Na Salma Said, Zanzibar
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imepiga marufuku utoaji wa leseni za vileo katika maeneo wanaoishi watu na nyumba za ibada.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ, Suleiman Othman Nyanga aliyasema hayo juzi wakati akizindua mahakama ya vileo ofisini kwake Vuga, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Mahakama ya vileo imeanzishwa maalum visiwani hapa ili kushughulikia na kusimamia vilabu vyote na uendeshaji wake.
Vile vile mahakama hiyo itakuwa inapokea malalamiko ya wananchi juu ya vilabu vilivyofunguliwa maeneo mbalimbali, kutoa maamuzi ya malalamiko hayo na kuangalia nidhamu za vilabu.
Nyanga alisema kumejitokeza malalamiko mengi kuhusu kuwepo kwa vilabu vya pombe karibu na makazi ya wananchi pamoja na nyumba za ibada jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa na wananchi wengi.
“Tuwe waangalifu sana katika suala la utoaji wa leseni za vileo...yapo malalamiko mengi kwamba leseni zinatolewa bila ya kufanya utafiti wa kina,” alisema Nyanga.
Alisema utoaji ovyo wa leseni usiozingatia maadili umekuwa ukileta ufumbufu kwa wananchi katika maeneo yanayokaliwa na watu.
Alisema mara nyingi wananchi huwa wanavurumishiana maneno ya ovyo jambo ambalo huzusha malalamiko mengi na wakati mwengine ugomvi wa mara kwa mara kati ya wamiliki wa baa na jirani zao.
Alisema utoaji wa leseni za vileo katika makazi ya wananchi husababisha kuvuruga maadili ya vijana, utamaduni na kuchochea vitendo vya kihuni.
Mwenyekiti wa Mahakama ya Vileo, Abdulrazak Abdulkadir, alisema mahakama yake itakuwa makini katika utoaji wa leseni kwa wamiliki wa baa hizo.
Alisema jambo la kwanza watakaloangalia ni mazingira ya mahali panapotaka kufunguliwa baa, na kwamba endapo ni sehemu iliyo karibu na msikiti au kanisa, hawatatoa kibali.