Na Mwandishi Wetu
MAKALI ya mgao wa umeme yakizidi kuongezeka na kusababisha tabu kwa watumiaji, Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, ametoa ahadi kuwa mwisho wa mwezi Dedemba, tatizo hilo litamalizika.
Karamagi, Waziri mwenye dhamana na masuala ya umeme, amesema serikali, kwa kushirikiana na wadau wengine wa sekta hiyo, ipo katika jitihada kubwa za kuhakikisha kuwa tatizo hilo, ambalo limekuwa kero kubwa kwa wananchi kwa zaidi ya miezi sita sasa, linamalizika kabla ya Januari mwakani.
Hii si mara ya kwanza kwa waziri anayeshughulika na masuala ya umeme kutoa ahadi kama hiyo. Mtangulizi wa Karamagi, Dk Ibrahim Msabaha, pia aliwahi kutoa ahadi kama hiyo, akisema makali yangepungua mwishoni mwa Oktoba lakini haikuwa hivyo.
Badala yake, makali ya umeme yakazidi kuongezeka na ingawa haijawekwa wazi, inaelezwa kuwa ni moja ya sababu zilizomfanya Rais Kikwete akamhamishia katika Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Karamagi alitoa ahadi hiyo jana jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Akizungumza kwa kujiamini, Waziri Karamagi alisema jitihada mbalimbali za dharura zinafanywa kwa lengo la kumaliza mgao wa umeme uliopo sasa.
Alisema jitihada hizo ni pamoja na kuhakikisha kuwa mitambo ya kuzalisha umeme ya kampuni ya Richmond, yenye uwezo wa kuzalisha megawati 100, inafungwa haraka ili hadi kufika mwezi ujao, iwe imeanza kuzalisha umeme kikamilifu.
Alisema kazi ya kufunga awamu ya kwanza ya mitando ya kampuni hiyo yenye uwezo wa kuzalisha megawati 20 ambayo iliwasili hivi karibuni kutoka Marekani, inakaribia kukamilika na kwamba mafundi wamefikia asilimia 80 ya ufungaji wake, hali inayotia matumaini kuwa kuanzia wiki ijayo megawati hizo 20 zitaanza kuzalishwa.
Alisema awamu ya pili ya mitambo ya kampuni hiyo yenye uwezo wa kuzalisha megawati 80 ipo katika maandalizi ya mwisho kuletwa nchini wakati wowote kuanzia sasa, ili iweze kufungwa na kufanya jumla ya megawati zitakazozalishwa na kampuni hiyo kuwa 100.
Hata hivyo, wasiwasi uliopo ni kwamba huenda ufungaji wa mitambo ya awamu ya pili usikamilike katika kipindi anachokitaja Waziri Karamagi, hasa ikizingatiwa kuwa mitambo yenyewe bado haijawasili nchini.
Wasiwasi huo unatokana na ukweli kwamba mtambo wa kwanza wa Richmond, uliwasili nchini Oktoba 21, 2006 na hadi leo, Novemba 24, bado kazi ya kufunga inaendelea. Wengi wanahoji kuwa iwapo mtambo wa megawati 20 unachukua zaidi ya mwezi mmoja kufungwa na kuanza kazi, ni wazi kuwa kazi itakuwa ngumu zaidi kwa mtambo wa kuzalisha megawati 80.
Kuhusu wasawasi wa wananchi kuwa huenda umeme wa kampuni hiyo ukawa ghali, Karamagi alisema, “Hiyo ni dhana tu iliyojengeka, sisi tunasema hapana.”
Alisema umeme wa kampuni hiyo ndiyo rahisi kuliko wa makampuni yote yaliyoomba zabuni wakati ilipotangazwa. Alifafanua kuwa kampuni hiyo inaiuzia Tanesco uniti moja ya umeme kwa senti 1.99 za dola ya Marekani, tofauti na makampuni mengine ambayo umeme wake ulifikia hadi senti 6.57 kwa uniti moja.
Alisema kampuni nyingine ya kuzalisha umeme ya Aggreko tayari inazalisha megawati 40 za umeme na kwamba kampuni nyingine ya Ostram ya Mwanza nayo hivi karibuni itazalisha umeme wa megawati nyingine 40 hivyo hadi kufikia Desemba jumla ya umeme wa makampuni yote matatu utakaokuwa ukizalishwa ni megawati 180 zitakazoingizwa gridi ya taifa na kumaliza tatizo hilo la mgao.
