Na Abdallah Bawazir, Dodoma
WABUNGE wameupongeza Muswada wa Sheria ya Udhibiti wa Biashara ya Fedha Haramu kuwa umekuja wakati muafaka kutokana na mazingira ya sasa ya kiuchumi na kibiashara, lakini wameonyesha wasiwasi wao juu ya utekelezaji wa sheria hiyo.
Wakichangia maoni yao juu ya muswada huo uliowasilishwa bungeni na Naibu Waziri wa Fedha, Abdisalam Issa Khatib mjini hapa jana, baadhi ya wabunge, waliishutumu serikali kuwa imekuwa ikizembea kutekeleza sheria mbalimbali zinazopitishwa na Bunge.
Walisema kutokana na hali hiyo, baadhi ya mambo yanafanywa kama mazoea na wakaipa changamoto kuhakikisha kuwa sheria hiyo mpya inatekelezwa ipasavyo na kuwagusa watu wote bila ya kujali nyadhifa zao serikalini, uwezo wa kifedha na umaarufu wa mtu.
Walisema tatizo la fedha haramu linaleta athari kubwa kwa uchumi wa nchi, lakini serikali imekuwa haichukui hatua zozote kukabiliana nalo.
Kwa mujibu wa muswada huo, shughuli zote zinazohusisha fedha haramu ni makosa kuanzia masuala ya rushwa, biashara ya dawa za kulevya, ukahaba, uhalifu, kughushi, nyaraka na ugaidi.
Katika maoni yaliyotolewa na kambi ya upinzani bungeni ambayo yalisomwa na Halima Mdee (Chadema), kambi hiyo ilitaka kuwepo na dhamira ya dhati ya serikali katika kuitekeleza sheria hiyo.
"Hivi kweli kuna nia na utashi wa kisiasa wa kuitekeleza sheria hii au ni kutekeleza tu matakwa ya wakubwa! Sheria hii inaenda sambamba na vita dhidi ya rushwa, je wenye mali kubwa kuliko vipato vyao, wanaochangia fedha nyingi katika harambee za kisiasa fedha wamezipata wapi kama siyo fedha haramu?" aliohoji Halima.
Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, katika maoni yake, yaliyosomwa na Mbunge wa Mkuranga, Adam Malima, ilionyesha wasiwasi katika utekelezaji wa sheria hiyo, hasa pale wahalifu wanapoingiza fedha zao walizopata kwa njia haramu katika miradi inayogusa maslahi ya wananchi.
"Utekelezaji wa sheria hii unaweza kuwa mgumu kama tusipokuwa makini, wahalifu wanaweza kuingiza fedha chafu katika miradi inayogusa maslahi ya wananchi, hapa inawaeza kuwa vigumu kukabiliana nao kwani wananchi hawataelewa kwa kuwa watakuwa wananufaika na miradi hiyo," alisema Malima.
Kamati hiyo pia iliikosoa sheria hiyo kuwa hamlindi mtu anayetoa taarifa juu ya watu wanaofanya shughuli haramu na ikapendekeza kiongezwe kufungu cha sheria kitakacho mlinda mtoa taarifa ili watu wasihofu kufichua wahalifu.
Mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakiembe (CCM), alitaka watu watakaopewa jukumu la kusimamia sheria hiyo waweke uzalendo na maslahi ya taifa mbele na kuepuka kutumiwa na wahalifu ili wafumbie macho vitendo hivyo.
Pia alishauri watoa taarifa vikiwemo vyombo vya habari vilindwe pindi vinapotoa taarifa au kuripoti habari zinazohusu wahalifu wa namna hiyo.
Awali akisoma muswada huo wa sheria mbele ya wabunge, Khatib, alisema biashara ya fedha haramu ni tishio la usalama wa nchi, kwani hudhoofisha mfumo wa uchumi na huyumbisha serikali kwa kununua viongozi walioko madarakani.
Alisema madhumuni ya muswada huo ni kupendekeza kutungwa sheria madhubuti yenye kuzingatia viwango vya kimataifa vya udhibiti wa biashara ya fedha haramu kwa kuharamisha mapato na mali zote zinazotokana na biashara na vitendo vya kihalifu.