Na Mwandishi Wetu
Kampuni ya Umeme Tanzania (Tanesco) ikiwa inakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha hadi kuomba msaada serikalini, maafisa wake watatu wamefikishwa mahakamani wakidaiwa kuiba karibu Sh2bilioni za shirika hilo.
Waliofikishwa jana katika Mahakana ya Kisutu jijini Dar es Salaam, ni Afisa Utawala, Gloria Lima (36) pamoja na Mhasibu, Martin Semng’indo (36) na Mhasibu Msaidizi, Salvatory Kimaro (36), wote wakiwa ni waajiriwa wa Tanesco na wakazi wa Dar es Salaam.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya wizi wa fedha taslimu, jumla ya Sh1, 969, 342, 508.70.
Akisoma hati ya mashitaka, mbele ya Hakimu Michael Luguru, Mwendesha Mashtaka, Mrakibu wa Polisi, Naima Mwanga, alidai kuwa kati ya Novemba 1, 2004 na Februari, mwaka huu, Kimaro aliiba fedha taslimu Sh189,789,710 mali ya shirika hilo.
Aliendelea kudai kuwa kati ya Novemba 1, 2004 na Februari mwaka huu, Lima aliiba fedha taslimu Sh1,242,380,926.45 nazo mali ya shiraka hilo.
Pia alidai kuwa kati ya Novemba 1, 2000 na Desemba 22, 2005, Semng’indo aliiba fedha taslimu Sh 537,176,872.25 mali ya shirika hilo la usambazaji umeme.
Alidai kuwa washitakiwa hao walifanikisha wizi huo kwa kutumia nyadhifa zao wakati wakiwa waajiriwa wa shirika hilo. Hata hivyo, washitakiwa walikana shitaka hilo.
Upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na Hakimu Luguru aliiahirisha kesi hiyo hadi Desemba 5 itakapotajwa tena.
Alitawataka washitakiwa hao kuwa na wadhamini wawili wanaominika ambao watasaini hati ya dhamana ya Sh 30 milioni.
Kesi hiyo iliwahi kufikishwa mahakamani hapo Juni 7, mwaka huu, lakini washitakiwa hao waliondolewa bila kusomewa mashitaka kwa sababu ambazo hazikufahamika, hadi jana waliporejeshwa tena kizimbani kusomewa mashitaka.
Kesi hiyo imekuja wakati shirika hilo likiwa katika ukata mkali, ambapo limewasilisha serikalini maombi ya Sh300 bilioni ili kujinusuru chini ya mpango wake uliobatizwa Tanesco Financial Recovery Programme.
Pia shirika hilo sasa linakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha kutokana na makusanyo hafifu yaliyosababishwa na mgawo mkali wa umeme ambao umedumu kwa karibu miezi sita sasa nchi nzima.