Nipe kinasa sauti, mheshimiwa spika,
Ninajambo nalo nyeti, napenda kulitamka,
Vuteni viti mketi, wajumbe mliofika,
Viongozi kama wapo, basi hawa wapo wapo!!
Ametamka Lowassa, kwa mashairi bungeni,
Beti nne zikapasa, malenga akazighani,
Viongozi wapo hasa, wenye sifa kama nini,
Viongozi kama wapo, basi hawa wapo wapo!!
Kanipandisha hasira, mkono wanitetema,
Ningekuwa na bakora, angeona cha mtema,
Sitaki miye hasara, ya Dito si mambo mema,
Viongozi kama wapo, basi hawa wapo wapo!!
Mikataba ya madini, ni nani aliingia,
Huyo kiongozi gani, sahihi kaimwagia,
Adhabu yake ni nini, Lowassa twaulizia,
Viongozi kama wapo, basi hawa wapo wapo!!!
Ati leo twaambiwa, mikataba yachunguzwa,
Hoja ikashangiliwa, kumbe nchi imeuzwa,
Migao ikagawiwa, vipi hao wamefunzwa,
Viongozi kama wapo, basi hawa wapo wapo!
Mikataba ya umeme, ya Songa na Richimondi,
Lowassa sasa useme, kiongozi yupi fundi,
Hatua gani useme, kafukuzwa kwenye kundi?
Viongozi kama wapo, basi hawa wapo wapo!!
Mapesa mabilioni,yamepotea kijanja,
Walokula ni nani, kama si hao viranja,
Idara na wizarani, kwa upole wazikunja,
Viongozi kama wapo, basi hawa wapo wapo!!
Leo sifa wamwagiwa, waitwa waadilifu,
Makofi wanapigiwa, wadhani sisi vipofu,
Pochi hawa wakatiwa, wajichana bila khofu,
Viongozi kama wapo, basi hawa wapo wapo!!
Anayetaka tukana, tusi huyo hachagui,
Lowassa katutukana, kama siye hatujui,
Viongozi twawakana, tuko macho kama chui,
Viongozi kama wapo, basi hawa wapo wapo!
Napenda kutoa hoja!!!
Nisikilize: http//mwanakijiji.podomatic.com