Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Ramadhan Semtawa  »  Bandari yajitetea kuhusu meli
Bandari yajitetea kuhusu meli
By Ramadhan Semtawa | Published  11/18/2006 | Ramadhan Semtawa | Unrated

Na Ramadhan Semtawa

MAMLAKA ya Bandari Tanzania (TPA), imejivua lawama kwa kutoa ufafanuzi kwamba, udhaifu wa pampu za meli za mafuta ndiyo chanzo cha kudorora kwa kasi ya upakuaji mafuta kwenye mita maalum za mamlaka hiyo Kurasini (KOJ).

Udhaifu huo wa pampu za meli unatokana na uwezo wa mita za Bandari (Flow Meters) wa kupitisha mafuta kuwa mkubwa ikilinganishwa na uwezo wa pampu za meli hizo.

Katika ufafanuzi wake wa maandishi kwa gazeti hili, uliotolewa jijini Dar es Salaam jana na Meneja Uhusiano wa TPA, Franklin Mziray, mamlaka ilisema si mita wala kompyuta za mita zake zinazochelewesha upakuaji, bali ni meli zenyewe.

Ndani ya ufafanuzi huo, mamlaka ilisema uwezo wa pampu za meli ndicho kipimo cha kuhakikisha uharaka katika upakuaji wa mafuta.

TPA imekiri kwamba mwaka 1958 ilipojengwa KOJ, ilikuwa na uwezo mdogo wa kupakua mafuta ambayo ni tani 18,000 lakini mfumo huo umekuwa ukiboreshwa mwaka hadi mwaka kutokana na maendeleo ya kiuchumi nchini na nchi jirani.

Ikitaja maboresho ya uwezo wa mfumo huo, mamlaka ilisema mwaka 1985 hadi 1990 ilifanya ukarabati mkubwa na kuiongezea gati uwezo wa kuhudumia meli kubwa kutoka tani 18,000 hadi 30,000.

Maelezo hayo ya TPA yanafafanua zaidi kwamba, mwaka 1993/05 KOJ ilikarabatiwa na kufikia kiwango cha kuhudumia meli za hadi tani 45,000 na mwaka 1995/08 ilijengwa gati ndogo ya kuhudumia meli za mwambao, kuongeza kasi ya upakuaji mafuta zenye uwezo wa kubeba hadi tani 5,000.

Kutokana na kuboresha mfumo huo, uwezo wa juu wa mitambo na mita kwa sasa katika kupokea na kusoma umeongezeka hadi kufikia mita za ujazo 740 kwa saa, ambao unaweza kutumiwa na asilimia 4 tu ya meli za mafuta zinazoingia katika gati ya KOJ.

"Kwa mantiki hiyo, si mita wala kompyuta zake zinazopunguza kasi ya upakuaji mafuta, bali uwezo mdogo wa pampu za meli ndicho chanzo."

TPA pia imetoa ufafanuzi wa meli nne zilizokwama nje ya KOJ kwa kusema hiyo inatokana na kushindwa kukamilisha taratibu za mamlaka hiyo, ikiwa ni pamoja na malipo ya gharama ambayo hata hivyo, haikuyataja.

Imezitaja meli hizo na shehena zake kwamba ni Alexandra Park iliyoingia nje ya mlango wa bandari Oktoba 25 ikiwa na tani 24,103 za mafuta yatokanayo na petroli.

Meli nyingine ni Oversea Rimar iliyoingia Novemba 5, yenye tani 26,813 za mafuta yatokanayo na petroli, Jasmine iliyoingia Novemba 7 ikiwa na tani 14,000 pia za mafuta yatokanayo na petroli na nyingine ni Bow Plata iliyoingia Novemba 12, ikiwa na tani 13,500 za mafuta yatokanayo na mimea.

TPA imefafanua zaidi kwamba, meli ya Alexandra Park na Oversea Rimar, ziliingiza shehena nchini bila kuagizwa na kwamba mwenye mzigo amefahamika kama Chevron.

Hata hivyo, hadi juzi tani 11,000 kati ya 13,103 za Alexandra Park zilikuwa zimekwishapata wateja wakati meli hiyo ikisubiri kukamilisha taratibu, wakati meli ya Hulda hadi jana ilikuwa ikipakua shehena baada ya kukamilisha taratibu.

Hivi karibuni aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Masoko, Nazir Karamagi, alilieleza Mwananchi kuwa tatizo la msongamano wa meli bandarini hapo linatokana na wafanyabiashara wa mafuta kuingiza meli nyingi ndogo ndogo.

Karamagi alisema hilo si tatizo pekee, kwani waagizaji wa mafuta wana mtindo wa kuagiza meli ndogo ndogo nyingi za mafuta zinazosababisha msongamano usiostahili.

Aliongeza kuwa mitambo ya kusafisha mafuta ya Zambia inafanyiwa matengenezo, jambo linalosababisha nchi hiyo kuhitaji mafuta yaliyosafishwa kutoka bandari ya Dar es Salaam.

Alisema ili kupunguza tatizo hilo, kinachotakiwa ni kuzungumza na waagizaji wa mafuta kupitia chama chao, ili wale wanaochukua mafuta kutoka eneo moja, washirikiane kukodi meli moja kubwa badala ya kuleta nyingi ndogondogo kama wanavyofanya sasa.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.