Na Ansbert Ngurumo, Huli, UKNimesoma maneno ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Edward Lowassa) dhidi ya gazeti la Tanzania Daima wiki hii, Sikuamini!
Nimebaki kujiuliza: Hivi Lowassa anaogopa nini? Mbona inaonekana na anajitambulisha, kuwa jasiri na shupavu? Mtu mwenye mamlaka makuu kama yeye, ambaye anakaimu madaraka ya Rais mara kadhaa anaweza kutishwa na gazeti, halafu akahamaki hadharani?
Kwa nini Lowassa anashindwa kuwa mvumilivu? Kwa nini haamini uwezo wa wengine katika kufikiri na kutafsiri hali, matukio, maneno na hisia? Kwa nini anadhalilisha waandishi kwa kudhani kwamba hawana akili na kutafsiri kauli za wanasiasa?
Kwa nini anataka kujenga misingi ya matumizi mabaya ya madaraka? Kwa nini atumie cheo chake kuwaonea na kuwatisha wanyonge? Anataka wasio na madaraka waishi vipi? Kwa nini anakuwa mbabe hivyo? Na kwa nini anatumia fedha za walipa kodi wa Tanzania kutangaza alivyotangaza magazetini? Bado najiuliza. Kwa nini?
Katika toleo lake la Novemba mosi, Tanzania Daima liliandika habari kuu yenye kichwa cha habari: Kisingizio kingine cha Serikali kutohamia Dodoma; likimnukuu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Maafa na Ukimwi), Dk. Luka Siyame, akijibu swali bungeni kwamba mojawapo ya sababu zilizoifanya serikali ishindwe ‘kuhamishia shughuli zake’ Dodoma ni upungufu katika sheria ya ustawishaji wa makao makuu.
Sheria Na. 7 ya 1989 ya kuvutia uwekezaji katika Eneo Maalumu la Mji wa Makao Makuu Dodoma ililenga kuhamasisha uwekezaji katika mji wa Dodoma katika maeneo muhimu ya ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma mbalimbali za kijamii, kiuchumi na usafirishaji; ili pamoja na mambo mengine, kujenga na kuboresha mazingira ya mji huo ili kuuwezesha kumudu idadi kubwa ya watu iliyotarajiwa kuongezeka kutokana na shughuli za kibinadamu na wale waliotarajiwa kuhamia katika mji huo. Sababu kubwa ya ongezeko hilo la watu ni hadhi ya Dodoma, ambayo ilitangazwa kuwa makao makuu ya Tanzania mwaka 1973.
Gazeti limetafsiri swali la mbunge na jibu la Serikali. Limeona kushindwa kwa serkali kuhamia Dodoma. Limekuwa lisikia sababu za serkali inapojitetea kwa nini haijahamia Dodoma. Likisema hiki ni kisingizio.
Sioni kilichomkasirisha Waziri Mkuu, hata akalipatia gazeti siku tano liombe radhi kwa kuandika habari hiyo, kwa jinsi hiyo, huku taarifa yake, iliyosambazwa katika magazeti mengi nchini, ikisisitiza; “vinginevyo suala hili litafikishwa kwa mamlaka inayohusika na masuala ya usajili na uratibu wa vyombo vya habari kwa hatua za kinidhamu.”
Hivi ni vitisho! Ni matumizi gani haya ya nyadhifa? Ni ubabe! Na huyu si mwandishi wa Waziri Mkuu. Ni mwandishi wa Tanzania Daima; na hiyo ndiyo tafsiri yake ya habari hiyo.
Wakati Waziri Mkuu akitaka gazeti liombe radhi, taarifa yake ya vitisho imekuja na kisingizio kingine, ikisema eti. “hali ngumu ya uchumi wa nchi yetu” ndiyo sababu kubwa ya kukwama kwenda Dodoma.
Nasikitika kusema kwamba vitisho hivi haviijengi nchi, ofisi ya Waziri Mkuu wala Lowassa mwenyewe, ambaye majuzi aliahirisha Bunge kwa mbwembwe na kusoma utenzi wa “Tupo Tumejaa Tele,” akitambia umakini, umaridadi, ushujaa na uadilifu wa viongozi wa serikali ya sasa.
