KWA mara nyingine, kilio cha haki kimeendelea kusikika dhidi ya Idara ya Wanyamapori, iliyo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Safari hii, kilio hiki si cha wale waliozoeleka, yaani Watanzania, wakereketwa wa maendeleo ya nchi, wapenda mageuzi, wabunge na wachukia ufisadi.
Kilio cha safari hii, kimetoka kwa wafadhili kupitia umoja wao wa Kundi la Wadau wa Maendeleo ya Tanzania (DPG).
Kama ni maneno kutoka kwa Watanzania wa kawaida, tungeweza kusema hizi ni fitina, uzandiki, chuki, husuda, umbea na kila aina ya chuki kutoka kwa Watanzania. Sasa si hivyo tena. Kilio cha hujuma ndani ya Idara ya Wanyamapori, kimekwenda mbali zaidi - kimekwenda kwa wafadhili.
Wafadhili hawa wameeleza bayana jinsi idara hii tajiri inavyotumiwa na watu wachache-wageni walioingia Tanzania-kujinufaisha.
Wanasema kiasi cha sh bilioni 9 kinapotea kila mwaka kutokana na ufisadi kati ya kampuni za kigeni za uwindaji wa kitalii, zilizojenga urafiki na baadhi ya viongozi waandamizi serikalini.
Kama tulivyosema, kilio hiki kimetolewa na wabunge, kimetolewa na wananchi wa kawaida, kimetolewa na wadau wengi, na sasa kimefika hapa tulipo.
Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, imeahidi ‘maisha bora kwa kila Mtanzania’. Hayo maisha bora yatakuja kwa njia gani kama habari za ufisadi zinatolewa, lakini watawala hawashituki?
Viongozi katika Idara ya Wanyamapori, inawezekanaje wasingiziwe na wote wanaotoa maoni? Hizi sh bilioni tisa zinazotafunwa kila mwaka, hazimgusi Rais Jakaya Kikwete au Waziri Mkuu, Edward Lowassa?
Kuna mapendekezo yaliyotolewa mwaka 1995, miaka 11 sasa, ya kurekebisha idara hii, hayajatekelezwa hadi leo, maana yake ni nini?
Kuna habari kwamba watendaji katika Idara ya Wanyamapori wanalihujumu taifa. Wanashirikiana na wageni kuhodhi sekta ya uwindaji wa kitalii. Vitalu vinatolewa kwa upendeleo kwa wageni. Wazawa wanapewa maeneo kame, hayana wanyama, ili washindwe, kisha ipatikane sababu ya kuwaondoa kwenye sekta hii.
Tajiri mmoja mgeni, na mtoto wake, wanamiliki eneo la uwindaji katika hifadhi ya Selous lenye ukubwa sawa na nchi ya Djibouti. Wamepewa eneo hili huku Watanzania wakizidi kubanwa.
Tayari kuna habari za uhakika kwamba leseni za wageni hawa zinazomalizika muda wake mwaka 2009, zinaongezwa muda tena mwaka kesho! Hii maana yake ni nini? Je, Tanzania iachwe itafunwe tu na wageni, huku wazawa wakiendelea kutaabika na kunyanyasika katika nchi yao?
Mwanafalsafa mmoja katika zama zake aliwahi kusema: “Hakuna kisichobadilika, isipokuwa mabadiliko.” Tunaamini kuwa ni mabadiliko pekee yanayoweza kuifanya Idara ya Wanyamapori iwe na manufaa kwa Watanzania wote.
Idara hii kuendelea kuwa mali ya watu wachache, maana yake ni kuwaumiza Watanzania ambao watakuwa na haki ya kuihoji Serikali ya Rais Kikwete mwaka 2010.
Moja ya mambo yanayoyaangamiza mataifa maskini ni kuendeleza sera za kulindana. Kama kuna viongozi walioshindwa kazi, au wanaolinda masilahi yao, badala ya masilahi ya taifa, kinasubiriwa kitu gani kuwarekebisha? Kama polisi kumerekebishwa, na bado kazi hiyo inaendelea, huku Idara ya Wanyamapori kuna kitu gani kisichogusika?
Je, wabunge ni waongo? Wafadhili ni wazushi? Kamati ya Bunge iliyotoa maoni mazito yaliyoainisha uoza ndani ya idara hii, ina chuki binafsi? Wananchi ni wenye wivu? Kwa nini viongozi waandamizi hawataki kuirekebisha idara hii ili iwanufaishe Watanzania wote?
Panapofuka moshi, kuna moto. Lisemwalo lipo, kama halipo laja. Sauti ya wengi ni sauti ya Mungu. Haiwezekani idara hii isemwe na kila mtu, kila asasi, lakini serikali pekee iendelee kuikumbatia.