serikali kupitia jeshi lake la polisi inavyofanya kazi hatakuwa na wasiwasi.
“Hata kama ni vigogo wa ngazi za juu na wafanya biashara wakubwa itakapokamilika tu hiyo ripoti kuwa imethibitishwa wapo, basi watapelekwa mbele ya sheria bila kuonewa aibu,”alisema
Alisisitiza kuwa hata wale wafanyabiashara waliotangazwa wakati ule walipofikishwa mahakamani ndio majina yao yaligundulika na orodha ilikuwepo kabla hivyo watu wawe na subira na kazi itakapomalizika basi hakutakuwa na kificho.
"Kwa mfano mtu yoyote anayejihusisha na dawa leo hii akiona jina lake gazetini ni rahisi kuficha biashara yake au yeye mwenyewe hata kutoweka, kwa hiyo kinachofanyika kwa sasa ni kuwa wanafuatiliwa na kuhojiwa kimya kimya yule anaeonekana kuwepo na mazingira yoyote yanayohusiana na kujihusisha na biashara hiyo atawekwa chini ya ulinzi na kufikishwa mahakamani.
“Naomba ieleweke kuwa kutokutaja majina sasa haina maana kuwa tunaogopa kwa kuwa yana list (orodha)ya wafanyabiashara wakubwa au vigogo ni kwa kuwa watavuruga uchunguzi, “alieleza.
Hata hivyo, Mwapachu alisema si vizuri kwa wananchi kwa sasa kuingilia kazi ya polisi kwani polisi wanaweza na kuikamilisha kazi hiyo.
“Hata hivyo, nawahakikishia wananchi kuwa polisi wakishamaliza uchuguzi bila kujali kuwa ni kigogo au nani atakayethibitika atashtakiwa," alisema.