Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Agizo la Lowassa halitekelezeki
Agizo la Lowassa halitekelezeki
By Habari Tanzania | Published  11/22/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated

Na Waandishi Wetu

AGIZO la Waziri Mkuu, Edward Lowassa la kutaka kipindupindu kiwe kimekwisha ndani ya wiki mbili zijazo, halitekelezeki kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo uchakavu wa miundombinu ya majisaf,i ambao umekuwa ukisababisha maji hayo kuchanganyika na majitaka.

Sababu zingine, ni msongamano wa nyumba ambao unazuia magari yanayotoa huduma ya kunyonya majitaka kushindwa kufika katika maeneo ambayo ugonjwa huo umekuwa tishio.

Pia wakazi wa baadhi ya maeneo wanalazimika kutumia maji ya visima vifupi kutokana na pampu zinazotumia nguvu za umeme kushindwa kufanya kazi kutokana na tatizo la umeme, ni sababu nyingine iliyotajwa kuwa ni kikwazo kikubwa cha utekelezwaji wa agizo hilo la Lowassa, kutokana na mgawo wa umeme unaondelea.

Ugonjwa huo ambao umekuwa ukilipuka mara kwa mara, hivi sasa umekuwa tishio nchini, hususan katika maeneo kadhaa ya jijini Dar es Salaam.

Watu kadhaa wamekwisha kuripotiwa kufariki dunia na wengine kulazwa katika vituo mbalimbali vya afya vilivyoko katika maeneo mbalimbali ya wilaya mkoani humo.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mnyamani, Kata ya Buguruni, jijini Dar es Salaam, Mbaraka Ulanga, alisema zipo sehemu katika mtaa wake ambako mabomba yanayotoa majisafi yametoboka, hali ambayo imekuwa ikiyapa mwanya majitaka kupenya na kusababisha mabomba hayo kutiririsha majisafi yaliyochanganyika na maji machafu.

Alisema tatizo la msongamano wa nyumba na ukosefu wa maeneo ya kujenga vyoo, limekuwa likisababisha pia baadhi ya wakazi kulazimika kutapisha vyoo na wengine kuvifungulia wakati mvua zinaponyesha.

Alisema hali hiyo imekuwa ikisababisha majitaka yaliyochanganyika na kinyesi kusambaa katika maeneo mbalimbali.

"Ndio sababu utaona magonjwa mengi hukithiri katika kipindi cha mvua. Kipindi hicho tumekuwa tukipokea malalamiko kutoka kwa wakazi wengi kuhusu tatizo hilo," alisema Ulanga.

Maeneo ambayo yamekithiri kwa matatizo hayo katika mtaa wake, aliyataja kuwa ni Kwa Mkanda, eneo la katikati na Bondeni Kwa El-Hamza ambako alisema hakuna barabara inayoruhusu magari kupenya na kufika katika eneo hilo.

Chanzo kingine kinachosababisha mlipuko wa ugonjwa huo, alisema ni majitaka yanayotiririka kutoka katika mabomba ya magari yanayotoa huduma ya kunyonya maji hayo.

Alisema tatizo hilo linachangiwa na wahusika kushindwa kudhibiti mifuniko ya mabomba hayo, hali ambayo imekuwa ikisababisha magari hayo kutiririsha majitaka sehemu yanakopita.

"Tatizo hilo limekwishawahi kulalamikiwa na tumewahi kuyakamata baadhi ya magari kwa kitendo hicho, lakini hadi sasa bado linaendelea," alisema Ulanga.

Kutokana na hali hiyo, Ulanga, aliwataka watu waliosambaza maji ya visima kuhakikisha mabomba yao hayavujishi maji ili kuepuka majisafi kuchanganyika na majitaka.

Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Bugurni Kisiwani, Fatuma Moto, alisema ni vigumu kwa kipindupindu kumalizika katika kipindi kilichotajwa na Lowassa kwa kuwa mazingira katika maeneo mengi katika mtaa wake, kiusafi, ni mabaya.

"Mtiririko wa maji machafu, uchakavu wa mabomba, kutokupatikana majisafi, mkondo wa mifereji ya majitaka kuelekea kwenye mabomba ya majisafi, visima kutokuwa na kina kirefu, vyoo kuwa karibu na kisima, ni katika vyanzo vikubwa vinavyosababisha mlipuko wa mara kwa mara wa kipindupindu katika mtaa huu," alisema Fatuma.

Alisema sababu nyingine, ni mfereji mkubwa unaopita katika eneo la Mtaa wa Buguruni Kisiwani kuelekea katika bonde Msimbazi kutumiwa na baadhi ya watu kutupa takataka na kuzibulia vyoo.

