Waandishi Wetu, Dar na mikoani
MATUMAINI ya Watanzania kupata nafuu ya maumivu ya mgawo wa umeme yanazidi kupungua, baada ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kutangaza kuwa sasa mgawo huo umeongezeka mpaka usiku.Hatua hiyo ya Tanesco imeibua hisia tofauti miongoni mwa wananchi, baadhi yao wakiona kuna usanii unaofanywa na baadhi ya watendaji ndani ya shirika na serikali, kutaka kuwaibia Watanzania kupitia zabuni za kuzalisha umeme wa dharura.Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya wananchi walisema kuongezeka kwa makali ya mgawo wa umeme kunathibitisha kwamba ndani ya Tanesco kuna matatizo makubwa, lakini serikali haitaki kusema ukweli.
Mkazi wa Mwananyamali Kwa Msisiri, Samia Karim, alihoji sababu za kuongezeka kwa makali ya mgawo hivi sasa baada ya kikao cha bunge kuahirishwa wiki iliyopita.Kutokana na hali hiyo, alisema ana wasiwasi huenda tatizo hilo limetokana na baadhi ya watendaji ndani ya Tanesco na serikali kutaka kujinufaisha kutokana uzalishaji wa umeme wa dharura."Serikali iseme ukweli, tatizo ni nini? Na kwanini limetokea baada ya Bunge kwisha? Kwa nini lisiwepo wakati Bunge linaendelea? Hapa kuna mchezo mchafu umepita," alisema Samia.
Zebadayo Kairuki, mkazi wa Keko Magurumbasi, jijini Dar es Salaam, alisema tangazo la Tanesco, linaonyesha kwamba tatizo lililopo ni kubwa na serikali haitaki kuzungumza ukweli.Kairuki alidai kuwa habari za ndani alizonazo ni kwamba, Tanesco inakabiliwa na hali mbaya fedha za kuiwezesha kununua umeme.Alisema karibu Sh 80 bilioni zinahitajika kuiwezesha Tanesco kununua umeme angalau katika mwezi huu na mwezi ujao, lakini hadi sasa fedha hizo imekuwa ni mtihani mkubwa kuzipata."Serikali haiko 'serious' katika kulitafutia ufumbuzi wa kudumu tatizo la umeme, haitaki kuchukua maamuzi, inachofanya ni kuwafurahisha watu kwa hivi 'vimgao' vidogo vidogo vya umeme," alisema Kairuki.
Naye Charles Masaburi, aliishauri serikali kufungua mjadala wa wiki moja utakaotoa fursa kwa wananchi kujadili kwa uhuru na serikali iseme ukweli kuhusu tatizo hilo.Kutoka Moshi, wananchi mbalimbali wakiwemo wasomi, wameitaka serikali kulitangaza tatizo la umeme nchini kama janga la kitaifa ili mataifa mbalimbali yenye uwezo yaweze kuisaidia nchi kutatua tatizo hilo. Wakizungumza na Mwananchi mjini hapa jana, wananchi hao wamedai kuwa hata ziara za Rais Jakaya Kikwete nje ya nchi kwa ajili ya kuvutia wawekezaji hazina maana yoyote kama nishati ya umeme hakuna. "Nani atakuja kuwekeza kwenye nchi ambayo haina umeme, ni vema rais na watendaji wake wakaachana na ziara hizo na fedha wanazotumia zitumike kutafuta suluhisho la kudumu,ˇ¨alisema Jacob Kilati wa Moshi Mjini.
Kilati, ambaye ni fundi mtaalamu wa injekta pampu, nozzle na turbo, maarufu kama Kadogoo, alisema mgawo huo wa umeme utazidisha makali ya maisha mara dufu ili kufidia gharama za umeme wa jenereta. Kwa upande wake, Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Dk Lyatuu alisema "Katika hali hii wananchi wataumia sana lazima serikali ichukue hatua.
