INAWEZEKANA Rais Jakaya Kikwete, ameona bila kuwa mkali, mambo hayawezi kwenda kama alivyotaka, huku akielekea kubakiza miaka minne, kati ya mitano ya ngwe ya kwanza ya uongozi wake.
Kwa kutambua hilo, ameanza kutoa siku za utekelezaji wa maagizo anayotoa, baada ya kubaini kuwa wanaoagizwa, baadhi yao wanampuuza.
Kwa kuanzia, amewaagiza wakuu wa mikoa ya Mtwara na Lindi, baada ya siku 14, wampe taarifa ya wafanyabiashara ya korosho waliofanya vizuri na waliofanya vibaya katika ununuzi wa korosho.
Alitoa agizo hilo juzi wilayani Masasi, alipokuwa akihitimisha ziara ya kikazi mkoani Mtwara ya kukagua shughuli za maendeleo na mchakato wa ununuzi wa zao hilo.
“Kwa kweli baada ya siku 14 nitataka kupata taarifa, wala msidhani nimesahau, nitataka mniambie kama wanafanya kazi vizuri au la, kama wote wanafanya kazi vizuri sawa, lakini anayefanya kazi vibaya mnyang’anyeni leseni.
“Na muwaambie kabisa, ‘bwana hapa ulipotufikisha, mwakani usihangaike, hutapata leseni tena’,” alisema.
Aliendelea kusema: “Tunaweza kuchuma dhambi, lakini kwa kweli tunaweza kuwashuku wafanyabiashara hawa kwamba shabaha yao sasa ni kuwachosha wakulima, wanachelewa kununua ili wananchi waendelee kusubiri na hatimaye wachoke na kuuza korosho yao kwa bei ya kutupa.”
Rais Kikwete ambaye katika ziara nzima wananchi walikuwa wakimweleza matatizo wanayokumbana nayo kuhusu bei ya korosho, aliwaeleza viongozi wa mikoa hiyo kwamba maagizo yake yanaweza kuwa magumu, na kwamba ugumu wake unatokana na ukweli kuwa baadhi ya viongozi wa mikoa hiyo ni mawakala wa wafanyabiashara hao.
“Maagizo yangu yana ugumu wake, na ugumu wake ni pale wenyewe kati yetu, sisi wenyewe tunapokuwa mawakala. Hapo ndipo watu tutakapoingia kigugumizi. Mimi siingii kigugumizi kwa sababu si wakala wa mtu yeyote, nitaendelea kuwakumbusha tu,” alisema.
Alisema ni lazima viongozi wasimame imara katika utoaji wa uamuzi, kwani wasipofanya hivyo watu watadhulumiwa.
“Serikali lazima isimame upande wa wanyonge, ikisimama upande mwingine wanyonge hao hawana pa kukimbilia.
“Sasa wale ambao kati yetu ni mawakala wa kununua, mnaishi kwa uwakala, mnapata riziki kwa uwakala, wahimizeni wafanyabiasha wachangamke, waambie ‘mzee mambo yameharibika, wenyewe wamekuja juu’,” alisema.
Rais Kikwete aliwataka viongozi wa mikoa wasingoje, bali waandae orodha ya wanaostahili kunyang’anywa leseni