Nahisi Lowassa anajua kuwa kauli yake si hitimisho la mjadala wa Watanzania juu ya watawala wetu mmoja mmoja na serikali kwa jumla. Hivyo ndivyo anavyojiona. Lakini awaache na wengine waseme wanavyomuona. Na asiwatishe. Hata akiwatisha, hataondoa kile wanachokijua, bali atakuwa amewaongezea sifa yake ya ziada.
Nami nasema, ndiyo mpo, lakini waoga! Hamjatuonyesha kwamba mnaweza kuishi bila nguvu ya vyombo vya habari. Hamjaonyesha kwamba mpo tayari kujibu maswali yo yote yanayojitokeza, bila kwanza kujifungia ndani, kutunga majibu na kuweka msimamo.
Ndiyo, mpo; lakini mnapenda sana sifa. Inakuwaje serikali adilifu, yenye dhamira njema na dhamana iliyopewa iogope kuandikwa gazetini? Inakuwaje Waziri Mkuu, kiongozi wa tatu kwa ukubwa nchini anayeweza kuja kumrithi Rais Jakaya Kikwete (mwenyewe atathibitisha kwa vitendo) aogope habari ndogo kama hiyo gazetini?
Yawezekana gazeti limekosea. Nani asiyekosea? Kama yeye ana taarifa sahihi, haitoshi kulikosoa bila kutoa vitisho na kudokeza ‘kulifuta’ au ‘kulifungia’ kwa kutumia sheria dhalimu? Na kama habari inayolalamikiwa inatokana na majibu yaliyotolewa bungeni, Ofisi ya Bunge imeshindwa kufanya kazi yake?
Na kama kweli ofisi yake imekosewa haki, anashindwa nini kulipeleka gazeti katika Baraza la Habari Tanzania; ukweli ukasemwa, uongo ukakemewa? Anataka kuficha nini? Anatahadharisha nini? Kwamba asiguswe kamwe?
Nani amemwambia kwamba wahariri hawana haki ya kutafsiri maswali ya wabunge na majibu ya serikali? Kwa nini? Waandishi si kasuku; wala si makarani wa watawala.
Mtu akichunguza majibu ya serikali, akasoma habari gazetini, atahisi kuna jambo ndani ya moyo wa Waziri Mkuu au serikali dhidi ya gazeti husika. Si rahisi kuamini kwamba Lowassa amekerwa na habari hiyo tu, basi.
Ama kuna kitu anataka kukilinda ndani ya serikali, au kuna kitu anataka kubomoa katika gazeti husika. Yawezekana amefungua mlango wa watu kuchunguza hatima ya vitisho hivi. Na kwa hakika, wachambuzi waanze sasa kangalia kule ambako Lowassa anataka kulifikisha Tanzania Daima.
Mbona yapo mambo mengi yamekuwa yakiandikwa na vyombo vingi vya habari - yenye uzito mno kwa nchi kuliko hilo? Mbona si mara ya kwanza watu kuhoji serikali kushindwa kuhamia Dodoma? Nini maana ya kuhamishia shughuli za serikali Dodoma, kama si kuhamisha makao makuu? Ni kipya gani ambacho Tanzania Daima limeandika, kinachoiudhi serikali au Lowassa kiasi cha kutaka kutumia sheria hizo dhidi yake?
Na hapa imesemwa tu serikali - na si mara ya kwanza. Ingekuwaje, kama gazeti lingeibua kashfa binafsi ya Lowassa au kiongozi mwingine wa serikali? Ni kitu gani kinamzuia Lowassa kutambua kuwa hii ni mojawapo ya huduma ambazo jamii inazitegemea kutoka kwa vyombo vya habari? Kwa nini hajui kwamba umakini wa vyombo vya habari katika kuweka bayana udhaifu wa serikali ni njia ya kuipa changamoto serikali kutekeleza wajibu wake kwa wananchi? anataka kutuambia kwamba anaongoza serikali isiyowajibika kwa wananchi?
