Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Sherehe za uhuru miaka 45
Sherehe za uhuru miaka 45
By Habari Tanzania | Published  11/19/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated

WAKATI tunajiandaa kusherehekea miaka 45 ya uhuru wa taifa letu, nimekuwa nikitafakari tangazo la HakiElimu, linalorushwa kwenye luninga na kwenye redio.

Tangazo hili ambalo lina maneno ‘tulia, tafakari na chukua hatua’, linasumbua sana akili yangu. Inawezekana tangazo hili linasumbua akili ya Watanzania wengine.

Tangazo hili linaonyesha au linaeleza kwamba kutokana na takwimu za kitaalamu na kiuchumi, uchumi wetu unaendelea, na Tanzania imepiga hatua kubwa ya maendeleo, lakini hali halisi inaonyesha maisha duni ya wananchi.

Kwenye luninga zinaonyeshwa picha za nyumba mbovu, watu wenye afya na lishe mbaya, wamevaa nguo zilizochanika, wamekata tamaa na kuduwaa kwa kusikia habari za maendeleo ya taifa lao.

Mzee Small, mwigizaji wa siku nyingi, anaonekana akishangaa kwa kulinganisha yale yanayotangazwa na redio kwamba uchumi unakua na hali halisi. Tangazo hili ni muhimu sana wakati huu tunapoandaa sherehe za miaka 45 ya uhuru wetu.

Ni vigumu kukataa ukweli kwamba baada ya miaka 45 ya uhuru Watanzania wengi bado wanaishi maisha duni.

Michango inakusanywa na watu wanahamasishwa kuchanga fedha za sherehe za uhuru. Sote tunaisubiri siku hiyo kwa hamu, siku ambayo taifa letu lilipata uhuru.

Tunasubiri kucheza, kuimba, kunywa na kula. Lakini, ni kweli kwamba uhuru wetu umekuwa uhuru wa kweli, uhuru wa neema kwa kila Mtanzania, uhuru wa kuleta maisha bora na ukombozi wa kila Mtanzania?

Je, si kweli kama tangazo la HakiElimu, linavyoonyesha kwamba kwa nje yanaonekana maendeleo, lakini kwa ndani watu wanaishi maisha duni?

Kuna mafanikio makubwa yaliyopatikana baada ya uhuru. Hata kule kuwa huru ni mafanikio tosha. Lakini mafanikio ya kutuwezesha kufanya sherehe kubwa za kula, kunywa na kucheza, yanatiliwa shaka.

Taifa letu limeweza kudumisha utulivu na amani, tumejenga mshikamano na aina fulani ya uzalendo. Taifa letu limekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa nchi nyingine za Afrika zinapata uhuru wake. Haya ni mafanikio makubwa sana.

Shule zimejengwa, hospitali na huduma nyingi za kijamii zimeendelezwa. Pamoja na mafanikio hayo yote, bado kuna ukweli unaosumbua, kwamba baadhi ya Watanzania bado wanaishi maisha duni. Na namba ya wale wanaoishi maisha duni ni kubwa kuliko ile ya wenye neema!

Kwa nini takwimu zinaonyesha uchumi kupiga hatua wakati hali halisi inaonyesha kinyume? Kwa nini Watanzania wanaishi maisha duni, wakati nchi yetu ina utajiri mkubwa? Tatizo ni nini?

Je, ni kweli tusherehekee sikukuu hii ya uhuru wetu, au tutulie, tutafakari na kuchukua hatua? Hatua gani? Elimu? Ukombozi wa fikra? Siasa safi na uongozi bora? Ni lazima kuna tatizo mahali fulani, na tatizo hili haliwezi kutanzuliwa kwa kula, kunywa na kucheza ngoma!

Baada ya miaka 45 ya uhuru wetu, huduma ya maji bado si nzuri. Watanzania wengi hawajui kwamba dunia ya leo maji yanamfuata mtu, na si mtu kuyafuata maji. Watu bado wanatembea kilomita zaidi ya 10 kufuata maji. Watu hawa hawajui maji ya bomba, hawajui maji ya ndani ya nyumba.

Lakini mbaya zaidi, hata na wale walio na bomba, hizo bomba hazileti maji! Tunajionea kila siku kwenye vyombo vya habari uhaba wa maji katika Jiji la Dar es Salaam na majiji mengine kama Mwanza, ambalo siku za hivi karibuni limekumbana na mgawo wa maji.

Miaka 45 ya uhuru inapita na bado kuna Watanzania wasiokuwa na mwanga nyakati za usiku. Hata bila kuzungumzia umeme, wapo watu wasiokuwa na uwezo wa kununua mafuta ya taa! Wananchi hawa wanatumia mwanga wa jua, hivyo inawalazimu kupata chakula cha usiku kabla ya jua kuzama, ili waweze kutumia mwanga wa jua!

Miaka 45 ya uhuru inapita na bado hakuna kitu hata kimoja ambacho tunakishughulikia vizuri na kwa kujitosheleza. Hatujaweza kushughulikia kilimo chetu na kujitotesheleza kwa chakula.

