Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Wafadhili nao washtukia ubadhirifu Wanyamapori
Wafadhili nao washtukia ubadhirifu Wanyamapori
By Habari Tanzania | Published  11/23/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Mwandishi Wetu

WAFADHILI wameingilia kati na kutaka Idara ya Wanyamapori iliyo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, ifanyiwe marekebisho makubwa kwa vile inatumiwa kuhujumu uchumi wa nchi.

Wafadhili hao kupitia umoja wao wa Kundi la Wadau wa Maendeleo ya Tanzania (DPG), wametoa taarifa wakichambua, wakifichua, wakikosoa, na wakipendekeza mengi yanayopaswa kufanywa. Tanzania Daima imefanikiwa kuipata ripoti hiyo.

Wanasema wazi kuwa utajiri katika biashara ya uwindaji, kama ungekusanywa vizuri, hawaoni ni kwa nini Tanzania isifanikiwe katika MKUKUTA.

Moja ya vikwazo walivyobaini ni uongozi mbovu, hujuma, wizi na usiri mkubwa. Inakadiriwa kuwa kila mwaka sh bilioni 9 zinaingia mifukoni mwa viongozi wa idara kupitia mtandao wao ulioenea hadi serikalini na kwa kampuni kadhaa za uwindaji, ambazo nyingi zinamilikiwa na wageni, na ndizo zilizopewa maeneo manono ya uwindaji.

DGP wanasema ingawa Idara ya Wanyamapori ina ukwasi mkubwa, inaliwa na wachache.

Idara hiyo kwa muongo mmoja sasa, inaongozwa na Emanuel Severe. Miongoni mwa mambo yaliyobainika ni kutotekelezwa kwa mageuzi makubwa yaliyopendekezwa na kukubaliwa tangu mwaka 1995 ya kuifanya idara iendeshe mambo kwa uwazi na kwa haki.

Mapema mwaka huu, Severe aligongana na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Anthony Diallo, baada ya kugoma kuhamishwa.

Baadaye Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, alihusishwa na kutohama kwa Severe, akidaiwa kuwa ni rafiki yake mkubwa.

Luhanjo alikanusha madai hayo, na kusema Diallo hakufuata taratibu za kiutumishi za kumwondoa Severe, kwa vile mwenye mamlaka hayo ni Rais pekee.

Chini ya uongozi wa idara hiyo, wageni wamemilikishwa maeneo manono ya uwindaji, huku mmoja akimiliki eneo katika Hifadhi ya Selous ambalo ukubwa wake ni sawa na nchi ya Djibouti.

Wabunge wamepiga kelele nyingi kuhusu uongozi na mfumo mzima wa idara hiyo, lakini kama ilivyotarajiwa, serikali imeendelea kutia pamba masikioni.

Sasa wafadhili, kupitia DPG, nao wameanza kuanika uoza katika idara hiyo, na kushauri mageuzi makubwa na ya haraka yafanyike. Taarifa yao inapatikana pia kwenye mtandao wa www.tzdac.or.tz.

Wanasema: “Sekta ya uwindaji imekuwa ikikua kwa kasi katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, na hivyo kuifanya Tanzania iwe moja ya nchi zinazoongoza kwa uwindaji wa kitalii duniani.

“Pamoja na ukuaji huo, Idara ya Wanyamapori inahitaji kufanyiwa mabadiliko makubwa ya kimenejimenti, ukusanyaji mapato na kuinufaisha jamii.”

Wafadhili hao wanasema kuwa kwa sasa hakuna mwongozo mzuri katika sekta ya uwindaji wa kitalii kutokana kuhodhiwa na kundi la watu wachache wanaolindwa na viongozi serikalini.

Chini ya idara hii, upotevu wa mapato na jamii za vijijini kutofaidika ni moja ya kasoro kubwa. Upendeleo kwa wageni na kuwaacha wazawa, ni mambo yaliyobainika na hivyo kuifanya iwanufaishe zaidi wageni.

Ada inayotozwa kwa shughuli za uwindaji, ni ya kiwango cha chini nchini Tanzania kikilinganishwa na nchi nyingine zinazopakana na Tanzania.

Wafadhili hao wamebaini kuwa idara inaendeshwa na kudhibitiwa na mtandao ambao si rahisi kwa mtu mwingine kujua kinachoendelea ndani yake.

Wanaosemwa ni raia wa kigeni ambao wamekumbatiana na baadhi ya viongozi ndani ya idara na serikali.

Kwa uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima, imebainika pasi na shaka kwamba, tayari kundi la wageni wanaohodhi zaidi ya nusu ya vitalu vyote vya Tanzania, wameanza mikakati ya kupata leseni baada ya muda wa leseni za sasa kumalizika mwaka 2009.

Kwa kawaida, leseni mpya huanza kutolewa miaka miwili kabla ya muda wa mwisho wa leseni. Kwa utaratibu huo, mwaka 2009 ndiyo mwisho wa leseni za sasa, lakini tayari kumefanyika vikao vya siri, vikiwahusisha wawindaji hao wageni na baadhi ya viongozi waandamizi ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii ili leseni zianze kutolewa mwaka kesho.

Wafadhili kwenye taarifa yao wamesema usiri mkubwa uko ndani ya idara, na ni kikundi kidogo tu cha waandamizi katika idara hiyo ndicho kinachoweza kuielewa sawasawa.

