Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mufti akana kufukuza masheikh mikoani
Mufti akana kufukuza masheikh mikoani
By Habari Tanzania | Published  11/20/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated

Na Mwandishi Wetu
MUFTI wa Tanzania, Sheikh Mkuu, Issa bin Shaban Simba, amekuja juu na kukanusha taarifa zilizotolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu Taifa ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata), Alhaj Habib Ndassiwa, zinazowaagiza makatibu wa mikoa na wilaya wa baraza hilo kuomba upya nafasi wanazozishikilia.

Mbali na taarifa hiyo, taarifa nyingine iliyotolewa na Alhaj Ndassiwa katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya Bakwata Jumatatu wiki iliyopita ambayo imekanushwa pia na Mufti Simba, ni ya kusema kwamba baraza hilo halijawahi kufanya ukaguzi wa mahesabu kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita.

Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya Bakwata, jijini Dar es Salaam jana, Mufti Simba, alisema taarifa zilizotolewa na kiongozi huyo si sahihi kwa kuwa ni kinyume na maazimio yaliyopitishwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya baraza hilo, kilichofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

"Siwalaumu waandishi waliotangaza habari hizo, bali ninayemlaumu ni mtoa taarifa," alisema Mufti Simba.

Alisema tofauti na taarifa zilizotolewa na Alhaj Ndassiwa, kilichoazimiwa na Halmashauri Kuu katika kikao chake, ni kuwaagiza makatibu wa mikoa na wilaya wa Bakwata kupeleka maelezo yao binafsi (CV) makao makuu ya baraza.

Alisema azimio hilo lilipitishwa na Halmashauri Kuu ili kulipa baraza sura kamili za watumishi na watendaji wake na kuwafahamu wenye uwezo wa kulisaidia.

Kuhusu taarifa kwamba, Bakwata halijawahi kufanya ukaguzi wa hesabu zake kwa zaidi ya miaka 20, Mufti Simba alisema taarifa hizo hazina ukweli kwa kuwa Tume ya Halmashauri Kuu Taifa ya baraza hilo ilikwisha kupewa kazi ya kukagua mali za Waislamu katika kipindi cha miaka iliyopita.

Alhaj Ndassiwa, alitoa taarifa hizo sambamba na kutangaza kuwafukuza kazi viongozi saba wa Bakwata, akiwamo Naibu Katibu Mkuu, Alhaj Mohamed Ramiya na kusema kwamba, ni katika maazimio ya kikao cha Halmashauri Kuu Taifa ya Bakwata ambayo yameridhiwa pia na Mufti Simba.

Pamoja na mambo mengine, viongozi hao walituhumiwa kuiba mamilioni ya shilingi ya baraza hilo na tende zilizotolewa na Ubalozi wa Falme za Kiarabu nchini kama msaada kwa Waislamu kwa ajili kifungua kinywa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.