PROFESA Leonard Lema, ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Uteuzi huo utaanza Desemba mosi, mwaka huu.
Taarifa ya uteuzi wa Profesa Lema imetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la MNH, Abdulrahman Kinana.
Profesa Lema amewapiku waombaji wengine watatu; Rozina Lipyoga, Profesa Andrew Swai, na Dk. Dominicus Dominic.
Baada ya habari za uteuzi huo, Tanzania Daima, ilifanya mahojiano na baadhi ya wafanyakazi hospitalini hapo, na wengi walipongeza uteuzi huo.
Miongoni mwa waliopongeza ni Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya Tanzania (TUGHE), Tawi la Muhimbili, Constantine John.
“Chama kwa niaba ya wafanyakazi, tunampongeza na tunamkaribisha Muhimbili iliyojaa matatizo ya wafanyakazi.
“Wafanyakazi waliposoma kwenye mbao za matangazo uteuzi huo, wameonyesha nyuso za tabasamu.
“Sisi TUGHE tunaomba ushirikiano wake, na sisi tunaahidi kumpa ushirikiano wa hali ya juu katika kutenda kazi zake za kila siku,” alisema John.
“Mimi binafsi ninamshauri kitu kimoja kuwa akianza kulima shamba aanzie miguuni pake, pori ni kubwa sana, limejaa nyoka na ghasia mbalimbali,” alisema John.
Alimshauri mkurugenzi huyo azingatie matatizo ya wafanyakazi wa vipato vya chini, asikaribishe majungu ofisini kwake, na afanye kazi kwa kuzingatia taratibu na sheria.
Alisema akishakabidhiwa ofisi, aitishe mkutano wa wafanyakazi, azungumze nao na awasikilize.
“Naupongeza uteuzi huo, nakubaliana nao jinsi tulivyofanya naye kazi, anajua matatizo ya Muhimbili, ni mchapakazi mzuri tunajua tabia yake,” alisema Yusufu Kasikasi ambaye ni fundi magari hospitalini hapo.
Dereva wa MNH, Shaban Bakari, alimwelezea Profesa Lema kama kiongozi asiyependa majungu, na aliye tayari kuwasikiliza wafanyakazi wa chini.
Profesa Lema alikuwa Mkuu wa Idara ya Upasuaji katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Tiba za Afya Muhimbili (MUCHS).
Habari zilizopatikana zilisema Profesa Lema yuko Nairobi, Kenya kwa shughuli za kikazi.
Mkurugenzi Mtendaji aliyemaliza muda wake, David Tregoning, alimazika mkataba wake Aprili, mwaka huu. Serikali haikutaka kumwongeza muda mwingine raia huyo wa kigeni.