Suala la uwazi na ushindani katika sekta hiyo na njia nyingine ambazo zingeweza kuiboresha sekta ya uwindaji zimekuwa zikikabiliwa na vipingamizi kutoka ndani ya Idara yenyewe ya Wanyamapori.

Hali hiyo imeelezwa kwamba inatokana na baadhi ya viongozi hao ‘kutiwa mifukoni’ na baadhi ya wageni wenye kampuni za uwindaji.

Kwa mfano, mpango wa sera na utawala wa uwindaji wa kitalii ulibuniwa, ulisainiwa na kukubaliwa na Mkurugenzi wa Wanyamapori mwaka 1995, lakini haujatekelezwa hadi leo, ikiwa ni miaka 11.

Mpango huo unahusisha pamoja na mambo mengine, mageuzi mahususi ya sekta ya uwindaji wa kitalii na kuruhusu ushindani ambao ni halali.

Wafadhili wamesema: “Kutokana na kutokuwapo kwa mfumo wenye uwazi katika utoaji wa vibali vya umiliki wa maeneo ya uwindaji kwa sekta binafsi, kwa sasa vibali hutolewa kwa gharama isiyoendana na soko halisi.

“Vibali havijali ukubwa wa eneo, ubora wa eneo wala ukubwa wake katika kuzalisha mapato. Hayo yote hufanywa na maofisa waandamizi wa serikali ambao huwa na mamlaka ya utoaji wa vibali.

“Ufedhuli huu huipotezea Tanzania mapato mengi, inakadiriwa kuwa mapato yanayopotea ni dola za Marekani zaidi ya milioni saba.

“Idadi ya kampuni za uwindaji na watalii wanaokuja kuwinda, inaongezeka nchini Tanzania, wakati mapato katika Idara ya Wanyamapori yamebakia pale pale, au yameshuka.

“Zaidi ya asilimia 70 ya vitalu vyote hutolewa kwa wawindaji ambao huvikodisha kwa wasio na uwezo wa kuendesha shughuli za uwindaji,” imesema ripoti hiyo.

Baadhi ya athari za kuuziana vitalu ni kwa serikali kukosa mapato yanayotokana na biashara hiyo, lakini kubwa zaidi ni hatari ya wanyama kuuawa bila kufuata sheria endapo mnunuzi wa kampuni hana sifa zinazotakiwa.

Kwa kawaida, kabla ya kampuni kupewa leseni, moja ya masharti huwa ni kutaka kujua uwezo wake wa kuendesha biashara hiyo ili asiue wanyama ovyo. Kampuni inapouzwa pamoja na vitalu, huchukuliwa na watu ambao hawakufanyiwa uhakiki na Idara ya Wanyampaori; jambo ambalo ni ukiukaji wa sheria.

“Menejimenti ya sasa ya sekta ya wanyamapori na hasa sekta ya uwindaji ni mfano wa kasoro zilizopo katika utawala, lakini ikiwa inafaidisha masilahi ya muda mfupi ya walio wachache, hasa wanaoshikilia vibali vya uwindaji na maofisa wachache wa serikali, kutokana na kuwanufaisha, hufanya kila njia kukwamisha mageuzi.

“Mfumo wa sasa unahatarisha mkatati wa muda mrefu wa ustawishaji wa sekta hii.

Mfumo huu hautoi haki kwa serikali, wazawa, wala jamii kwa mujibu wa sheria za Tanzania, badala yake unanufaisha kundi la watu wachache katika sekta binafsi ambao wengi ni wageni kutoka nje ya nchi, na walio serikalini,” imesema ripoti.

Hayo yameelezwa kuwa ni matumizi mabaya ya maliasili yanayosababishwa na kutokuwapo mfumo mzuri wa soko ambalo kwa sasa linaendeshwa na kundi la viongozi serikalini, hasa katika Wizara ya Maliasili na Utalii, hususan Idara ya Wanyamapori.

Wafadhili wamependekeza yafanyike mabadiliko ya haraka kwenye sekta ya uwindaji wa kitalii, ili utajiri huo uweze kuwanufaisha Watanzania wengi.

“Bila kuwapo kwa mfumo unaoeleweka wa sekta ya uwindaji, matatizo yatakayoikabili yatakuwa makubwa zaidi,” imesema.

Utafiti uliofanywa na Wizara ya Fedha juu ya Menejimenti ya Idara ya Wanyamapori unaweza kutumika kuleta mabadiliko ya udhibiti wa fedha za sekta hiyo ambazo sasa zinaliwa na kundi la wachache serikalini.

Wafadhili hao wameshauri Wizara ya Fedha iwe na utaratibu wa kufanya ukaguzi katika Idara ya Wanyamapori ili kuleta mabadiliko kwenye udhibiti wa fedha za umma.

Pia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imependekezwa ihusishwe juu ya utaratibu wa utozaji kodi wa sekta binafsi unaohusisha uwindaji


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by James)
    Rating
    Hawa ndio waandishi tunaowahitaji kwa maslahi ya Taifa sio wale wa kupika Majungu na kuishushia hadhi fani hii.
    Kwa kweli maliasili ni kichefuchefu kabisa,hizi njaa na tamaa za wachache zinaharibu jian na sifa za Taifa na hivyo kushindwa kuwapata "serious investors" wenye nia ya kutusaidia Umma wa Watanzania.Keep it Up Writter !!!
     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.