Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Mzee Mwanakijiji  »  Hapa Walipo Hawapo!
Hapa Walipo Hawapo!
By Mzee Mwanakijiji | Published  11/26/2006 | Mzee Mwanakijiji | Rating:
Viongozi kama wapo!

Bismillahi naanza, kwa jina lake Rabuka,
Mmoja mwenye uweza, na asiye mshirika,
Mbele yake najilaza, namkiri Mtukuka,
Viongozi kama wapo, hapo walipo hawapo!!
Wapo wamelala mbele!!

Lowassa ninampinga, ninazidi kumpinga,
Hoja yangu naijenga, kwa tenzi ninayotunga,
Hawawezi piga chenga, wale wanaoboronga,
viongozi kama wapo, hapo walipo hawapo!!
Wapo wamelala mbele!!

Yataje yale mazuri, na tukuunge mkono,
Ni hili la Mzuzuri, au la huyo Mkono,
Utamke kwa dhahiri, tujue yao maono,
Viongozi waliopo, hapo walipo hawapo!!
Wapo wamelala mbele!!

Wenye kupiga lolongo, waoga kufanya kweli,
Watudhani siye chongo, ati hatuoni mbali,
Hawa waivunja bongo, viongozi mushkeli,
Viongozi waliopo, hapo walipo hawapo!!
Wapo wamelala mbele!!

Wanaisha kuonya, kila kukicha jamani,
Amri wazitawanya, wanatisha radioni,
Kama maneno ya Chonya, wao wanaturubuni,
Viongozi waliopo, hapo walipo hawapo!!
Wapo wamelala mbele!!

Wanasubiri pongezi, ndo wafanye mazuri?
Kwani sisi ni machizi, tusioijua shari,
Sifa zao tangu enzi, paani na kwenye dari,
Viongozi waliopo, hapo walipo hawapo!!
Wapo wamelala mbele!!

Umewashinda umeme, na mikataba ya maji,
Mnasema tusiseme, tunyamaze tusihoji,
Mnajifanya mitume, ati ni Mungu mpaji,
Viongozi waliopo, hapo walipo hawapo!!
Wapo wamelala mbele!!

Walio waadilifu, wanaitwa kina nani,
Wasio na upotofu,wanafanya kazi gani,
Kwa katiba watiifu, Lowassa utujibuni,
Viongozi waliopo, hapo walipo hawapo!!
Wapo wamelala mbele!!

Ni nani aliyegoma, kati yao viongozi,
Hadharani akasema, dili hili siliwezi,
Moyoni akajituma, kuliokoa jahazi,
Viongozi waliopo, hapo walipo hawapo!!
Wapo wamelala mbele!!

Kama kweli hawa wapo, miye nawaulizeni,
Wizara gani walipo, majina tutajieni,
Wasiofuata upepo, idadi yao ni gani,
Viongozi waliopo, hapo walipo hawapo!!
Wapo wamelala mbele!!


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by Nkuzi Nkwazi Mhango)
    Rating
    Shairi lako ni tamu,hakika nalitamani,
    ulosema ni muhimu,tukitia akilini,
    umepiga baragumu,tusikie tulo ndani,
    tatizo la nchi yetu, ni upole wa jamia.

    ona wanavyoshindana,kutazama midundiko,
    kwenye baa wajazana,wakienga mikatiko,
    kwao hilo la maana,siasa kwao ni mwiko,
    tatizo la nchi yetu jamii imelemaa.

    kweli viongozi bomu, hili halina ubishi
    nani kachagua bomu,kama siyo wananchi,
    nani wa kumlaumu,kama siyo wananchi,
    mambo yakiharibika wao wanakaa kimya!

    endelea na utunzi, nakubali u nyakanga,
    wataambua wajuzi, mipango wataipanga,
    wawazie ukombozi,kuwakomesha vipanga,
    jamani watanzania,amkeni kumekucha.
     
Submit Comment


Article Options
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Is Tanzania a safe place to invest?
  4. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Linda Garner
  4. Nthelezi Nesaa
  5. Marshy Abdu
  6. Prosper Kwigize
  7. Salehe Mmoro
  8. Ramadhan Semtawa
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.