Na Mwandishi Wetu
IDADI ya watalii wa kigeni wanaoingia nchini imeongezeka kutoka 582,807 mwaka 2004 hadi 612,754 mwaka jana.
Ongezeko hilo limeongeza mapato kutoka dola za Marekani 746.02 milioni mwaka 2004 hadi dola 823.59 mwaka jana ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 10.12.
Matarajio ya mwaka 2006/07 ni kupata watalii wa kigeni 700,000 ambao wataliingizia taifa dola 900 milioni.
Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti ya utalii ya mwaka 2005, juhudi za kutangaza vivutio vya utalii Tanzania bado ni ndogo ukilinganisha na sehemu nyingi duniani na kuwa fedha zinazotengwa na serikali kwa ajili ya kazi hiyo ni ndogo.
Ripoti hiyo imelinganisha juhudi za kutangaza utalii baina ya nchi na nchi, na kubaini kuwa katika bajeti ya mwaka jana, wakati Bodi ya Utalii Tanzania ilitengewa dola 1.5 milioni, Bodi ya Utalii ya Kenya ilipewa dola 15 milioni, Afrika Kusini dola 150 milioni wakati Malaysia ilitengewa dola 100 milioni.
Ripoti hiyo imebainisha zaidi kwamba, watalii wengi ambao huingia nchini hutumia usafiri wa njia ya anga na kwamba mwaka jana walikuwa ni 330,587 ikilinganishwa 257,195 waliotumia usafiri huo mwaka 2004.