MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema kikundi cha wanasiasa wanaotaka kukwamisha juhudi za Rais Jakaya Kikwete za kutafuta ufumbuzi wa mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar hakina nguvu za kisiasa.
Profesa Lipumba alisema hayo jana alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mnazi Mmoja, mjini hapa, baada ya maandamano ya chama hicho ya kumlaani Rais Amani Abeid Karume kwa kusema hakuna mseto wala mazungumzo yanayoendeshwa kuhusu mpasuko huo.
Profesa Lipumba alisema viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar wanaopita na kukejeli ahadi ya Rais Kikwete hawana nguvu za kisiasa na kwamba kama kweli Rais ataamua kutekeleza ahadi aliyoitoa bungeni Desemba 30, mwaka jana hakutakuwa na athari zozote.
“Chama cha CUF kinatoa mwito kwa ahadi hiyo kutekelezwa kwa muda muafaka ili kuepusha wananchi kushindwa na subira ambayo wameionyesha,” alisema na kuongeza kuwa CUF inazingatia kuwa Watanzania ni binadamu, si malaika na kwamba subira ina kikomo chake.
Alisema iwapo amani na utulivu vitavurugika Zanzibar, basi hata Tanzania Bara kama sehemu ya Jamhuri ya Muungano pia itaathirika.
Alisema Watanzania wanamuunga mkono Rais Kikwete katika ahadi yake hiyo na hatua anazozichukua, lakini CUF inataka kurejewa kwa uchaguzi chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa (UN).
Profesa Lipumba alimrushia madongo Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, kwa kupinga msimamo wa CUF na kusema kuwa anaganga njaa. Alisema yeye kama mlezi wa vyama, hakupaswa kuizungumzia CCM, kwa vile kazi yake kubwa ni kusimamia sheria zinazoongoza vyama hivyo.
Alisema Zanzibar ina rasilimali za kutosha, kama vile ardhi yenye rutuba na mafuta, lakini bado haujapatikana utawala wa kutumikia masilahi ya wananchi.
Alisema mapendekezo ya muafaka wa mwaka 2001 yalitaka chama kitakachokosa rais, kipewe nafasi ya Waziri Kiongozi na kushirikishwa katika kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.
Kwamba Zanzibar inazidi kuwa nyuma kiuchumi kutokana na sera mbovu na kukosa viongozi wenye uwezo wa kutumia vizuri rasilimali zilizopo.
Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema aliyeandamana na Lipumba, alisema Rais Kikwete ndiye anayepaswa kusimamia amani ya kweli Zanzibar, na wala si viongozi wachache wa SMZ.
Alitaka wadhibitiwe kama alivyofanywa mzee Aboud Jumbe na Dk. Salmin Amour, alipotaka kubadilisha katiba ili aendelee kuongoza kwa kipindi cha tatu.
Alisema chimbuko la kuunda serikali ya mseto Zanzibar lilianza Mwalimu Julius Nyerere alipotoa pendekezo baada ya CCM kushinda asilimia 50.2 na CUF asilimia 49 katika uchaguzi wa 1995, lakini viongozi hawakulizingatia.
Alisema Rais Karume alisema hakuwatendea haki wananchi wa Kisiwa cha Pemba, kwa kuteua mtu mmoja tu kutoka Pemba kuwa waziri wakati kuna asilimia 40 kati ya idadi ya watu wa Zanzibar.
Risala ya wananchi wa Pemba ilishutumu utendaji wa Radio Zanzibar na Televisheni ya Zanzibar, kwamba vinaendeleza chuki na upendeleo.
Naibu Mkurugenzi wa Habari, Haki za Binadamu na Mawasiliano ya Umma, Salim Bimani, alisema CUF itaendelea kutetea haki kwa kutumia nguvu zake zote za kisiasa, na ni wananchi wanaoamua wala si mizinga na risasi vinavyoweza kuwaamulia.
Bimani alikumbusha viongozi wa SMZ kujifunza kutokana na yanayowakuta viongozi wa mataifa mbalimbali kama Saddam Hussein aliyehukumiwa kifo kwa kuua raia, Charles Taylor wa Liberia aliyefunguliwa mashitaka kwa makosa ya uhalifu wa kivita na Mengistu Haile Mariam wa Ethiopia anayesubiri kupandishwa kizimbani kwa uovu alioufanya.
Alisema sababu za CUF kutaka uchaguzi urudiwe ni kwamba hapakuwa na uchaguzi huru wala wa haki, kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu, kama wananchi kunyimwa haki ya kujiandikisha kupiga kura na raia kupigwa risasi za moto na kufunguliwa kesi za kisiasa.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad hakuhudhuria, kutokana na kuwa safari nje ya nchi.