Na Muhibu Said
BARAZA Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata), limeonya juu ya njama zinazodaiwa kuandaliwa na wanaharakati wa Kiislamu, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuliteka na kuliweka baraza hilo chini ya himaya yao.
Kamishna wa Tume ya Mufti wa Tanzania, Sheikh Khamis Mataka, alitoa onyo hilo alipokuwa akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana.
Sheikh Mataka, ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Bakwata Taifa, alisema baraza lake linazo taarifa sahihi juu ya njama zinazoandaliwa na wanaharakati hao, kwa kutumia mwavuli wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania kutaka kuliteka na kuliweka baraza hilo chini ya himaya yao.
Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu, Issa bin Shaban Simba, alikiri pia kuwa na taarifa za njama hizo zinazoandaliwa na wanaharakati hao, lakini hakuwa tayari kuelezea kwa undani suala hilo.
Sheikh Mataka, alisema njama hizo wamezibaini kupitia taarifa zilizosambazwa na wanaharakati hao katika vyombo vya habari na mitaani wakitangaza mpango wa kufanya kongamano kujadili hatima ya Bakwata na mali zinazosimamiwa na baraza hilo.
"Tunasema, jambo hilo hatutalivumilia kabisa," alisema Sheikh Mataka ambaye hata hivyo hakueleza ni hatua gani watakazozichukua kukabiliana njama hizo.
Alisema jaribio la kuliteka Bakwata si jambo jipya katika historia ya baraza hilo na kutoa mfano kwamba lilikwishawahi fanywa na wanaharakati hao kwenye miaka 1990 bila mafanikio.
Alisema baada ya kufeli, wanaharakati hao waliamua kuachana na Bakwata na kuamua kuunda baraza lao waliloliita Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania (BARAZA KUU).
Sheikh Mataka, alisema Bakwata haitosambaratika kama inavyodaiwa na baadhi ya watu na badala yake inachokifanya hivi sasa ni kuboresha utendaji wake, ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua kwa matatizo yote yanayotokea.