Na Mwandishi Wetu, Mtwara
RAIS Jakaya Kikwete ameeleza kukerwa kwake na mgomo wa wanunuzi wa korosho na kusema serikali inawatafutia jawabu.
Alitoa kauli hiyo jana baada ya wakazi wa Wilaya ya Mtwara Vijijini kumpokea kwenye baadhi ya maeneo aliyopita kwa mabango yanayoshutumu soko huria la korosho wakati akielekea kukagua uzalishaji wa gesi katika eneo la Msimbati.
Akihutubia wakazi wa Msimbati na wa Mtwara Mjini kwa nyakati tofauti, alisema pamoja na serikali kukubali sharti la wanunuzi wa korosho la kutaka baadhi ya kodi kuondolewa, ili waweze kununua zao hilo kwa Sh 600 kwa daraja la kwanza na 480 daraja la pili, wengi wamegomea bei hiyo bila maelezo.
"Natambua kuwepo kwa tatizo la kucheleweshwa ununuzi wa korosho. Ucheleweshaji umesababishwa na wanunuzi, baadhi ya kodi zimeondolewa wasiponunua, basi dhamira yao itakuwa ni kudhulumu," alisema Kikwete katika mkutano wa hadhara mjini Mtwara.
"Ninawasihi waje kununua. Ningependa nipate taarifa kwamba kasi ya ununuzi imeongezeka, tusipoiona baada ya miaka miwili watapata majibu, " alisema.
Huku akionyesha kukerwa na wanunuzi hao, alisema, "tunatafuta jawabu na naamini tutalipata." Hata hivyo alisema tatizo hilo limetokana na kufa kwa vyama vya ushirika ambavyo vilikuwa na wajibu wa kununua mazao.
Aliwataka viongozi wa Mkoa wa Mtwara kukaa na kutafuta njia za kuimarisha vyama vya ushirika kuliko kuwa mawakala wa wanunuzi ambao wakati mwingine wamekuwa wakitumia vipimo vinavyowapunja wakulima.
Alisema makubaliano ya awali baina ya wakulima na wanunuzi yalikuwa ni kununua korosho za daraja la kwanza kwa Sh 600 lakini bila ya sababu za msingi, wanunuzi waliamua kugomea bei hiyo.
Mapema Waziri wa Kilimo, Steven Wasira, alikiri mbele ya wananchi wa Msimbati baada ya kuona mabango ya wananchi njiani yanayolalamikia bei ya korosho, lakini alisema serikali haijihusishi na kupanga bei na kwamba hiyo ni kazi ya wakulima na wanunuzi.
"Najua kwamba hamjauza korosho, tunaendelea kushauriana na wanunuzi ili waje kwa bei iliyokubalika," alisema Wasira.
Hata hivyo, aliwataka wakazi wa mikoa inayozalisha zao hilo kuendelea kupanda mikorosho inayofaa na kwamba suala la bei ni jambo la muda mfupi wakati serikali ikitafuta suluhisho la kudumu.
Zao la Korosho ndio zao kuu mkoani hapa na kwa mujibu wa takwimu zilizopo, inakadiriwa kuwa mwaka huu uzalishaji ulikuwa ni tani 60,000, lakini hadi sasa ni tani 8,341 tu ndio zimenunuliwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Henry Shekifu, pamoja na serikali kukubali kuondoa ushuru wa Sh15 uliokuwa ukilipwa kwa vijiji, bado kuna tani 51,659 za zao hilo ambazo hazijanunuliwa.
Taarifa hiyo inaonyesha kuwa hali ni mbaya kwa wakulima wa Wilaya ya Masasi ambao hadi sasa wameuza tani 2,000 tu kati ya 25,000 za korosho zilizozalishwa msimu huu