MAHAKAMA Kuu jana iliendelea kusikiliza ushahidi wa upande wa washitakiwa katika kesi ya mauaji ya wakili Eleuther Kapinga, ambako mshitakiwa wa kwanza, Zakaria Mahushi (Ngosha), alikana maelezo (ungamo).
Maelezo hayo aliyatoa kwa mlinzi wa amani Juni 14, 2002. Alikana akidai kwamba alilazimishwa na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe.
Ngosha alionyesha kujikanganya kujibu maswali aliyokuwa akiulizwa na Wakili wa Serikali, Angaza Mwipopo, Jaji Juxon Mlay, na wazee wa baraza.
Ngosha alisema kwamba anakana ungamo kwa kuwa hakulitoa kwa hiari yake, na kwamba alishinikizwa na Zombe.
Mwipopo: Kwa nini leo hii unadai ungamo lile si lako, na unadai ni la Zombe na huku ulipelekwa na askari polisi hadi kwa mlinzi wa amani katika Mahakama ya Mwanzo Kinondoni na ukaungama na kisha ukatia saini kwenye ungamo lako?
Mahushi: Kweli nilipelekwa na askari hadi kwa mlinzi wa amani ambaye mnamsema sasa, lakini siku hiyo mimi niliambiwa aliyekuwa anachukua maelezo ni bosi wa Zombe.
Mwipopo: Nani alikwambia yule ni bosi wa Zombe?
Mahushi: Sikuambiwa na mtu bali yule askari aliponifikisha kule nilipochukuliwa maelezo na S. Tuwa ambaye ni mlinzi wa amani, askari huyo aliniambia tumefika kwa bosi ila hakusema yule ni bosi wa Zombe.
Mwipopo: Sasa hiyo kauli ya bosi wa Zombe umeipata wapi?
Mahushi: Kimya
Mwipopo: Na je, wakati unatoa ungamo lako ndani ya chumba kile alikuwapo Zombe?
Mahushi: Hakuwapo.
Mwipopo: Sasa ni kwanini ung’ang’anie kuwa lile ungamo ni la Zombe, huoni unaidanganya mahakama?
Mahushi: Kimya.
Jaji Mlay aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 27, mwaka huu. Siku hiyo, mshitakiwa wa pili, Ramadhani Amir, ataanza kujitetea