Mjumbe wa Kamati ya Mazingira na Afya ya Serikali ya Mtaa wa Buguruni Kisiwani, Godfrey Molandi, alisema mfereji huo umepasuka na baadhi ya wakazi wametengeneza kienyeji bomba la majisafi katika eneo hilo ambalo hutoa majisafi yaliyochanganyika na majitaka.

Alisema sababu nyingine inayochangia mlipuko wa kipindupindu, ni wananchi kutokupewa elimu juu ya ugonjwa huo na kamati za mazingira kutokuwezeshwa kutoa elimu hiyo kwa wananchi.

Katika hatua nyingine, wamesema Serikali na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wasisubiri kuchukua hatua za kuzuia ugonjwa wa kipindupindu ukiishaenea, badala yake uwekwe utaratibu wa kufanya kampeni madhubuti ya kudumu kwa kuwa tatizo hilo linaonekana kuwa sugu.

Wananchi hao waliitaka Serikali iweke utaratibu wa kudumu wa kuielimisha jamii kuhusu kanuni za usafi ili kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa hatari wa kipindupindu.

Walisema utaratibu wa kuelimisha viongozi wa mitaa na kata peke yao hautoshi kuutokomeza ugonjwa huo, kwani kuelimisha jamii inahitaji gharama ambayo viongozi peke yake hawawezi kuimudu.

"Kuelimisha viongozi tu haitoshi, waelimishwe wananchi juu ya kanuni za usafi kwa ujumla," alisema Mwinyimbegu Millundi, ambaye ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Madenge, Kata ya Buguruni.

Millundi alisema ugonjwa wa kipindupindu si suala la dharura bali ni suala endelevu, hivyo kuitaka Serikali kupambana nalo siku hadi siku na si kusubiri mlipuko wa ugonjwa huo utokee.

Aidha Millundi alisema hatua zilizochukuliwa na manispaa kupiga marufuku biashara ya baa na chakula sio suluhisho la tatizo hilo, kwani walishafanya hivyo eneo la Vingunguti ambako vilabu vya pombe vilifungwa lakini idadi ya wagonjwa wa kipindupindu iliongezeka.

Naye Omary Fereji, Mkazi wa Ilala Mchikichini aliwalalamikia viongozi wa kata na mitaa kuwa si wafuatiliaji na kudai kuwa kama wangewahimiza na kuwasimamia wananchi kufuata kanuni za usafi, tatizo hilo lisingekuwapo au lingekuwa na madhara kidogo sana.

Mwananchi ilitembelea maeneo ya Buguruni na Ilala na kukuta wananchi wakiishi katika mazingira machafu kutokana baadhi ya nyumba kutokuwa na mahala pa kutupia takataka pamoja na mvua kidogo iliyonyesha jijini juzi kusababisha maji kutuama.

Nayo Kata ya Manzese imeanza kuchukua hatua za kuutokomeza ugonjwa wa kipindupindu kufuatia agizo la Lowassa ili kuutokomeza ugonjwa huo ndani ya wiki mbili.

Akizungumza na Mwananchi jana asubuhi, Afisa Mtendaji wa Kata ya Manzese, Pius Milanzi, alisema kampeni ya usafi ilianza Novemba 18 mwaka huu na kwamba hatua zinazofanyika sasa ni kuwaelimisha wakazi wa eneo hilo na kufanya ukaguzi katika kila kaya.

Utekelezaji wa kampeni hiyo ni pamoja na kukagua vyoo, utiririshaji wa maji machafu ya vyooni, kutoa ilani kwa wafanyabiashara wa vyakula na uboreshaji wa mifereji ya kupitishia maji machafu.

Mfanyabiashara mmoja wa Soko la Tandale, Suleiman Ahmed aliwaambia waandishi wa habari kuwa hali ya usafi wa soko hilo hairidhishi na kwamba ni hatari kwa afya yao na anaunga mkono agizo lililotolewa na Waziri Mkuu.

Mwananchi ilipita katika baadhi ya maeneo ya Tandale na Midizini na kujionea hali halisi ya uchafu kwenye makazi ya watu na maeneo ya biashara, hasa za vyakula ambavyo ndio chanzo kikubwa cha mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.

Hata hivyo uongozi wa serikali za mitaa umeagiza kuwa kufikia Desemba 9 mwaka huu, wawe wamefanikiwa kuutokomeza ugonjwa huo kwa asilimia 99 katika Kata ya Manzese na kuiomba Serikali kuwapatia vitendea kazi, kwani walivyonavyo sasa havitoshi.

Imeripotiwa na Muhibu Said, Jimmy Tara, Gloria Shetui na Godfrey Katiligi


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.