Kwa mujibu wa takwimu za Tanesco, IPTL inazalisha megawati 100, Songas, ambayo mtambo wake namba nne umeharibika, inazalisha megawati 140, wakati maporomoko ya Pangani yanazalisha megawati 68.
Pia Kidatu, yenye uwezo wa kuzalisha megawati 204 inazalisha megawati 25, wakati Kihansi, inayoweza kuzalisha megawati 180, inazalisha megawati 30. Hii ina maana kuwa ukijumlisha na megawati zinazozalishwa na Aggreko, jumla ya megawati 403 zinaingia katika gridi ya taifa, huku kukiwa na upungufu wa megawati 159 katika mahitaji ya megawati 568 nchini.
Kuhusu mtambo wa kuzalisha umeme wa Songas ulioharibika, Karamagi alisema mtambo huo kwa sasa bado upo nje ya nchi ufanyiwa matengenezo na kwamba serikali inafuatilia kwa karibu ili matengenezo hayo yamalizike haraka na kurejeshwa nchini.
Karamagi alisema kuharibika kwa mtambo huo, kumesababisha kiwango cha umeme unaozalishwa na kampuni hiyo ya Songas kushuka kutoka megawati 180 hadi 150.
Hata hivyo, alisema ratiba ya mgao wa umeme itaendelea kubaki kama ilivyo sasa, ambapo kundi la kwanza linalokosa umeme kuanzia saa 12:00 asubuhi na kurejeshwa saa 1:00 usiku; na la pili linalopata huduma hiyo kuanzia saa 1:00 usiku hadi saa 4:00 usiku.
Alisema lengo la mgao huo ni kupunguza matumizi ya maji katika maeneo ya kuzalisha umeme ambako kina cha maji kimepungua sana na kwamba utaratibu huo utawezesha maji machache yaliyopo yaendelee kuendesha mitambo hiyo hadi Desemba wakati mitambo ya dharura ya kuzalisha umeme itakapoanza kufanya kazi kwa uwezo wake wote.
“Bila ya kupunguza matumizi ya maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme maji yatakauka na mitambo itazimika na ikizimika katika hali hii haitawaka tena ndiyo maana tumeweka mgao huu ili kutunza maji hadi hapo mitambo ya dharura itakapo anza kufanya kazi” alisema.
Kuhusu matatizo ya ukata yanayolikabili Tanesco, Karamagi, alisema serikali inaandaa mipango ya kuliwezesha shirika hilo ili lijiendeshe lenyewe na kuipunguzia serikali mzigo wa kulipatia ruzuku.
Alisema miongoni mwa mikakati hiyo ni serikali kununua mitambo ya kampuni ya Independent Power tanzania Limited (PTL) na mazungunzo kati ya kampuni hiyo na serikali juu ya suala hilo yanaendelea.
Mkakati mwingine aliutaja kuwa ni kuboresha miundombinu ya shirika hilo, ambayo ubovu wake unalifanya lipoteze asilimia 26 ya umeme inaozalisha.
Wakati huo huo, waziri huyo alisema makampuni tisa ya kigeni yamejitokeza kwa ajili ya kufanya utafiti wa gesi na mafuta nchini.
Alisema kampuni kubwa ya mafuta ya Brazil ya Petrobrass pia imeonyesha nia ya kutafuta mafuta nchini ambapo mkataba kati ya serikali na kampuni hiyo utatiwa saini mwezi ujao kwa ajili ya kufanya utafiti huo kwenye bahari ya kina kirefu.
Jana, Karamagi alitia saini mkataba wa utafutaji gesi katika eneo la Pande lilopo Kilwa, kati ya serikali ya Tanzania na kampuni ya gesi ya Ghuba ya Al Khaimah (KARGT) katika Falme za Kiarabu.
Mkataba huo wa miaka 11 una thamani ya dola za Marekani 28 milioni ambapo katika kipindi hicho kampuni hiyo itakuwa ikitafuta nishati hiyo ili ikipatikana iweze kuchimbwa.
Karamagi alisema kila mwaka kampuni hiyo pia itakuwa ikitumia dola za Marekani 30,000 kwa ajili ya kulipia leseni ya kutafuta gesi na 10,000 kila mwaka kwa kuendeleza nguvu kazi.
Alifafanua kuwa endapo kampuni hiyo itafanikiwa kugundua kuwepo kwa gesi katika eneo hilo la Pande, itaanza kazi ya uchimbali kwa makubaliano ya kugawana faida itakanayo na gesi hiyo na serikali ya Tanzania kutegemea na kiasi cha gesi itakayokuwa ikizalishwa.