Na Mwandishi Wetu, TSJ
TANZANIA ni miongoni mwa mataifa 30 duniani yaliyo nyuma katika kufikiaji malengo ya kuwaendeleza watu wake.
Kwa mujibu wa ripoti iliyozinduliwa nchini jana na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Tanzania imeshika nafasi ya 162 kati ya mataifa yote 177 duniani ikiwa ni ya mwisho kwa nchi za Afrika Mashariki.
Ripoti hiyo imezingatia vigezo muhimu vitatu katika kupima ufanisi wa mataifa hayo 177, ikiwemo umri wa kuishi, kufikia malengo ya kielimu na kipato cha mtu mmoja mmoja.?
Ripoti hiyo imegawanya mataifa hayo katika makundi matatu ambapo yapo yale yanayofanya vizuri zaidi, yaliyofanya wastani na yale ambayo hayakufanya vizuri kabisa.
Katika nchi za Afrika Mashariki, Tanzania na Kenya zipo katika kundi la nchi 31 zilizofanya vibaya zaidi zikiwa zimeshika nafasi ya 162 na 152 kati ya mataifa 177. Uganda ipo kati kundi la kati ikiwa imeshika namba 145.
Katika kundi la mataifa yaliyofanikiwa zaidi nchi ya Afrika iliyofanikiwa zaidi ni Seychelles (47) na Mauritius (63).
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mataifa kama Norway, Iceland na Australia ndiyo yaliyoongoza wakati Mali, Sierra Leone na Niger zikiwa zimeshika mkia.
Akizungumza katika uzinduzi wa ripoti hiyo Mwakilishi wa Shirika hilo nchini, Oscar Taranco, alisema ingawa Tanzania imeonekana kufanya vibaya, lakini kuna mabadiliko makubwa katika kuhakikisha maendeleo ya watu yanapatikana.
Akilinganisha ripoti ya mwaka huu na miaka mitatu iliyopita tangu mwaka 2003, Taranco alisema kumekuwa na mafanikio kuliko ilivyokuwa awali.“Uchambuzi wa ripoti ya mwaka huu unaonyesha kwamba kuporomoka kwa kipimo cha maendeleo ya binadamu (HDI), ambacho ni muhtasari wa vipimo vitatu; umri wa kuishi duniani, kuelimika na kiwango cha maisha kumepungua," alisema.
Alisema wao kama UNDP wanavutiwa na mafanikio na utekelezaji wa mipango ya kibunifu iliyotokana na Watanzania wenyewe mfano Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umasikini (Mkukuta) ambao bila shaka utasaidia kufikia malengo ya milenia.Tangu kuanza kuchapishwa kwa ripoti hiyo mwaka 1990 , imesaidia kubadilisha falsafa na dhana ya maendeleo.
Na kwa kipindi chote hicho, ripoti hiyo imewezesha kugundua masuala muhimu ambayo huko nyuma hayakuwa yakichukuliwa kama ni vigezo muhimu katika maendeleo ya binadamu.Ripoti hiyo kwa mara ya kwanza ilizinduliwa Cape Town Afrika Kusini, na kwa hapa nchini jana ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kuzinduliwa.Ujumbe wa mwaka huu ulikuwa ni ‘mapambano dhidi ya upungufu wa nishati, umasikini na tatizo la maji’.
Akizindua ripoti hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, aliutaka Umoja wa Mataifa kuendelea kuisaidia serikali katika mikakati yake kama ule wa dharura wa kukabiliana na mmomonyoko wa ardhi na uharibifu wa vyanzo vya maji ili kulisaidia taifa litekeleze malengo yake ya mkukuta na ya milenia