Na Mpoki Bukuku
RAIS Jakaya Kikwete juzi alilazimika kukiri udhaifu wa ahadi ya aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Basil Mramba ya kukamilisha ujenzi wa sehemu ya barabara ya Sam Nujoma Novemba mwaka huu.
Akizungumza katika uzinduzi wa jengo jipya la biashara la Milimani City jijini Dar es Salaam juzi, Rais Kikwete alikiri kutotimia kwa ahadi hiyo na kuwa waziri aliyepo sasa ameomba miezi miwili zaidi ili kuitimiza.
"Bahati mbaya ahadi yetu ya kukamilika kwa barabara hii mwezi huu wa Novemba haikuwezekana. Nimeonana na Waziri mhusika, Andrew Chenge akiwa na Katibu Mkuu wake leo asubuhi, wamekiri upungufu na kuahidi kuwa wanahitaji miezi miwili zaidi kutimiza ahadi yao ya Julai," alisema Rais Kikwete na kuongeza:
"Tuwape nafasi nyingine, najua watakamilisha kama walivyoahidi," alisema na kuahidi kuwa kukamilika kwa barabara hiyo, kutarahisisha wateja kuweza kufika katika eneo hilo lenye maduka ya kisasa.
Mramba aliyekuwa anaongoza wizara hiyo kabla ya mabadiliko ya hivi karibuni, aliahidi mbele ya Rais Kikwete Julai mwaka huu kuwa barabara hiyo ingekuwa imekamilika kwa kiwango cha lami umbali wa km1.5 kutoka Mwenge ifikapo Novemba.
Ahadi hiyo ya Mramba ilifuatia malalamiko ya uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuwa kuchelewa kwa ujenzi wa barabara hiyo, kunakwamisha ukamilishaji wa mradi wa Mlimani City, na hivyo Rais Kikwete kumtaka Mramba aeleze ni lini mradi huo ungekamilika.
Pamoja na mapungufu hayo ya barabara, Rais Kikwete aliwapongeza wawekezaji katika mradi huo kuwa huo ni ushirikiano mzuri kati ya sekta binafsi na serikali na kuahidi kwamba serikali inabakia na jukumu la kufanya mambo ya msingi ya utawala, ulinzi na usalama, kutoa huduma za msingi za kiuchumi na kijamii, hususan miundombinu na mazingira mazuri kwa uchumi kukua na sekta binafsi kustawi.
Aliwahakikishia wawekezaji hao kuwa mradi huo mbali ya kufanya watu kupata bidhaa zenye ubora utakuwa kivutio kwa kutembelea kwani kutakuwa na kila aina ya burudani kwa familia.
Hivyo alisema serikali itahakikisha kuwa huduma ya umeme na maji itapatikana mahali hapo na kwamba matatizo yaliyopo kwa sasa ni ya muda mfupi.
Kabla ya kuzindua rasmi Rais alitembelea maduka mbalimbali yaliyoko kwenye jengo hilo ambapo alipongeza duka la Shoprite kwa kuuza bidhaa za nchini na kuwataka wawekezaji wengine kuiga mfano huo.
"Nimefurahi kuona Shoprite wakiuza bidhaa za Tanzania, hii ni nzuri kwani inawasaidia wazalishaji wa ndani kupata masoko ya bidhaa zao, naomba na wawekezaji wengine wafanye hivyo ili kuinua uchumi," alisema.
Awali akielezea mradi huo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaa, Prof Matthew Luhanga, alisema katika mpango wa mradi huo sehemu hiyo itakuwa na hoteli kubwa na vyumba 100, ukumbi wa mikutanoi wa kuchukua watu zaidi ya 1000, maofisi na maduka pia hifadhi ya wanyama (zoo) na maegesho y amagari yenye uwezo wa magari 2,100