Mbona nimemsikia mara kwa mara akiimba kwamba hizi ni zama za ari mpya, nguvu mpya, na kasi mpya? Kwa nini afikirie kwamba wananchi hawapaswi kuwa na ari, nguvu na kasi hiyo hiyo kuhoji na kujua mipango ya serikali yao?
Na kwa nini wasiseme pale wanapogundua haijatekeleza wajibu wake sawa sawa? Kwa nini hajui kwamba gazeti ni mdomo, masikio, moyo na macho ya wananchi? Kwa nini anataka kila mmoja aone, asikie, aguswe, ahisi kwa kutumia nyenzo za serikali?
Yeye si ni mmojawapo wa waliojipanga nyuma ya Rais Kikwete kuwatangazia wananchi jinsi wanavyodhamiria kushamirisha demokrasia? Si hawa hawa waliokuwa wakiucheka na kuubeza utawala wa Rais Benjamin Mkapa kwa ubabe dhidi ya vyombo vya habari? Wamekuja na lipi jipya kwa wanahabari na wananchi wanaopenda uhuru wa kuwasiliana?
Anatarajiaje kukuza demokrasia bila kuwaachia watu wafikiri, wazungumze, waandike, wahoji, watafakari na kuchambua mambo kadiri wanavyoyaona? Kwa nini wanataka kulazimisha magazeti yachuje habari nyeti kama hizo, zifike kwa wananchi zikiwa rojorojo? Kwa nini viongozi wetu wanataka kushiriki kuharibu dhana ile ile waliyoapa kuilinda?
Ni kitu gani kinawazuia kujifunza kutoka kwa nchi nyingine zilizoendelea, zinazojua umuhimu wa vyombo vya habari; zinazotambua kuwa ofisi za viongozi na madaraka yao ni mali ya wananchi? Kwa nini hawaoni wivu kwamba zipo nchi - tena nyingine jirani zetu - zinazotumia vyombo vya habari kufichua kasoro, uzembe na kashfa nyingine za watumishi wa serikali, ili zirekebishwe jamii ipate huduma iliyokusudiwa?
Vyovyote ilivyo, Lowassa anashindwaje kuona uhusiano kati ya swali lililoulizwa na ustawishaji wa Makao Makuu Dodoma? Hapana. Nakaribia kuamini kwamba kuna jambo limejificha katika hatua yao hiyo dhidi ya Tanzania Daima.
Najiuliza zilipokwenda mbwembwe za kwamba serikali hii ni kipenzi cha wanahabari! Marafiki gani wanaotishana? Marafiki gani wanaodharauliana? Naye si mmoja wa vinara wa serikali hii ambayo inajidai haina la kuficha?
Lakini wanaomjua Waziri Mkuu huyu wanasema hakuna jipya katika huluka yake kwa wanahabari. Hawamwambii, lakini nao wanamjua - na kwa hakika, wanamwogopa; na wanamlalamikia chini chini. Hata baadhi ya mashabiki wa mtandao wameanza kusema kuwa kwa tabia hii, ‘atamharibia’ Rais Kikwete.
Wanasema Kikwete ni mkali lakini mvumilivu; Lowassa - mkono wa kuume wa Kikwete -ni mbabe, asiyependa kukosolewa. Wanasema ana dharau kwa taaluma ya habari, huku ajibidisha kuwakumbatia wahariri na wamiliki wa vyombo hivyo.
Haamini kwamba waandishi wanajua, wanasikia, wanatafakari, wanachambua, wanatafsiri na kueleza kile wanachoamini kwamba ni habari. Haamini kwamba wana taaluma nyeti kwa ustawi wa taifa. Anataka waone kama yeye, wafikiri na waamue kama yeye. Vinginevyo, wamekosea!
Labda anaamini kwamba waandishi ni makarani wa wanasiasa walio madarakani - yeye akiwamo. Na kama anakubali kwamba ni waandishi, basi haamini kama wana uwezo wa kufanya kazi yao bila kusimamiwa na serikali. Kwa muda mrefu, inasemwa Lowassa amekuwa akifanya kazi ya ‘uhariri wa habari’ zinazomhusu yeye, wizara yake au serikali yake. Waandishi wananong’ona pembeni; lakini hawapendi!
