Na Mussa Juma, Arusha.
POLISI mkoani hapa, inamshikilia mmiliki wa gari la abiria maarufu kama kifodi(daladala), ambalo dereva na kondakta wake ndio waliomjeruhi kwa sime askari wa usalama barabarani baada ya kuwakamata.
Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Matei Basilio alimweleza mwandishi wa habari hii kuwa mmiliki wa basi hilo linalofanya safari kati ya Stendi ya Arusha na Kikatiti, wilayani Arumeru, ni mkazi wa eneo la Makao Mapya jijini hapa.
Kamanda Basilio alisema, wanamshikilia mmiliki huyo ili awasaidie kukamatwa kwa dereva wa gari lake, aliyekimbia mara baada ya kumcharaza na sime askari PC Hamad.
Alisema dereva huyo ni mkazi wa eneo la Ngulelo jijini hapa, ambapo jitihada za kumkamata zinaendelea, kwani hadi jana alikuwa hajaonekana.
"Vijana wangu walikwenda hadi nyumbani kwake usiku wa manane lakini hakulala nyumbani, hivyo tutaendelea kumshikilia Mnaro hadi apatikane dereva wake," alisema Basilio.
Kuhusu kondakta wa gari hilo alisema, mmiliki wa gari hilo, alidai hamjuwi kwa maelezo kuwa, alitafutwa na dereva na hivyo naye bado anasakwa ili afikishwe katika vyombo vya sheria.
Dereva na kondakta wa basi hilo walimcharaza kwa sime askari wa usalama barabarani PC Hamad na kumjeruhi vibaya bega la kulia na kifuani.
Tukio hilo lilitokea katika barabara ya Chaga jijini hapa.
Hata hivyo, PC Hamad aliruhusiwa juzi hospitali baada ya kupatiwa matibabu na hadi jana hali yake ilikuwa ikiendelea vizuri.
Tukio la kushambuliwa kwa sime askari huyo limekuwa gumzo kubwa jijini hapa, ambapo makundi ya madereva na watu mbalimbali walikuwa wakijadili na baadhi yao walitoa wito kuwepo vikao vya mara kwa mara vya madereva na askari wa usalama barabarani.
Wakari huo huo, Umoja wa Madereva Mkoa wa Arusha, (UMMA) umelaani kitendo cha dereva na kondakta wake, kumjeruhi kwa sime askari wa usalama barabarani.