" Dk Lyatuu alihoji kwanini jenereta ambazo zimekuwa zikipigiwa chapuo kuwa ndio zingemaliza tatizo la mgawo wa umeme na serikali zimeingia na kufungwa nchini lakini nini hazimalizi makali ya umeme. Wakili mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alitahadharisha serikali ya Kikwete kuwa mwaka 2010 isitumie kisingizio cha umeme kushindwa kutekeleza ahadi zake na kuitaka iwe makini.
"Kama tuliweza kulazimishwa kuwa hata kula majani tutakula ilimradi ndege ya Rais inunuliwe, wanashindwa nini leo kutangaza kwamba tujifunge mkanda ili suala la umeme litatuliwe? hatutaki bla bla,ˇ¨alisema wakili huyo. Kutoka Arusha baadhi ya wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda wameiomba serikali kuingilia kati hatua ya Tanesco kutaka kuongeza makali ya mgao wa umeme hadi nyakati za usiku kwani hali hiyo itazidi kuua uchumi wa nchi.
Wakizungumza na Mwananchi jana, wamiliki wa viwanda kadhaa na wafanyabiashara jijini hapa, walisema kitendo cha kutaka kurefushwa mgao wa umeme kinadhihirisha kuwa serikali imeshindwa kabisa kulipatia ufumbuzi tatizo la umeme nchini."Serikali lazima sasa iwe makini na hili, haiwezekani mgao uwe hadi usiku kwani tayari viwanda kadhaa jijini hapa vilifungwa kwa tatizo hili na hivi basi uzalishaji utasimama katika karibu viwanda vyote. Ni hasara kubwa kwa wafanyabiashara na serikali," alisema Mkurugenzi wa kiwanda cha Nyirefarm LTD, Robert Nyirenda.
Nyirenda alisema athari za tatizo hilo zitaokena muda mfupi ujao kwani kodi kadhaa hazitalipika tena, uchumi utashuka kwa kasi kubwa na umaskini, badala ya kupungua kwenye jamii, utaongezeka."Sasa tunalazimika kununua jenereta kubwa za kisasa sisi hatukuweka kwenye bajeti yetu matumizi haya, tatizo hili linamaanisha fedha za kodi na nyinginezo ndizo zitanunua mashine, sasa tutapata wapi fedha za kulipa kodi ya serikali," alisema
Nyirenda.Mfanyabiashara Jackson Minja na Abdi Hussein wote wa mjini Arusha, ambao wanamiliki vituo kadhaa vya huduma za kompyuta, walisema mgao wa umeme hadi nyakati za usiku sasa utalazimisha kufungwa kwa shughuli zao."Tumekuwa tukifungua saa 12.00 jioni sasa kama mgao ukiongezeka tutafunga kwani wastani wa sasa umeme unapatikana kati ya siku tatu na nne kwa wiki kwa saa 12," alisema Hussein.
Alisema hadi sasa wamefunga baadhi ya vituo vyao vinavyojiendesha kwa hasara na kwamba kwa tangazo hili jipya la Tanesco, watalazimika kufunga vituo vingine na kupunguza tena wafanyakazi.Hata hivyo, tangu tatizo la mgao wa umeme lianze, viwanda kadhaa vya nguo na vingine jijini hapa, vimepunguza idadi ya wafanyakazi sambamba na maduka ya kuuza samaki na kuku mengi yamefungwa.
Wakati huo huo, baadhi ya wanasanyasi hapa nchini wametaka uwekezaji katika sekta ya nishati uangaliwe kwa makini zaidi kwani utaendelea kutilia hasara taifa. Akizungumza katika mkutano wa 13 wa mwaka wa wanasayansi uliofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa Hoteli ya Mkonge jijini Tanga, mmoja wa wanasayansi hao kutoka mkoani Kilimanjaro, Emiani Temu, alisema viko baadhi ya vipengele ambavyo si vya lazima katika mikataba ambavyo serikali haipaswi kukubaliana nayo.
