Jumuiya ya Kiislamu ya Ahmadiyya Muslim Jamaat Tanzania, imetoa wito kwa jamii ya Waislamu nchini kupuuza kauli zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa dini ya Kiislamu za kuwataka kususia vyombo vya habari vya IPP.
Kauli hiyo ilitolewa jana Jijini Dar es Salaam na Kiongozi Mkuu wa Jumuiya hiyo nchini, Amir Alli Said Mosse alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali yanayofanywa na jumuiya yake.
Kiongozi huyo alisema mtu yeyote anayetoa maneno ya uchochezi hana dhamira ya kweli katika kuendeleza Uislamu bali anafanya hivyo kwa maslahi yake binafsi.
’’Sisi hatuko upande wowote bali tunasimama katika misingi ya dini yetu inayotutaka kuwapenda watu wote,’’ alisema.
Alisema ingawa hafuatilii kwa kina masuala ya vyombo vya habari, lakini anajua kuna watu wanatumia misikiti kuwapotosha waumini wao na kupandikiza chuki dhidi ya vyombo vya habari vikiwemo vya IPP kwa madai kuwa haviwatendei haki .
Aliongeza kuwa, kitendo hicho ni cha hatari katika jamii kwa kuwa kinalenga kuigawa na kuifarakanisha jamii ya Watanzania.
Kuhusu shughuli zinazofanywa na jumuiya yake hapa nchini, alisema inajishughulisha kuwasaidia watu wasiokuwa na uwezo, kujenga hospitali na kuendeleza elimu katika ngazi mbalimbali.
Alisema katika kuhakikisha jamii inanufaika na matunda ya jumuiya hiyo, wamejenga hospitali mbili zilizopo mkoani Morogoro na kwamba wanatoa huduma bila kujali dini.
Aliongeza kuwa, shughuli zao zote wanazozifanya kwa jamii hazitegemei wafadhili kutoka nje ya nchi bali kwa kutumia fedha walizonazo ingawa ni kidogo.
Aidha, aliwaasa wanajumuiya hiyo kuwa wavumilivu na wala wasitumie kisingizio chochote katika kuwaangamiza watu wengine kwa kujitoa mhanga.
’’Uislamu ni kitu safi ambacho kimeletwa na Mwenyezi Mungu kwa wanadamu ili kiweze kuwasaidia katika maisha yao,’’ alisema.
Alisema jumuiya yao imetokana na mtu mmoja raia wa India kudai kuwa ametumwa na Mwenyezi Mungu ili kuwaonyesha njia wanadamu wenzake na kwamba wao wanaamini hivyo katika imani zao.
Aliitaka jamii kushirikiana na jamuiya yao katika masuala mbalimbali kwa kuwa ipo katika jamii na wala haina ubaguzi wa dini za watu wengine.
Kiongozi huyo alisema kwa sasa wana matawi 400 nchini kote na kwamba wana tawi kila mkoa.