Bismillahi naanza, kwa jina lake Rabuka,
Mmoja mwenye uweza, na asiye mshirika,
Mbele yake najilaza, namkiri Mtukuka,
Viongozi kama wapo, hapo walipo hawapo!!
Wapo wamelala mbele!!
Lowassa ninampinga, ninazidi kumpinga,
Hoja yangu naijenga, kwa tenzi ninayotunga,
Hawawezi piga chenga, wale wanaoboronga,
viongozi kama wapo, hapo walipo hawapo!!
Wapo wamelala mbele!!
Yataje yale mazuri, na tukuunge mkono,
Ni hili la Mzuzuri, au la huyo Mkono,
Utamke kwa dhahiri, tujue yao maono,
Viongozi waliopo, hapo walipo hawapo!!
Wapo wamelala mbele!!
Wenye kupiga lolongo, waoga kufanya kweli,
Watudhani siye chongo, ati hatuoni mbali,
Hawa waivunja bongo, viongozi mushkeli,
Viongozi waliopo, hapo walipo hawapo!!
Wapo wamelala mbele!!
Wanaisha kuonya, kila kukicha jamani,
Amri wazitawanya, wanatisha radioni,
Kama maneno ya Chonya, wao wanaturubuni,
Viongozi waliopo, hapo walipo hawapo!!
Wapo wamelala mbele!!
Wanasubiri pongezi, ndo wafanye mazuri?
Kwani sisi ni machizi, tusioijua shari,
Sifa zao tangu enzi, paani na kwenye dari,
Viongozi waliopo, hapo walipo hawapo!!
Wapo wamelala mbele!!
Umewashinda umeme, na mikataba ya maji,
Mnasema tusiseme, tunyamaze tusihoji,
Mnajifanya mitume, ati ni Mungu mpaji,
Viongozi waliopo, hapo walipo hawapo!!
Wapo wamelala mbele!!
Walio waadilifu, wanaitwa kina nani,
Wasio na upotofu,wanafanya kazi gani,
Kwa katiba watiifu, Lowassa utujibuni,
Viongozi waliopo, hapo walipo hawapo!!
Wapo wamelala mbele!!
Ni nani aliyegoma, kati yao viongozi,
Hadharani akasema, dili hili siliwezi,
Moyoni akajituma, kuliokoa jahazi,
Viongozi waliopo, hapo walipo hawapo!!
Wapo wamelala mbele!!
Kama kweli hawa wapo, miye nawaulizeni,
Wizara gani walipo, majina tutajieni,
Wasiofuata upepo, idadi yao ni gani,
Viongozi waliopo, hapo walipo hawapo!!
Wapo wamelala mbele!!