Mwamko wa Watanzania wengi kutembelea vivutio vya kitalii vilivyopo nchini bado ni mdogo kulinganisha na ule wa wageni toka nje ambao wanaingiza mapato mengi katika sekta hiyo.
Miongoni mwa sababu zinazosemwa ni kutofahamu vizuri vivutio na umuhimu wa utalii hata kudhani kufikiria kuwa vivutio hivyo ni kwa ajili ya wageni tu au fikra kuwa ni gharama kubwa kuvitembelea.
Hivi karibuni uongozi wa Hifadhi ya Taifa ya milima ya Udzungwa (UMNP) umetangaza mikakati mipya ya kuinua kiwango cha utalii wa ndani kama anavyosimulia Mwandishi FELIX ANDREW.
’’Ule utamaduni wa Watanzania wengi kutembelea vivutio vya kitalii bado haujapata kipaumbele kinachostahili.
Ni jambo la kushangaza kuona kuwa watu wanatoka nchi za mbali kuja kuona vivutio vilivyopo nchini kwetu , wenyewe hatuna habari navyo lazima tujiulize kuna nini?’’, anasema Bw. Ludovic Kisara ambaye ni mtalaam wa masuala ya utalii nchini.
Anasema muda umefika watanzania kubadilika kwa kuvitambua vivutio hivyo na kuvitembelea kwa lengo la kuongeza pato la taifa, kujiburudisha na kujifunza mengi.
’’Tuepukane na ule msemo wa kusema kuwa vivutio hivi ni urithi wa vizazi vijavyo, tuanze sasa” anaongeza.
Mhifadhi katika Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa anayeshughulikia utalii Bw Seth Mihayo anakiri kuwa idadi ya watanzania wanaotembelea hifadhi hiyo kwa mwaka bado ni ndogo sana kulinganisha na wageni.
Milima ya Udzungwa ipo kusini kati ya Tanzania katika wilaya za Kilombero mkoani Morogoro na Kilolo iliyopo Iringa.
Eneo la Udzungwa lina urefu wa kilomita za mraba zipatazo 10,000 ambapo kati ya hizo Hifadhi ya Udzungwa inachukua ukubwa wa eneo la kilomita za mraba 1,990.
Kwa mfano anasema katika kipindi cha mwaka 2003/ 4 kulikuwa na watalii wa ndani wapatao 328 kulinganisha na 1,421 watalii wa kigeni waliotembelea mbuga hiyo.
Katika kipindi cha mwaka 2004, idadi iliongezeka kidogo na kufikia watalii 486 wa ndani kulinganisha na 1,637 wa kutoka nje.
Hali hii ya uchache wa watalii wa ndani ipo karibu katika kila vivutio hapa nchini anasema.
Kutokana na suala hili, hifadhi hiyo imeamua kujipanga upya kwa kuanzisha kampeni maalum ya kuhakikisha kuwa idadi ya watalii wa ndani inaongezeka sambamba na ile ya nje.
Miongoni mwa kampeni kubwa ni kushiriki katika maonyesho ya kimataifa ya Saba Saba yanayotarajiwa kuanza Juni 30 mwaka huu jijini Dar es Salaam na ya wakulima iitwayo Nane nane yatakatayo fanyika mkoani Morogoro baadaye mwake huu.
Anasema kuwa wataangalia uwezekano wa kuandaa safari za wananchi kutembelea hifadhi hiyo wakati wa maonyesho hayo kwa gharama nafuu.
kwa sasa kiingilio katika hifadhi hizo ni kati ya shilingi 1,000 kwa watu wazima na 500 kwa watoto ambapo wageni ni dola 15 kwa watu wazima na dola 5 kwa watoto.
Anadokeza kuwa uongozi wa hifadhi una mpango wa kufanyia mabadiliko viingilio kwa wageni ifikapo Julai mosi mwaka huu.
Anabainisha kuwa inawezekana watanzania wengi bado hawajajua umuhimu na vivutio vinavyopatikana katika hifadhi za hapa nchini.
’’Cha kufurahisha zaidi ni kuwa asilimia kubwa ya utalii katika hifadhi hiyo unafanyika kwa kutembea kwa miguu badala ya gari kama hifadhi nyingine’’, anasema.
Anasema hii inatoa fursa kwa wananchi kuwaona kwa ukaribu wanyama huku hatua za kuwalinda zikiwa zimechukuliwa.
Akitolea mfano , anasema hifadhi hiyo ina wanyama wengi ambao hawapatikani katika hifadhi nyingine za aina hiyo duniani.
Hifadhi hiyo ina wanyama , mimea na wadudu wa aina ya kipekee hapa nchini na duniani wanaopatikana huko.
Baadhi ya wanyama ambao ni vivutio wanaopatikana katika hifadhi hiyo ni Ngolaga wa Sanje (Sanje Mangabey), Mbega Mwekundu wa Iringa (Iringa Red Colobus Monkey),Komba mdogo wa Matundu(Matundu dwarf Galago)na Kipunji(Highland Mangabey).
Inasemekana kuwa katika miaka ishirini iliyopita hakuna primata aliye gunduliwa duniani. Mwaka jana, aligunduliwa primata kipunji na hii inadhihirisha kuwa Tanzania na hususani Hifadhi ya milima ya Udzungwa ina viumbe hai wengi ambao hawapatikani mahali popote duniani.
Kwa upande wa mijusi ni Kinyonga mdogo, vipepeo ni Papilio hornimanii Mwaninanae, Charaxes,lucyae, Mwanihanae vyura ni chura wa kwenye miti .
