Na Mwandishi Wetu
MTUHUMIWA wa ujambazi wa kutumia silaha, Charles Nyamasero (32), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akiwa amebebwa kwenye machela.
Mtuhumiwa huyo alisomewa mashitaka ya unyang’anyi wa kutumia silaha na wizi wa mali mbalimbali, akiwa kwenye machela yake kutokana na jeraha la risasi analodaiwa kupata katika tukio la ujambazi, Mbagala jijini Dar es Salaam.
Mtuhumiwa huyo alifikishwa mahakamani baada ya kukamatwa na polisi kwa kushirikiana na wananchi, akiwa amejificha porini baada ya kujeruhiwa na risasi mguu wake wa kushoto katika tukio la uporaji katika mitaa mbalimbali ya Mbagala, Dar es Salaam na wenzake kumtelekeza.
Inadaiwa kuwa kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na wenzake watano alioshirikiana nao katika uporaji huo wa nyumba hadi nyumba, kulitokana na ushirikiano wa polisi na wananchi kufuatilia nyayo zao baada ya kufanya uporaji huo na kuelekea eneo la Kitunda.
Akisoma hati ya mashitaka, mbele ya Hakimu Khadija Msongo, Mwendesha Mashitaka, Inspekta Danstan Kombe, alidai kuwa Novemba 16, saa 1.30 usiku katika eneo la Kilungule wilayani Temeke, Nyamasero alipatikana na bunduki yenye namba za siri 1720606 kinyume cha sheria.
Kombe alidai kuwa Novemba 13, majira ya saa 2.30 usiku katika eneo la Charambe Majimatitu, mshitakiwa huyo na wenzake watano walipora vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh70,000 mali ya Sigo Mkaiari baada ya kumtishia kwa bastola.
Aliendelea kudai kuwa siku hiyo hiyo nyakati za usiku, watuhumiwa hao waliiba simu ya mkononi aina ya Nokia yenye thamani ya Sh70,000, fedha taslimu Sh200,000 vyote vikiwa na thamani ya Sh270,000, mali ya Habibu Kingwanda na kabla ya kufanya wizi huo walimtisha kwa bastola.
Inspekta Kombe aliendelea kuieleza mahakama kuwa baada ya kupora mali za Kingwanda, watuhumiwa hao wa ujambazi kwa kutumia silaha walimpora Saidi Omar simu mbili za mkononi zenye thamani ya Sh155,000 na pete tatu za dhahabu zenye thamani ya Sh 45,000.
Katika uporaji huo Nyamasero anadaiwa kushirikiana na watuhumiwa wengine waliotajwa kwa majina ya Lucas Mayomba (50), Charles Chacha (22) na mwanamke wa nyumbani Bageni Martine (19) ambao wanashitakiwa pamoja naye.
Watuhumiwa hao pia wanadaiwa kuwa Novemba 12 nyakati za usiku katika eneo la Mbagala Chemchem, waliiba bastola yenye namba ya siri 503078, risasi 12, fedha taslimu Sh1,505,000, kisu chenye thamani ya Sh10,000 pamoja na mali mbalimbali mali za Edward Jones.
Ilidaiwa kuwa siku hiyo hiyo saa 2.00 usiku, pia watuhumiwa hao waliiba fedha taslimu Sh711,000 mali ya Rozina Kasonde na kabla ya kufanya wizi huo, walimtishia bastola ili kujipatia kiasi hicho fedha kwa urahisi.
Upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na washitakiwa walikana mashtaka na kurudishwa rumande hadi Desemba 8, kesi hiyo itakapotajwa tena.