KAMPUNI ya Barrick Tanzania inayomiliki mgodi wa dhahabu wa North Mara, imesema inakwazwa kupanua uwekezaji wake nchini kutokana na watu wachache kwa masilahi binafsi.
Meneja Mkuu wa mgodi huo, Bill MacNevin, aliwaambia waandishi wa habari waliotembelea mgodi huo uliopo eneo la Nyamongo mkoani Mara kuwa kampuni yake inapenda kuona wadau wote wakishirikiana.
“Tunakatishwa tamaa kwa karibu kila kitu cha maendeleo tunachofanya, watu wachache tu wanawachochea baadhi ya wanavijiji ili wasishirikiane nasi,” alisema.
Kauli ya MacNevin ilitokana na taarifa zinazodaiwa kuenezwa na shirika lisilo la kiserikali kuwa mgodi huo umekuwa ukiwalazimisha wanavijiji kuhama ili kupisha uchimbaji wa madini.
Alisema kuwa mgodi wake una mipango mikubwa ya uwekezaji katika eneo hilo, na kuongeza kuwa hilo linaweza kufanyika kama wadau wote watashirikiana na kampuni yake.
“Tuna mipango ya kujenga bwawa kubwa kwa ajili ya kutunza maji machafu kutoka mgodini, lakini watu wawili wamekataa kuhama kutoka kwenye ardhi yao bila sababu yoyote ya msingi pamoja na kutoa fidia kubwa,” alisema bila kutaja kiasi hicho.
Alisema kuwa kampuni yake ina sera ya kuwajengea nyumba za kisasa wanavijiji wanaohama maeneo yao kwa hiari na pia kuwapa fedha nyingi kama fidia.
“Kwa sasa kuna watu wawili tu katika eneo hili wanaomiliki ekari nne tu ambao wamegoma kuhama pamoja na serikali kuwataka wafanye hivyo,” alisema.
Alisema kuwa juhudi za pamoja zinahitajika katika ngazi za wilaya na mkoa kuhakikisha kuwa wawekezaji wanapata mazingira mazuri ya kufanya kazi.
Alisema kuwa mgodi wake umekabidhi sh milioni 100 kwa wanasheria kama dhamana ili wanavijiji wanaohamishwa waweze kulipwa, lakini wanavijiji hao wamegoma.
Barrick Tanzania imewekeza sh zaidi ya trilioni moja. Imeajiri Watanzania 4,511