.Mfanyabiashara maarufu jijini Arusha mbaroni
Na Mohammed Mhina, Polisi, Moshi
MTANDAO wa matajiri wanaonunua magari ya wizi umenaswa na mfanyabiashara maarufu amekamatwa.
Kunaswa kwa mtandao huo kumefuatia kukamatwa kwa watuhumiwa watatu wa uporaji wa gari mkoani Tanga ambao waliwaeleza jinsi mtandao huo unavyoendeshwa.
Maelezo ya watuhumiwa hao, yaliiwezesha polisi mkoani Kilimanjaro, juzi kubaini kuwepo kwa mtandao wa matajiri wanaonunua magari ya wizi na kumkamata mfanyabiashara maarufu wa mjini Arusha, Mariki Makindi (34) kwa kuhusika na mtandao huo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Lucas Ng’hoboko, alisema Makindi ambaye ni mkazi wa eneo la Mbauda mjini Arusha, alikamatwa akiwa kwenye hoteli moja iliyopo karibu na kituo cha mabasi cha zamani cha mjini hapo akiwa katika harakati za kuwasubiri watuhumiwa waliokwisha kamatwa ili wampelekee gari.
Ng’hoboko alisema mtuhumiwa huyo ambaye ni hatari, alikutwa akiwa na gari moja dogo lenye namba za usajili T.741 ADP aina ya Toyota Corola Exive aliyouziwa Septemba 3, mwaka huu.
Alisema mkataba wa gari hilo lililouzwa kwa sh. milioni 1.3 kwa tajiri huyo, ulikutwa kwa mmoja wa watuhumiwa hao hali inayoonyesha huenda hata gari hilo, aliuziwa na watuhumiwa hao.
Kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kunatokana na ushirikiano ulionyeshwa na watuhumiwa hao ambapo walimtaja Makindi kuhusika na ununuzi wa magari ya wizi.
Ng’hoboko aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Mohammed Rashidi (25), Abdallah Rajabu (26) wakazi wa Arusha na Henry Joseph (26) ambaye ni fundi magari wa jijini Dar es Salaam.
Alisema watuhumiwa walikamatwa Moshi, kufuatia taarifa za polisi mkoani Tanga kuhusiana na kuibwa kwa gari moja mjini Muheza aina ya Toyota Mark II yenye namba za usajili T. 766 AKG.
Kamanda alisema utaratibu unafanywa ili kuwasafirisha watuhumiwa hao kwenda Tanga kuendelea na upelelezi ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.