Anataja baadhi ya ya mimea kuwa ni Saintpaulia pusilla, Vernonia luhomeroensis, Lobelia udzungwensis, Meinecki udzungwaensis, Pauridiantha udzungwensis, Tarenna udzungwensis, na Disperis udzungwae.
’’Wanyama na mimea hii ina umuhimu mkubwa sana katika maisha ya kila siku ya binadamu na utunzaji wa misitu kwa ujumla,’’ anasema.
Vivutio vingine ni pamoja na Vilele vya milima Luhomero wenye kilele kirefu na Mwanihana ambao ni wa pili kwa urefu,maporomoko ya maji ya Sanje,Prince Bernhard, Njokamoni na Sonjo,Maeneo ya kihistoria kama mapango ya zamani ya Nyumbanitu, mwanalevele, bokela ambayo wananchi wanatumia kwa ajili ya kufanyia matambiko mbali mbali na mabaki ya kijiji cha Mbatwa .
Hifadhi hiyo pia imeamua kuongeza wigo wa shughuli za kitalii zinazofanyika ndani ya hifadhi hiyo.
Baadhi ya shughuli zinazotarajiwa kuongezwa ni uanzishwaji wa utalii wa kutumia mitumbwi na kuteleze kwa kamba na canopy walk way utalii utakuwa ni wa aina yake kwani Tanzania itakuwa ni nchi pekee Afrika Mashariki yenye utalii wa aina hii na inatarajiwa kuvutia watalii wengi.
Pia njia za utalii ndefu na fupi zimeongezwa kwenda kwenye vivutio mbalimbali vya utalii.
Hifadhi ya milima hiyo iliyoanzishwa rasmi mwaka 1992 ina malengo kadhaa ambayo ni kuhifadhi viumbe na mfumo mzima wa kipekee wa milima hiyo.
Malengo mengine ni kuhifadhi misitu ya asili, kulinda milima kwa kupunguza mmomonyoko wa udongo na kuhifadhi makazi na viumbe adimu vya kipekee na vilivyoko hatarini kutoweka.
Akielezea umuhimu wa hifadhi hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Meja Jenerali Mstaafu Said Kalembo anawaomba wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo kuitunza kwa moyo wao wote kwani wao ndio wadau wakuu na ni hazina kwa taifa.
’’Hifadhi hii ikitunzwa vizuri zaidi itatusaidia sana katika mambo mengi kama kuongeza pato la kigeni na ndani, na ajira kutokana na shughuli za kitalii,maji, umeme na kilimo,’’ anabainisha Kalembo.
Anasema kuwa hifadhi hizo ni chanzo cha maji katika maeneo mengi, pia umeme wa Kidatu na mashamba ya mpunga na miwa katika bonde la Kilombelo.
Anasema serikali mkoani humo itaendelea kuimarisha miundomnbinu itakayowawezesha wananchi kutembelea kwa urahisi hifadhi hizo.
Baadhi ya wananchi waliohojiwa walikiri kutokuwa na tabia ya kutembelea vivutio vya kitalii nchini.
’’Kwa kweli gharama kubwa kama usafiri, chakula na malazi ndizo zinazotufanya kushindwa kutembelea mbuga hizi”anasema Jumanne Mwilama.
Akitolea mfano anasema kutembelea hifadhi hasa zile za mbali ina kuwa gharama kubwa kulinganisha na maisha ya sasa na kuwafanya watu wengi kuamua kutafuta fedha za kula na kufanyia mambo mengine.
Mratibu wa Mfuko wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Wanyama na Mazingira (WWF) Bi Zakhia Aloyce, anasema katika kuimarisha shughuli za utalii nchini, mfuko huo utaendelea kusimamia na kutoa msaada katika kukuza sekta ya utalii nchini.
Anasema kuwa mfuko huo umepata kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuhifadhi mazingira katika milima ya Vidunda vilivyopo wilayani Kilombero.
Milima hiyo ambayo inapakana na hifadhi zaUdzungwa nayo ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya utalii.
Mtafiti mmoja wa mambo ya kijamii kutoka shirika la Comitode Bw. Huruma Kisaka, anasema kasi ya ukuaji wa utalii katika hifadhi ya Taifa ya milima ya Udzungwa itakuwa zaidi ikiwa shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi zitapigwa marufuku.
Kwa upande wake mhifadhi mkuu wa UMNP Bw.Christopher Timbuka anasema kwa sasa malengo ya kuanzishwa kwa hifadhi hiyo kwa yanaelekea tofauti kutokana na watu kuokota kuni, kuchimba dawa na kukata nyasi ndani ya hifadhi hiyo kinyume na sheria ya uanzishaji wa hifadhi za Taifa.
Katika kuboresha zaidi vivutio katika hifadhi hiyo viongozi wa hifadhi kwa kushirikiana na wadau waliamua kupiga marufuku shughuli za kibinadamu zilizokuwa zikifanyika katika hifadhi hiyo.
Kabla ya marufuku hiyo kuliundwa timu maalum iliyokuwa ikitafiti athari zilizotokana na uharibifu katika hifadhi hiyo.
Kutokana na kuendelea kwa uharibifu timu ya utafiti ilipendekeza katazo la kufanywa kwa shughuli za aina yeyote ndani ya hifadhi baada ya miaka mitano kuanzia sasa.
Wadau wote walikubaliana katika kikao ambacho kilisimamiwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kusimamisha sughuli zote baada ya miaka mitano.
Pia ilipendekezwa kuwa kila mwananchi kupanda miti katika eneo analoishi na kila kijiji kupanda miti kwa ajili ya kukata kuni za kupikia ili kutoendelea kutegemea kuni kutoka ndani ya hifadhi.
SOURCE: Nipashe