Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Meli za mafuta zaidaiwa kuingiaTanzania bila vibali
http://www.habaritanzania.com/articles/1865/1/Meli-za-mafuta-zaidaiwa-kuingiaTanzania-bila-vibali
By Ramadhan Semtawa
Published on 11/17/2006
 
NAIBU Waziri wa Miundombinu, Dk Maua Daftari jana alifanya ziara ya ghafla katika Bandari ya Dar es Salaam na kubaini kwamba kuna meli mbili za mafuta zilizoingia nchini zikiwa hazina nyaraka za maelezo wala kuagizwa na wakala yeyote.

Na Ramadhan Semtawa
NAIBU Waziri wa Miundombinu, Dk Maua Daftari jana alifanya ziara ya ghafla katika Bandari ya Dar es Salaam na kubaini kwamba kuna meli mbili za mafuta zilizoingia nchini zikiwa hazina nyaraka za maelezo wala kuagizwa na wakala yeyote.

Vyanzo vya habari vimelieleza Mwananchi kuwa kuna uwezekano wa meli hizo kujihusisha na biashara ya magendo ya mafuta.Alipoulizwa kuhusiana na ziara yake ta ghafla, Dk Daftari alisema, "Ngoja nikupe mpya, leo tumekwenda kweli bandarini, lakini tumekuta kuna meli hazina nyaraka na nyingine zina mafuta lakini hazina order (hazijaagizwa), ndiyo maana haziruhusiwa kuingia katika gati," alifafanua Dk Daftari.

Dk Dfatri alisema meli hizo ambazo hazina nyaraka, haziwezi kuingia katika eneo la gati ya kupakulia mafuta hadi hapo zitakapoonyesha vielelezo hivyo, ikiwa ni pamoja na ukubwa wa meli, aina ya bidhaa ilizobeba na zilikotoka.Alifafanua kwamba, taratibu za bandari haziruhusu meli kuingia katika eneo la gati kama hazina nyaraka wala kukamilisha taratibu zinazohusika.

Naibu waziri alisema tangu walipofika na kuondoka mchana, kulikuwa na meli tano ambazo ni pamoja na hizo zisizo na nyaraka na nyingine zilizokuwa zikikamilisha taratibu.Alisema meli moja iliyofahamika kwa jina la Hulda, ambayo ilikuwa katika hatua za mwisho za kukamilisha taratibu wa kupakua mzigo, ilikuwa tayari imeanza kuingia kwenye gati kwa ajili ya kupakua shehena yake ya mafuta.

Hata hivyo, Dk Daftari hakuweza kutaja majina ya meli zilizokosa nyaraka na zilizokuwa zikikamilisha taratibu za nyaraka, lakini alitaja baadhi ya majina ya meli zilizokuwa katika foleni kwamba ni pamoja na Hulda na Alexander.Alisema meli hizo zilizokuwepo zilikuwa na uzito wa wastani wa tani 22, 20 na 13 za mafuta lakini akasema pia haikuwa rahisi kueleza kila moja ilikuwa katika kundi lipi.Kutokana na hali hiyo, Dk Daftari, ameiagiza Mamlaka ya Bandari (TPA) kutoa taarifa sahihi kwa umma kuhusu hali hiyo.

"Baada ya kuona hali hiyo, nimeagiza bandari itoe taarifa kwa umma kuhusu hali halisi ya bandarini ili kuondoa taarifa za utata, sijaona tatizo kwa upande wa bandari," alisema Dk Daftari. Kuhusu uwezekano wa meli hizo kujihusisha na biashara za magendo ya mafuta, Dk Daftari alisema hilo ni moja ya maagizo aliyotoa kwa Mamlaka ya Bandari kulifanyia kazi ili kubaini kama kuna ukweli wowote."Nimewaambia TPA wasilichukulie kama suala jepesi, nimewaambia walifanyie kazi na kesho nitaviarifu vyombo vya ulinzi visiwani, kikiwemo kikosi maalum cha kuzuia magendo (KMKM) na Marine ili kufanya doria na uchunguzi zaidi," alisema.

Alisema upo uwezekano wa meli kwa meli kuuziana mafuta katika bahari kuu, jambo ambalo linaweza kuharibu mazingira ya bahari. "Watu wanafanya biashara ya mafuta kama ya daladala, kwa nini wasiuze huko kwao badala yake waje huku kutuchafulia bahari yetu," alilalamika Dk. Daftari.Hatua ya Naibu Waziri akifuatana na Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Omary Chambo, kufanya ziara hiyo, imekuja siku chache baada ya kuwepo taarifa za msongamano wa meli zinazosubiri kupakua mafuta. Chanzo kingine cha habari kutoka bandari ya Dar es Salaam, kilisema meli hizo ambazo hazina wakala, zimekuwa zikileta shehena zikitegemea kuuza kwa wateja ambao zitawapata zikiwa nchini.

"Unajua hili ni soko huria, kuna meli zinakuja bila order, wenyewe wanajua wakija hapa watauza, huwezi kuwakataza, lakini haziwezi kuingia katika gati," kilidokeza chanzo hicho.Kwa mujibu wa chanzo hicho, meli hizo zimekuwa zikionekana kama zinazocheleweshwa kupakua shehena lakini kumbe zimekuwa hazifuati taratibu za mamlaka.Meneja Uhusiano wa TPA, Franklin Mziray, aliliambia gazeti hili kwamba, mamlaka hiyo ingetoa taarifa sahihi kuhusu suala hilo kuanzia leo.

Asubuhi Mwananchi ilifika Makao Makuu ya TPA na bandari ya Dar es Salaam na kudokezwa kwamba, viongozi wote wa ngazi za juu wa maeneo hayo mawili walikuwa katika mikutano mirefu ya kujadili sakata hilo kabla ya Dk Daftari hajafika."DG (Mkurugenzi Mkuu, Ephraim Mgawe), Meneja wa Bandari (Jason Rugaihuruza) wako katika mkutano nafikiri unaweza kuchukua saa mbili hadi tatu," kilidokeza chanzo hicho