WASAFIRISHAJI na wakulima wa mboga na matunda wameitaka serikali kuandaa programu za mafunzo, yatakayowawezesha kufikia viwango vya kibiashara vilivyowekwa na Jumuiya ya Ulaya (EU).
Akizungumza wakati wa kufunga semina ya kimataifa ya viwango vya matunda na mboga kwa nchi za Ulaya katika Ukumbi wa Golden Tulip, Dar es Salaam juzi, mwakilishi wa Kituo cha Utafiti wa Dawa na Mimea TPRI, Gratian Bambenda, alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu.
Alisema wakulima, wasafirishaji na wadau wengine wanatakiwa kupewa elimu ili kufikia kuzalisha bidhaa zao kwa viwango vinavyotakiwa, vitakavyosaidia kuinua vipato vyao.
Alisema kuwa matatizo katika sekta ya kilimo na matunda yanaanzia tangu kwa mkulima, na wataalamu wa kilimo, wakiwamo watafiti ambao hawana zana bora za kufanyia utafiti.
Bambenda alisema kuna tatizo la ufungashaji bora wa bidhaa zinazokwenda nje ya nchi, na bidhaa za matunda na mboga, hivyo kushusha viwango vya bidhaa hizo.
Mkuu wa viongozi wa Jumuiya ya Ulaya nchini, Frans Baan, alisema kuwa wasafirishaji na wakulima wanapaswa kufuata viwango vilivyowekwa na jumuiya hiyo ili kuhakikisha wanapata soko la nchi hizo.
“Jumuiya ya Ulaya ina jukumu la kuhakikisha usalama wa vyakula kwa wananchi wake, hivyo ni wajibu wao kusimamia viwango vya uzalishaji na usafirishaji kwa kutoa mafunzo ya viwango muafaka vinavyohitajika katika soko la jumuiya hizo,”' alisema