Na Mwandishi Wetu, Dodoma MKUU wa Mkoa wa Dodoma, William Lukuvi, amesema sekta ya usafiri wa nchi kavu na majini mkoani hapa imegubikwa na matatizo mengi yakiwemo ya watoa huduma ya mabasi ya daladala kutoa huduma isiyoridhisha, ikiwa ni pamoja na kutoa lugha chafu kwa abiria.
Lukuvi alisema hayo jana kwenye mkutano wa wadau wa sekta ya usafiri wa nchi kavu na majini, ulioandaliwa na Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini(Sumatra) na kufanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Alisema kitendo cha watoa huduma ya usafiri, hasa wa mabasi ya daladala kutoa lugha chafu kwa abiria, kuwabughudhi wanafunzi na kutoza nauli wanazotaka, kumesababisha wakazi wa mkoa huo kukata tamaa na usafiri huo.
Alisema hali hiyo imekuwa kukichangiwa na mambo mengi yakiwemo ya miundombinu dhaifu iliyopo katika mkoa huo na utendaji mbaya wa mamlaka na taasisi husika katika kusimamia na kudhibiti watoa huduma ya usafiri.
Alisema tatizo lingine ni elimu ndogo ya haki na wajibu wa watumiaji katika kuboresha huduma za usafiri kama uzembe wa wahudumu na waendesha vyombo vya usafiri, kama vile madereva na makondakta kutofuata sheria za usalama barabarani na ukiukwaji wa sheria za uendeshaji biashara ya usafiri wa abiria.
Alisema mkutano huo wa wadau wa huduma ya usafiri wa majini na nchi kavu kumekuja wakati muafaka ambapo mkoa umepania kupunguza matatizo yanayotokana na huduma ya usafiri isiyoridhisha.
Hata hivyo, alisema hivi sasa mkoa wa huo una mtandao wa barabara wenye jumla ya kilometa 5554.2.