Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Mzee Mwanakijiji  »  Lowassa twataka jibu!!
Lowassa twataka jibu!!
By Mzee Mwanakijiji | Published  11/17/2006 | Mzee Mwanakijiji | Rating:
Viongozi kama Wapo!

Nipe kinasa sauti, mheshimiwa spika,
Ninajambo nalo nyeti, napenda kulitamka,
Vuteni viti mketi, wajumbe mliofika,
Viongozi kama wapo, basi hawa wapo wapo!!

Ametamka Lowassa, kwa mashairi bungeni,
Beti nne zikapasa, malenga akazighani,
Viongozi wapo hasa, wenye sifa kama nini,
Viongozi kama wapo, basi hawa wapo wapo!!

Kanipandisha hasira, mkono wanitetema,
Ningekuwa na bakora, angeona cha mtema,
Sitaki miye hasara, ya Dito si mambo mema,
Viongozi kama wapo, basi hawa wapo wapo!!

Mikataba ya madini, ni nani aliingia,
Huyo kiongozi gani, sahihi kaimwagia,
Adhabu yake ni nini, Lowassa twaulizia,
Viongozi kama wapo, basi hawa wapo wapo!!!

Ati leo twaambiwa, mikataba yachunguzwa,
Hoja ikashangiliwa, kumbe nchi imeuzwa,
Migao ikagawiwa, vipi hao wamefunzwa,
Viongozi kama wapo, basi hawa wapo wapo!

Mikataba ya umeme, ya Songa na Richimondi,
Lowassa sasa useme, kiongozi yupi fundi,
Hatua gani useme, kafukuzwa kwenye kundi?
Viongozi kama wapo, basi hawa wapo wapo!!

Mapesa mabilioni,yamepotea kijanja,
Walokula ni nani, kama si hao viranja,
Idara na wizarani, kwa upole wazikunja,
Viongozi kama wapo, basi hawa wapo wapo!!

Leo sifa wamwagiwa, waitwa waadilifu,
Makofi wanapigiwa, wadhani sisi vipofu,
Pochi hawa wakatiwa, wajichana bila khofu,
Viongozi kama wapo, basi hawa wapo wapo!!

Anayetaka tukana, tusi huyo hachagui,
Lowassa katutukana, kama siye hatujui,
Viongozi twawakana, tuko macho kama chui,
Viongozi kama wapo, basi hawa wapo wapo!

Napenda kutoa hoja!!!


Nisikilize: http//mwanakijiji.podomatic.com


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by Nthe)
    Rating
    Longa mzee wa shamba

    Shairilo nimesoma, tena nimeburudika,
    Umenena kwa hekima , na wazi umetamka
    nami ni bora nkasema, uwazi tunautaka
    hata waimbe ngonjera, bado hatuwaelewi.

    Umeme kitendawili, nani amewajibika,
    wamezitapanya mali, wazila wanavyotaka,
    majumba ya serikali, wametupa kama taka
    Kikwete atupe jibu,tumechoka na ngonjera.

    Madini walishagawa, hii ya Mkapa kazi,
    kasi mpya itagawa, hili twaliona wazi,
    hawa watu gawa gawa, hii ndiyo yao kazi,
    Kikwete hata Lowassa, jamani tupeni jibu.

    Wala rushwa wanatesa, wanadaka vidagaa,
    nyangumi hawajanasa, wabaki kutahadaa,
    mara nyingi tumeasa,twajua watuhadaa,
    Kikwete tupeni jibu, ngonjera zimetosha.

    Juzi wametuambia, kuwa kuna kazi nzito,
    nguvuni kuwatia, wauza unga vizito,
    mara wanatuambia,wameishavuka mto,
    Wameikimbia nchi, nani wa kulaumiwa?

    Naona mauza uza,urongo umeshamiri,
    umma wameuchuuza, kwa kughani mashairi,
    umma umejituliza,unangoja bila shari,
    Kikwete twaomba jibu, matatizo yamezidi.

    Juzi nilikueleza, kuwahusu wahalifu,
    umma walouumiza, wakaufanya uchafu,
    wenyewe wametuliza, hawana uadilifu,
    wangapi umefukuza wale wakuu wilaya?

    Wale walopiga watu, wakanyanyasa mchana,
    hatuwasamehi katu, hata kama mwajuana,
    kwetu hawa siyo watu, hawana hata maana,
    wale Ma DC wako, Lowassa wangoja nini?

    Tukutajie majina, utadhani huwajui,
    waliyatenda bayana, mchana na asubuhi,
    hebu fanya la maana, tushakupa maudhui,
    Wale Ma DC wako, Lowassa wangoja nini?

    Zirejeshe nyumba zetu, zile mlizogawana,
    kwani hiyo pesa yetu, ndiyo tulichangishana,
    zirejeshe nyumba zetu, hili ndilo la maana,
    maneno yafuatie, tushachoka na maneno.


    Fukuza wabadhilifu, ambao tunawajua,
    wale wenye hitilafu, twajua mnawajua,
    wale walocheza rafu, hakika mnajijua,
    Hebu tufanyie kweli, tumechoka na ngonjera.

    Watuzomea jirani, walonga twalamba buti,
    japo tuna kisirani, hoja yao madhubuti,
    umma uko msambweni, mnaujaza kaputi,
    Kikwete imeshatosha, sasa anza chapa kazi.

    Longa mzee wa shamba, huu ni wajibu wetu,
    Atatulipa Muumba,anayo malipo yetu,
    wananchi twaamba,nanyi msilale katu,
    tusimame tuwabane, hawa wanotudanganya.
     
Submit Comment


Article Options
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Is Tanzania a safe place to invest?
  4. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Linda Garner
  4. Nthelezi Nesaa
  5. Marshy Abdu
  6. Prosper Kwigize
  7. Salehe Mmoro
  8. Ramadhan Semtawa
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.