Alitolea mfano wa mradi wa gesi wa Songosongo ambao huzalisha gesi na kisha kuisafirishwa mpaka kwenye mitambo ya umeme ya Ubungo jijini Dar es Salaam, akisema ungeweza kuzalishwa mkoani Lindi kuingizwa katika gridi ya taifa.Alisema gharama za utandazaji mambomba katika mradi mzima pamoja na matumizi ya vifaa vingine, zingeweza kuepukwa ili kuipa nafuu Tanesco kununua gesi kwa bei kubwa.
Hata hivyo, Afisa wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), James Ngereja, ambaye alisema hatua ya serikali kutegemea uzalishaji wa umeme kwa kutumia maji, gesi na mafuta ni ya dharura na kwamba mtazamo wa mbele ni kuzalisha umeme kupitia tungamotaka (Biomass) zilizoko nchini.Alisema asilimia 90 ya nishati inayopatikana hapa nchini inatokana na tungamotaka mbalimbali, asilimia nane mafuta, asilimia 1.2 umeme na asilimia 0.8 ni nishati inayotokana na vyanzo mbalimbali.
Alisema ili kupunguza tatizo la nishati, serikali haina budi kutoa fursa kwa wawekezaji kuwekeza katika kilimo cha mashamba makubwa ya miti ambayo mbali ya kuwezesha taifa kupata mbao, pia kutawezesha upatikanaji wa nishati zitakazotokana na takataka za miti hiyo.Rais wa chama cha Wataalam wa Misitu Tanzania (TAF), ambacho ndicho kilichoandaa mkutano huo, Dk Felician Kilahama, alisema ili kunusuru mazingira, serikali haina budi kuanzisha ushuru wa kuhifadhi mazingira kwa wanachama wake wanaotumia maji kuzalishia bidhaa kama vile vinywaji ili fedha zitakazopatikana zitumike kuhifadhi mazingira.
Katika mkutano huo, wanasayansi hao wamekubalina kuanzisha Baraza la Wataalam wa Misitu litakalosimamia shughuli za misitu ikiwa ni pamoja na kuwadhibiti wataalam wa misitu wanaokwenda kinyume na miiko ya taaluma hiyo.Kutoka Mufindi, Hakimu Mwafongo anaripoti kuwa kiwanda cha Karatasi cha Mufindi (MPM) kinatarajia kuiuzia Tanesco umeme wa megawati 15 ili kupunguza tatizo la umeme nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi mdogo wa mikutano wa kiwanda hicho juzi, Meneja Mkuu wa kiwanda hicho, Yerra Choudary, alisema lengo lao ni kuzalishaji megawati 46. Alisema hivi sasa uwezo wa kiwanda hicho ambacho hapo awali kilikuwa kikiitwa SPM Mgololo, ni kuzalishaji megawatt 10.4 kwa ajili ya matumizi ya kuendesha mitambo kiwandani hapo.
Choudary alisema mitambo kwa ajili ya uzalishaji wa umeme imeanza kuwasili na mingine itawasili miezi miwili ijayo.Alisema Megawatt 31 zinazobakia zitatumika kwa ajili ya matumizi ya kiwanda hicho baada ya upanuzi mkubwa kufanyika ili kuongeza uzalishaji wa karatasi.Alisema mitambo hiyo itagharimu dola za kimarekani milioni 70 (sawa na zaidi ya Sh88 bilioni) ikijumuisha ununuzi wa mitambo, usafirishaji na ufungaji wake.Alisema baaada ya kuanza uzalishaji wa umeme, mwekezaji wa kiwanda hicho atakuwa amewekeza zaidi ya Sh100 bilioni kwa kuwa tayari Sh25 bilioni ziliztumika kukarabati mitambo ya kiwanda kutoka mfumo wa zamani kwenda wa sasa unaotumia na kuongozwa na kompyuta.
Alisema kwa sasa kiwanda kina uwezo wa kuzalisha tani 130,000 kwa mwaka na soko lake kubwa ni la nje ambalo ni sawa na asilimia 86 ikiwa ni sawa na tani 110,000.Alizitaja nchi zinazonunua karatasi kuoka MPM kuwa ni pamaja na Siera Leone, Iran, Ethiopia, Kenya, Uganda, Zambia, Malawi, Sri Lanka, Singapore, India na Malasia.