Na Muhibu Said
WAKATI uingizaji wa nguruwe na mazao yake ukiwa umepigwa marufuku visiwani Zanzibar kwa kuhofia mafua ya ndege, wakazi wa Tanzania Bara wameondolewa wasiwasi huo kwa kuwa hakuna tishio la namna hiyo.Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Maendeleo ya Mifugo, Dk Peter Njau, aliliambia Mwananchi jijini Dar es Salaam jana, kuwa hakuna sababu yoyote kwa watumiaji wa nguruwe kuhofu kutumia nyama hiyo kwa kuwa tishio la mafua ya ndege halipo kwa wanyama wala ndege Tanzania Bara.
"Sisi hapa hatuna ugonjwa huo si kwa nguruwe tu, bali kwa mnyama na ndege yeyote," alisema Dk Njau ambaye pia ni mtaalamu wa mifugo katika wizara hiyo.
Kuhusu taarifa za kupigwa marufuku uingizaji wa mnyama huyo visiwani humo, Dk Njau, alikiri kuzisikia na kusema kuwa:"Nafikiri hilo ni tishio tu, kwa nini iwe nguruwe tu, isiwe kuku, ng'ombe au mbuzi? Huo ugonjwa hatujauona. Sidhani kama kuna sababu ya kutishia wananchi."Hivyo, Dk Njau, aliwataka watumiaji wa mnyama huyo kutokuwa na hofu kuendelea kutumia na kusema kuwa iwapo ugonjwa huo ungethibitika kuwapo nchini, serikali isingesita kuutangazia umma.
Naye Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Mifugo, Catherine Joseph, alisema juzi kuwa wakurugenzi wa wizara hiyo walikutana, lakini suala hilo halikujitokeza katika kikao hicho.Hata hivyo, Catherine ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Mipango wa wizara hiyo, alisema iwapo kungekuwapo na tishio la ugonjwa huo nchini, serikali isingesita kuwajulisha wananchi.Mapema, Afisa Mawasiliano wa Wizara ya Afya, Nsachris Mwamwaja, alisema wizara yake haina taarifa za kuwapo kwa tishio la ugonjwa wa mafua ya ndege Tanzania Bara na kumtaka mwandishi kufuatilia suala hilo Wizara ya Maendeleo ya Mifugo.
"Hilo nafikiri ni la huko huko Zanzibar, kama lingekuwapo huku tungetoa taarifa kwa wananchi," alisema Mwamwaja.Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kutangaza kupiga marufuku uingizaji wa nguruwe na mazao yake visiwani humo katika kile kilichoelezwa kuwa ni tishio la ugonjwa wa mafua ya ndege.
Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Mafua ya Ndege cha SMZ, Dk Ali Rabia, alisema nguruwe, kama walivyo jamii ya ndege pamoja na kuku, wapo katika orodha ya mifugo ambayo inatajwa kuwa inaweza kusambaza virusi vya mafua ya ndege. "Kutokana na kuwepo kwa hatari ya kuenea kwa mafua ya ndege, tumepiga marufuku uingizaji wa nguruwe pamoja na nyama yake kutoka sehemu zote nje ya visiwa hivi," alisema afisa huyo katika semina ya siku moja na waandishi wa habari juu ya hatari ya ugonjwa wa mafua ya ndege.Dk Rabia, alisema nguruwe anaweza kuathirika na virusi vya mafua ya ndege kama vitakuwa vimeshambulia jamii ya kuku na kumpata yeye kirahisi kwa kuchanganyika na mafua yake.Hatua ya serikali imekuja baada ya Zanzibar kuwa moja ya sehemu ambazo matumizi ya nyama ya nguruwe ni makubwa, hasa kutokana na kasi ya kuongezeka kwa hoteli za kitalii.
Ufugaji wa nguruwe Zanzibar umekuwa unaongezeka siku za karibuni katika maeneo mbalimbali kutokana na nyama hiyo kuuzwa kwa wingi katika hoteli za kitalii.Mbali na nguruwe, tayari SMZ imepiga marufuku uingizaji wa aina yote ya jamii ya ndege, ikiwemo kuku na mayai kama moja ya hatua za kukabiliana na maradhi hayo.Hivi karibuni, SMZ kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Maliasili, iliteketeza kwa moto mayai zaidi ya 60,000 ya wafanyabishara wa visiwani hapa, yenye thamani ya zaidi ya Sh6 millioni ambayo huingizwa Zanzibar kutoka Tanzania Bara.