SERIKALI ya Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete, inaelekea kukabiliwa na mtihani mwingine, katika mfululizo wa ile ambayo imekuwa nayo tangu iingie madarakani karibu mwaka mmoja uliopita.
Mtihani huo ni biashara na matumizi ya dawa za kulevya, au mihadarati, ambayo sasa inaaminika kwamba ina mikono ya watu wazito, ambao wananchi pamoja na wawakilishi wao bungeni, wanataka wakamatwe.
Hata katika mkutano wa Bunge uliomalizika wiki iliyopita, wabunge waligusia kwa uchungu hali hiyo, na kutaka hatua zichukuliwe haraka kuwanasa wahusika. Kama mwangwi wake, kada mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisema mwanawe ni mmoja wa waathirika, na kwamba atasaidia kuwataja wanaojihusisha na biashara hiyo chafu.
Mtu aliyevalia njuga zaidi kuzuiwa kwa biashara hiyo, kwa sababu yoyote ile iwayo, ni Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Chifupa (CCM), ambaye alifikia hatua ya kusema kwamba hata kama mumewe, Mohamed Mpakanjia, anajihusisha na biashara hiyo akamatwe na achukuliwe hatua.
Kumekuwapo na taarifa kwamba, alipata kuwaelekeza polisi sehemu mihadarati inapouzwa, lakini aidha walipuuza, au hawakuamini taarifa zake, kwa sababu hawakuchukua hatua yoyote.
Hata hivyo, baada ya wimbi la wiki iliyopita, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba, alisema watazifanyia kazi taarifa hizo, na kwamba watamlinda, ambapo tayari kuna taarifa kwamba wahusika wa biashara hizo wamemtishia maisha.
Baadhi ya wabunge walieleza kusikitishwa kwao na jinsi polisi wanavyovuta miguu katika kuwakamata watuhumiwa wa uuzaji wa dawa za kulevya, na kusuasua katika kuendesha kesi zao.
Biashara ya dawa za kulevya inaaminika kuwa imekithiri nchini, na wahusika hujishughulisha na shughuli nyingine kwa ajili ya kuficha kile hasa kinachowaingizia kipato.
Rais Kikwete mwenyewe amekiri hadharani kwamba ameshakabidhiwa orodha ya wahusika wa biashara hiyo hatari, na kwamba amekabidhi majina hayo kwa vyombo vinavyohusika kwa ajili ya kuchukua hatua.
Rais alieleza kwamba, majina yakitajwa huwezi kuwakamata mara moja wahusika, kwa sababu ni wazi kuna uwezekano kwamba wengine wanasingiziwa kwa sababu ya kuwapo chuki dhidi ya wanaotajwa.
Hata hivyo, katika siku za karibuni, kumekuwa na taarifa za kunaswa kwa baadhi ya watuhumiwa, na mmoja wao anayedaiwa kubobea, alielezwa kukamatwa Novemba 13, akatarajiwa angefikishwa mahakamani juzi Ijumaa, lakini hadi mwisho wa saa za kazi, hakuwa amefikishwa kushitakiwa. Inaelezwa kwamba mtuhumiwa huyo anashikiliwa katika Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam.
Taarifa nyingine zimeeleza kwamba, baadhi ya wafanyakazi wa shirika la ndege wanashikiliwa na askari wa kitengo cha kuzuia dawa za kulevya, wakituhumiwa kuruhusu uwanja wa ndege kutumiwa kupitisha mihadarati.
Yapo madai yasiyothibitishwa pia, kwamba baadhi ya watu hutumia nyadhifa zao kusafirisha dawa hizo, iwe kuziingiza nchini au kuzipeleka nje, jambo linalozidi kuwa mwiba kwa jitihada za kuzuia biashara na matumizi yake.
Maelezo mengine ni kwamba, watu wa kawaida kama wauza magazeti na wang’arisha viatu, wamekuwa mawakala wa kuuza dawa hizo, huku wakijificha kwenye mwamvuli wa biashara hiyo.
Meya wa Manispaaa ya Ilala, Abuu Jumaa, amenukuliwa akisema ameshapata taarifa hizo na ametoa miezi mitatu kwa wahusika wa biashara hizo, ambao hawakuhamishwa katika operesheni ya safisha jiji, wajirekebishe, kwa sababu mienendo hiyo ni kinyume cha kazi wanazodai kufanya.
Watu hao wametiwa kwenye kikaango, wakidaiwa kwamba wamegeuza maeneo yao ya biashara kuwa vijiwe vya watu kulundikana bila sababu, akisema wanawafuga watu wasiofanya kazi, jambo ambalo ni hatari.
Hata hivyo, tatizo kubwa halipo kwa watu hao ‘wadogo’, bali kwa vigogo wanaodaiwa kujihusisha na biashara hiyo, kwa sababu kuna uwezekano wa watekelezaji wa sheria kushindwa kuwachukulia hatua, kutokana na kuwapo madai ya kulindwa na wakubwa.
Suala la biashara na matumizi ya mihadarati limeshika chati, wakati serikali ikiwa katika jitihada za kutatua matatizo mengine makubwa nchini – ukosefu wa umeme unaosababisha matatizo ya kiuchumi na kuongezeka kwa uhalifu kulikodhibitiwa na sasa kutaka kuchipuka tena.
Kampuni kadhaa zimeingia mkataba na serikali, kwa ajili ya kuzalisha umeme kufidia upungufu uliotokana na kushuka kwa kina cha maji kwenye mabwawa makubwa ya kuzalisha umeme, hivyo kulazimika kufunga Bwawa la Mtera.
Kwa upande wa uhalifu, polisi wamejitahidi kuzuia ujambazi uliokuwa ukiambatana na kujeruhi au kuua watu, lakini katika wiki za karibuni unaelekea kuibuka tena.
Katika kuongeza nguvu kwenye mikoa iliyokithiri kwa uhalifu, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Saidi Mwema, amemhamishia mkoani Kagera, aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Venance Tossi, aliyemwelezea kufanya vema kazi yake katika kupambana na majambazi na dawa za kulevya kwa miezi minane aliyokuwa Kilimanjaro. Kagera imekithiri kwa vitendo vya utekaji magari, uporaji na uuaji.