Hatujaweza kuishughulikia elimu yetu na kuiendesha bila kutegemea misaada kutoka nje ya nchi. Hatujaweza kuendesha viwanda vyetu na kufanya uvumbuzi mbalimbali.

Hatujaweza kuendesha hospitali zetu bila misaada kutoka nchi za nje. Hatujaweza hata kuendesha serikali yetu bila kutegemea misaada na ruzuku kutoka nchi za nje.

Labda mimi ni kipofu, lakini ninatafuta ni kitu gani, hata kama ni kile ambacho hakina kisingizio cha fedha za kigeni, ambacho tunakishughulikia kikamilifu kwa kujitegemea, ni kipi? Kama hakipo, kwa nini tunataka kusherehekea? Kwa nini tunataka kutumia fedha nyingi kula na kunywa, eti tunasherehekea sikukuu ya uhuru wetu?

Kuna haja ya kutulia, kutafakari na kuchukua hatua kama tunavyoelezwa na tangazo la HakiElimu. Kuna mambo mengi ya kujiuliza juu ya uhuru wetu.

Inatosha tu kuwa na uhuru wa bendera na kuendelea na ukoloni mambo leo? Inatosha tu kuwa huru na watu kuendelea kuishi maisha duni? Inatosha tu kuwa huru na kuendeleza mifumo ya kikoloni? Inatosha kuwa huru na kuendelea kupokea misaada kutoka nchi za nje?

Mwalimu Nyerere alijitahidi sana wakati wa uhuru kubadilisha mifumo. Alileta falsafa ya Ujamaa na Kujitegemea na wakati anakaribia kutoka madarakani, alisukuma kwa nguvu zote demokrasia ya vyama vingi.

Wakati Mwalimu, anakazana kuleta falsafa mpya, bado mifumo mingine ilibaki ni ya kikoloni. Katiba yetu ilifanyiwa marekebisho kutoka ile ya mkoloni. Bunge letu liliendeshwa, na bado linaendeshwa kwa mifumo ya kikoloni.

Rais wa nchi alipewa madaraka makubwa na jambo hili bado linaendelea. Mfano, hadi leo hii rais, ndiye anayemteua jaji mkuu, rais ndiye anayeteua Tume ya Taifa ya Uchaguzi nk.

Mfumo wa serikali ya kikoloni, ulikuwa umesukwa, kwa namna ya wakoloni kujilinda na changamoto ya wananchi. Ulikuwa mfumo wa kuwasaidia kutawala kikoloni, kutawala bila demokrasia. Baada ya uhuru, baada ya kumfukuza mkoloni, tulichukua mfumo ule ule wa kujihami, mfumo ule ule wa kuwaogopa wananchi, mfumo wa kuogopa changamoto za wananchi.

Wakati wa mkoloni, kufikiri kinyume na serikali ulikuwa ni usaliti. Wale wote waliofikiri kinyume na serikali ya mkoloni, walionekana kuwa magaidi. Leo hii tupo huru.

Hakuna mkoloni, lakini kuna dalili zote za kutaka watu wote wawe na mawazo yale yale, watu wote wawe wa chama kile kile, kinyume na hapo ni usaliti. Tunawezaje kusherehekea kwa pamoja wakati uhuru wa baadhi ya Watanzania unanyimwa pumzi?

Ni kweli tupo huru. Kwa maana ya kumfukuza mkoloni na kuendesha mambo yetu wenyewe. Lakini kwa maana yenyewe ya neno uhuru, bado tupo chini ya mkoloni, maana hata mbali na kuishi maisha duni, fikra zetu bado zinatawaliwa.

Hili linajionyesha kwenye mijadala inayoendelea – kama ule wa kutumia lugha ya kigeni kufundishia. Watu walio huru hawawezi kujadili kutumia lugha yao au kutoitumia!

Mbali na baadhi ya Watanzania wanoishi maisha duni, kuna kundi jingine la Watanzania wasioipenda nchi yao. Watu hawa wanapora mali za nchi na kuziwekeza nchi za nje, au wanajilimbikizia wao na familia zao. Hawa si sehemu ya mafanikio, bali ni sehemu ya ukoloni mambo leo.

Ni dhambi kubwa kwa watu hawa, waporaji wa mali za taifa, kusherehekea pamoja na Watanzania wanaoishi maisha duni. Uhuru wa waporaji ni tofauti na uhuru wa wazalendo walalahoi.

Hili tangazo la HakiElimu litusaidie kuona kwamba, pamoja na uhuru wetu, pamoja na mafanikio yetu, bado kuna mambo mengi ya msingi ambayo lazima kuyashughulikia kama taifa. Yapo mambo mengi ya kushughulikia ili kuleta uhuru kamili wa taifa letu. Tunahitaji kutulia, kutafakari na kuchukua hatua Badala ya kufanya sherehe kubwa na kutumia fedha nyingi kwa kula na kunywa, ni vyema watu wakafanya mikutano ya majadiliano. Taifa liingie kwenye majadiliano.

Lazima tuangalie sababu ya watu wengi kuendelea kuishi maisha duni. Ni wakati mzuri wa kuanza kufikiria kutengeneza katiba mpya na mifumo mipya inayoendana na uhuru wetu. Tusherehekee kwa kuzama katika fikara


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.