Tabia hii imemfanya atambulike kama kiongozi ‘asiyeandikika’, na wengine wanadai pia kwamba wapo viongozi katika serikali hii ambao ni mahiri wa ‘kubandua’ habari zinazowasema vibaya gazetini kwa kutumia simu tu, au kushinikiza waombwe radhi, wasafishwe ikishatoka; na wanaoaminika ‘kuwapenda’ waandishi kama wanamshughulikia mshindani wake.
Waandishi wana mifano ya wenzao walioshughulikiwa na uongozi wa vyumba vyao vya habari kwa kuandika habari au makala zilizowaudhi watu hawa. Hii si sifa nzuri kwa viongozi.
Wanajua jinsi kiongozi wao huyu ‘anavyochukia’ waandishi wachache wanaojitegemea kimawazo na kimsimamo; wasiopenda kupangiwa habari za kuandika na kuendeshwa kama watoto wadogo.
Na si waandishi pekee. Hata wanajamii wanaofuatilia mambo wanadiriki kusema kuwa serikali hii inaongozwa na watawala wenye udhaifu wanaoficha udhaifu wao kwa kujizungushia magazeti ili yawapambe, waonekane wanaweza. Ni serikali inayotaka kuwa na waandishi wa habari wanaoshabikia kila kitu kinachofanywa na serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM)!
Katika taarifa yake yenye vitisho dhidi ya Tanzania Daima, Waziri Mkuu hakusita kutaja magazeti mawili anayodhani yameandika vizuri habari anayolalamikia. Moja ni la serikali, jingine linaelezwa kuwa la rafiki yake, na kiongozi mwandamizi wa CCM. Tutarajie nini?
Katika mwaka wake wa kwanza madarakani, anazungumziaje uvumilivu wa mtangulizi wake, Frederick Sumaye, ambaye alirushiwa makombora kwa miaka zaidi ya saba mfululizo ili asigombee urais?
Lowassa hajui zilikotoka shutuma dhidi ya Sumaye? Hawajui waliozipeleka kwenye vyombo vya habari? Hashangai kwa nini Sumaye hakujisafisha kwa gharama ya biashara na ajira za wengine?
Tunakoelekea, kama Lowassa na rafiki zake wataendelea na ubabe huu, magazeti jasiri yatafungiwa. Waandishi wenye msimamo watafukuzwa kazi au watawekwa kizuizini. Sitashangaa baadhi yao wakipoteza maisha.
Kwa kuogopa ukweli utokanao na ukali wa kalamu, waandamizi wa CCM na maswahiba wa viongozi wakuu wa serikali wameanza kununua hisa katika kampuni nyingi ya habari, ili kuwa na uwezo wa kudhibiti, kuendesha na kupanga ajenda za kusifia serikali na kujipanga vizuri. Tunajenga taifa gani?
Wote wanajua - Lowassa akiwa mmojawapo - kwamba wamevitumia, wakati mwingine bila vyenyewe kujua kwamba vinatumika. Si ajabu wasingefika hapo walipo bila nguvu ya vyombo vya habari. Si ajabu wasingewabomoa waliokuwa wanashindana nao kama si kwa nguvu ya vyombo hivyo. Yawezekana fursa hiyo imewawezesha kujua udhaifu wa vyombo hivyo. Ndiyo maana hawaviheshimu?
Tukubaliane. Hii ni dharau. Haikubaliki. Hawataki tuseme, na tumeshasikia tetesi za kuwafungia wasioufyata; lakini tutazidi kuwasema kwa sababu wao ni mali zetu; na tuna haki juu yao. Tunataka wawajibike kwa faida ya taifa. Sisi ndiyo wapiga kura na uongozi wao ni dhamana tuliyowapa. Ni katika misingi hiyo hivyo ndiyo maana wabunge tuliowachagua sisi ndiyo waliotuwakilisha wakati walipopiga kura ya kuidhinisha uteuzi wake Lowassa wa kuwa Waziri Mkuu. Mmoja wa marafiki zangu alipata kuandika; “Kuna nini katika uwaziri mkuu? Mbona kila aliyepata kupita hapo aliharibikiwa?