Na Mwandishi Wetu
WAFANYABIASHARA wawili wa duka la nyama, David Maungo (29) na Edward Galagaja (22) wakazi wa Tegeta, Kinondoni juzi wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakidaiwa kuwauzia wateja nyama yenye uzito pungufu.
Mwendesha Mashtaka kutoka Wakala wa Vipimo, Moses Mbunda, alidai mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Said Msuya kwamba washitakiwa walitenda kosa hilo Novemba 12, mwaka huu huko Tegeta, jijini.
Mbunda alidai Mahakamani hapo kwamba Maungo na Galagaja walikutwa wakimuuzia nyama Maango Kitwana Rajabu kwa kutumia jiwe la kilo mbili lenye upungufu wa uzito wa gramu 450.
Mwendesha Mashtaka alidai zaidi kuwa kwa kuuza nyama ambayo haikufikia uzito unaotakiwa, walitenda kosa kinyume cha vifungu Na 35 (i), 51 (i) na 45 (i) vya Sheria Na 20 ya Vipimo ya mwaka 1982.
Washtakiwa wote wawili walikana mashtaka dhidi yao na wamerudishwa rumande baada ya kukosa wadhamini hadi Novemba 29, kesi hiyo itakapotajwa tena. Upelelezi wa kesi hiyo unaendelea.
Kwa mujibu wa kifungu Na 45 cha Sheria hiyo, washtakiwa wanaweza kutozwa faini ya Sh10,000 au kifungo cha miaka mitatu jela ikiwa itathibitishwa na mahakama kwamba wametenda kosa hilo.